UONGOZI wa Kiwanda cha Kutengeneza Nguo cha Sunflag, kilichopo mkoani Arusha, kimeeleza kuwa na uwezo wa kuzalisha sare za majeshi na shule nchini baada ya kuongeza uwezo, mitambo na ujuzi wa wataalamu wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).
Haroun Mahundi, meneja uzalishaji wa kiwanda hicho amemweleza Angellah Kairuki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji.
Amesema, awali walipewa zabuni za kutengeneza sare hizo lakini baadaye ziliondolewa bila taarifa na kwamba, kiwanda hicho katika miaka ya hivi karibuni, kimeongeza uwezo maradufu wa uzalishaji kuanzia hatua ya kutengeneza nyuzi kwa kutumia pamba, vitambaa vya aina mbalimbali na nguo zinazouzwa ndani na nje ya nchi.
“Tuna uwezo wa kutengeneza nguo za aina mbalimbali na sare kwa majeshi yote kwa viwango vya juu, ni vizuri kiwanda hiki kitumike kikamilifu kuipunguzia serikali gharama ya kuagiza nje ya nchi,” amesema Mahundi.
Waziri Kairuki baada ya kutembelea idara mbalimbali za kiwanda hicho, aliridhishwa na uwezo wake na kuahidi serikali ipo tayari kushirikiana na mwekezaji kutatua changamoto zinazowakabili ili kuongeza tija.
Amesema, mpango wa Serikali ya Awamu ya tano ni kujadiliana na wawekezaji ili kushughulikia changamoto zinakwamisha uwekezaji katika maeneo mengi, ikiwemo sekta ya viwanda ambayo inatoa ajira kwa vijana wengi na kuitangaza nchi kupitia bidhaa zinazozalishwa.
Amesema, hatua ya asilimia 50 ya nguo zinazozalishwa, kuuzwa nchini ni mafanikio muhimu yanayoonesha wananchi kwamba wamejenga utamaduni wa kununua bidhaa zenye viwango vya juu kutokana na uchumi kuimarika.
Amesema, siku za nyuma asilimia 70 ya nguo zilikua zikiuzwa nje ya nchi huku 30 ikibaki nchini.
Saumumhilu34@gmail.com