Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Sukari yaendelea kuadimika
Habari Mchanganyiko

Sukari yaendelea kuadimika

Sukari
Spread the love

KUADIMIKA kwa bidhaa ya sukari katika baadhi ya maeneo Dar es Salaam nchini Tanzania, kumeendelea kuathiri wakazi na wafanyabiashara jijini humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Upatikanaji wa bidhaa ya sukari ulianza kusua sua katikati ya mwezi Machi 2020, baada ya Serikali kutangaza uwepo wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosabishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Ambapo baadhi ya maeneo nchini sukari ilikuwa inanunuliwa kwa wingi na kusababisha kupanda bei, kufuatia hofu ya baadhi ya watu,  kwamba serikali inaweza kuzuia watu kutoka nje (Lockdown), ili kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

Katika kipindi hicho, sukari ilipanda bei kutoka Sh. 2,400 kwa kilo moja, katika baadhi ya maeneo hadi kufikia Sh. 4,000, hali iliyosababisha Serikali kupanga bei elekezi kwa kila mikoa huku Dar es Salaam ikiwa ni Sh. 2600.

Licha ya Serikali kupanga bei elekezi, lakini bei ya sukari imepanda hadi kufikia Sh. 4,000 kwa kilo, kwenye baadhi ya maeneo.

Kufuatia changamoto hiyo, MwanaHALISI Online leo Jumatano tarehe 13 Mei 2020, ilitembelea baadhi ya maduka jijini humo, kwa ajili ya kufahamu hali halisi juu ya upatikanaji wa sukari na bei yake.

Godfrey Simba, mfanyabiashara wa duka la chakula maeneo ya Kinondoni Vijana amesema, bidhaa hiyo imekuwa adimu, kutokana na kutopatikana kwa urahisi katika maduka ya jumla.

Simba amesema, hata sukari hiyo ikipatikana, bei yake huwa kubwa, ikilinganishwa na bei elekezi iliyotolewa na serikali, ya Sh. 2,800 kwa kilo moja, hali inayosababisha kutonunua ili kukwepa hasara na au kuingia matatni pindi atakapolazimisha kuuza bei zaidi ya iliyopangwa na mamlaka husika.

“Mara ya mwisho kuwa na sukari sikumbuki, ila nina uhakika kama wiki mbili imepita sina sukari. Kwa sababu haipatikani katika maduka ya jumla. Nimeenda maduka ya jumla yaliyoko Mwananyama, Kinondoni  Studio na Manzese, lakini hakuna,” amesema Simba na kuongeza:

“Wauzaji wa maduka ya jumla wenyewe wanasema sukari imekuwa shida upatikanaji wake, hata zikipatikana huuzwa kwa bei juu, mimi siwezi kununua kg 50  za sukari kwa Sh. 140,000. Ambayo ni sawa na Sh 2,800 kwa kg 1 kwa bei ya jumla,  wakati bei elekezi ikiwa ni 2,600. Hautapata faida.”

Ally Masoud Ally, mfanyabishara wa duka la vyakula maeneo ya Manzese Bakhresa, amesema upatikanaji umekuwa adimu, hali inayoathiri wananchi hususan waumini wa dini ya Kiislamu ambao wako katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ally amesema Waislamu wengi huitumia bidhaa hiyo kwa ajili ya kutengenezea futari, lakini uadimikaji wake, unawaathiri.

“Kuna duka moja huwa nina nunua sukari, lakini ikiletwa leo basi ikiisha, inapita siku mbili ndio wanaleta tena, na kuipata kwake hadi uwe unajulikana.”

“Licha ya upatikanaji wake kuwa mgumu na kuwa na gharama kubwa, lakini siachi kuiuza kwa bei elekezi ya Sh. 2,800 ili kusaidia Waislamu wenzangu,” amesema Ally.

Karimu Shakibu, mfanyabiashara wa ubuyu, amesema biashara yake inayumba kwa kuwa, hulazimika kutotengeneza ubuyu kutokana na uhaba wa sukari, ambayo ni kiungo muhimu kwa bidhaa hiyo.

Shakibu amesema, anaamini bidhaa hiyo itaanza kupatikana hivi karibuni, baada ya serikali kuchukua hatua ya kuagiza sukari nyingi nje ya nchi.

Jana Jumanne tarehe 12 Mei 2020, Japheti Hasunga, waziri wa kilimo,  wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni jijini Dodoma, alisema bidhaa hiyo imeadimika kutokana na janga la mlipuko wa ugonjwa Covid-19,  pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu, kuficha sukari.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri Hasunga alisema serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari tani 40,000 kutoka nje ya nchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

DAWASA waanza utekelezaji agizo la Samia

Spread the loveMamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam...

Habari MchanganyikoKimataifa

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the loveTUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais wa...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

error: Content is protected !!