JOB Ndugai, Spika wa Bunge, ametoa waraka kwa wabunge wenye muongozo juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa wa Homa ya Kali ya Mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Kwa mujibu wa waraka huo uliotolewa jana tarehe 16 Aprili 2020 na kusomwa bungeni na Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika, wabunge hao wametakiwa kutotoka nje ya Jiji la Dodoma.
Pia, wabunge hao wametakiwa kupunguza mizunguko ndani ya Jiji la Dodoma, huku wakishauriwa kubaki nyumbani kama hawana ratiba za kwenda bungeni.
“Ni muhimu sana kupunguza safari za Dar es Salaam na maeneo mengine kwa ujumla, na hii itasaidia kupunguza hatari ya maambukizi katika taasisi yetu. Kuzingatia umbali wa mtu na mtu, kupunguza mizunguko ndani jiji la Dodoma.
Mheshimiwa spika anawasisitiza mtindo wa nyumbani bungeni na bungeni nyumbani, uwe ndio mwenendo wa maisha kwa wakati huu,” amesema Dk. Tulia wakati akisoma waraka huo.
Wakati huo huo, Dk. Tulia amewashauri wabunge kutenga siku moja maalumu katika wiki, kwa ajili ya manunuzi ya mahitaji ya nyumbani.
“Hata mahitaji ya nyumbani kutoka sokoni, iwe kwa siku maalumu ikiwezekana mara moja kwa wiki, “ amesisitiza Dk. Tulia.
Dk. Tulia amesema hatua hizo zitasaidia taasisi hiyo kutoshambuliwa na ugonjwa wa COVID-19, na kupata nafasi ya kukamilisha jukumu lake la kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2020/21, pamoja na kutunga sheria.
“Sisi kama bunge tunao wajibu wa kuchukua tahadhari zaidi katika kujikinga na ugonjwa wa Corona, ili kukamilisha jukumu muhimu tulilonalo mbele yetu kwa sasa, la kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21 na kutunga sheria,” amesema Dk. Tulia.
Dk. Tulia amewataka wabunge wenye magonjwa sugu kuwa makini katika kujikinga, kwa kuwa wako katika hatari zaidi dhidi ya ugonjwa huo.
“Kulingana na taarifa za wataalamu wa afya, ugonjwa huu una madhara zaidi kwa wazee na watu wenye magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la moyo, pumu, kifua kikuu na saratani. Ni vyema wenye maradhi hayo wakachukua tahadhari zaidi na kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona,” amesema Dk. Tulia na kuongeza:
“Tuepuka kufuatilia na kutazama habari za kuogofya na kujenga hofu kwani hofu inaweza kuongeza msongo wa mawazo, na kuzorotesha afya zetu.”
Leave a comment