Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Spika Ndugai azidi kumng’ng’ania CAG
Habari za SiasaTangulizi

Spika Ndugai azidi kumng’ng’ania CAG

Spread the love

JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri, amezidi kuchochea mgogoro wa kikatiba unaofukuta sasa, kati ya Bunge na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Dodoma, kiongozi huyo mkuu wa mhimili wa Bunge, “ameipiga marufuku,” baadhi ya kamati za kudumu za Bunge, kufanya kazi na ofisi hiyo.

Taarifa zinasema, katika kuonyesha msuli wake, Spika Ndugai, ameagiza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kutoshiriki kazi zozote zinazohusu ofisi hiyo ya CAG.

Kamati nyingine ambayo “imepigwa pini” kufanya kazi na CAG, ni Kamati ya Hesabu za serikali kuu (POC). Kamati zote hizo mbili zinaongozwa na wabunge wa kambi rasmi ya upinzani.

Kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja wiki moja baada ya Ndugai kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kumtuhumu moja kwa moja, Prof. Mussa Assad – mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali – kudhalilisha Bunge.

Rekodi za Bunge zinaonyesha, ripoti ya kamati hizi mbili zimekuwa mwiba mkuu kwa serikali bungeni na nje ya Bunge. Hii ni kutokana na ripoti zake kuegemea Zaidi uchambuzi wa CAG.

Spika Ndugai aliwaambia waandishi wa habari, kauli aliyoitoa Prof. Assad, akiwa nchini Marekani, kwamba mhimili huo wa kutunga sheria, ni dhaifu na hivyo umekuwa ukishindwa kutimiza wajibu wake, haikubariki. Alisema, ni sharti Bunge litumie kila njia kulinda hadhi yake.

Kufuatia matamshi hayo ambayo Ndugai alidai yanalidhalilisha Bunge, akaagiza Kamati yake ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, kumuita Prof. Asaad ili kumhoji na baadaye kupendekeza hatua za kuchukua.

Kupitia amri hiyo, Prof. Assad, anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo, tarehe 21 Januari 2019. Amesema, iwapo kiongozi huyo atashindwa kutii agizo hilo kwa hiari, “atakamatwa na kupelekwa mbele ya kamati kwa pingu.”

Naye Prof. Asaad akijibu madai hayo ya Spika Ndugai, amenukuliwa akimtaka kiongozi huyo wa Bunge,
kuheshimu katiba na kuwa mfano wa viongozi wanaolinda na kuitetea katiba ya Nchi.

Ofisi ya CAG imetajwa kwenye Ibara ya 143 ya Katiba; hakuna chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, kinachoruhusiwa kuingilia shughuli zake, ispokuwa Mahakama.

“Ni kweli kuwa spika ameagiza kamati zote zinazofanya kazi na CAG kusitisha shughuli zake. Uamuzi huu umechukuliwa kufuatia hatua ya Prof. Assad kutuhumiwa kulitukana na kulidhalilisha Bunge,” anaeleza mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye hakupenda kutajwa jina.

Anasema, kufuatia uamuzi huo, “spika ameamuru” shughuli zote za kamati ya LAAC na POC kufungwa na wajumbe wake kuhamishiwa kwenye kamati nyingine.

Anasema, “sisi tulikuwa na ratiba yetu, lakini ghafla tunaambiwa tumegawanywa vipande vipande kwenye kamati nyingine. Hii maana yake nini? Hivi waziri akikosea kwa mfano, inaadhibiwa wizara yote, kwamba kazi zote zinasimama?”

Mtoa taarifa anasema, kufuatia uamuzi huo wa spika, wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali (POC), waliokuwa wamepanga ziara ya siku saba ya kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma, nao walikatishwa safari yao na kuambiwa kushiriki shughuli za kamati ya Ukimwi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

error: Content is protected !!