Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Spika Ndugai ajuaje moyo wa Rais?
Makala & Uchambuzi

Spika Ndugai ajuaje moyo wa Rais?

Rais John Magufuli (kulia) akiteta jambo na Spika wa Bunge, Job Ndugai
Spread the love

UNAPOTAFAKARI kauli zinazotolewa na Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri kuhusu sakata lake na Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), bila shaka unapata msisimko. Anaandika Jabiri Idrisa … (endelea).

Maelezo ya Spika wa Bunge, Job Ndugai yaliyogusia kuzorota kwa uhusiano wa Bunge na Prof. Assad, yamenionesha hali mbili muhimu.

Ipo hali kuwa, Spika ndio Bunge na Bunge ndio Spika kwa uongozi wa Job Ndugai, huyu wa leo.

Kwamba, kwa hali ilivyo sasa – ya mvutano na kwa kweli ni Spika Ndugai kumjengea Prof. Assad chuki ya kupitiliza kiwango – Bunge haliwezi kurudisha msimamo laini dhidi ya Prof. Assad.

Bunge ni taasisi mhimili inayopaswa kuimarisha uhusiano wa kikazi na Prof. Assad, ambaye ndiye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hata sasa akiwa amefungiwa mlango wa ushirikiano na Bunge.

Spika Ndugai anazidi kuonesha kwamba, Bunge halimhitaji Prof. Assad bali litaendelea kushirikiana na Ofisi ya CAG.

Uhusiano wa kikazi wa pande hizi mbili ni pale CAG anapowasilisha ripoti za ukaguzi wa fedha za umma kila mwaka, na Bunge kuzipitia na kuzijadili ili kutekeleza jukumu lake kuu la kuisimamia serikali katika namna inavyopaswa kutumia fedha zinazotokana na kodi za wananchi.

Akigusia eneo hili katika mazungumzo yake na waandishi wa habari jana tarehe 14 Aprili 2019, jijini Dar es Salaam, Spika Ndugai alisema, ripoti ya ukaguzi haina maamuzi mpaka pale kamati za kudumu za Bunge zitakapoipitia na kubainisha maeneo yenye kasoro.

Baada ya kubainisha maeneo yenye kasoro, Spika Ndugai anasema, kamati huwaita viongozi watendaji wa ofisi husika na kuwataka maelezo ya kusawazisha hizo kasoro.

Na baada ya hapo, ndipo Bunge huamua kwamba, lipo au halipo tatizo la ubadhirifu wa fedha za serikali. Serikali hutakiwa kurekebisha kasoro kwa kuchukua hatua za kiutawala na ikibidi hata za kisheria kwa wahusika.

Maelezo hayo ya Spika Ndugai yanaeleweka haraka kwa jicho pana –kwamba, anaonesha kama vile bila ya Bunge kuingia, ripoti ya ukaguzi haina kubwa. Mtizamo huu sioni kama ni sahihi.

Si sahihi kwa sababu, Spika Ndugai ameona upande mmoja tu wa shilingi – wa umuhimu wa Bunge katika muktadha wa kuisimamia Serikali.

Je, hilo Bunge litafikiaje kuwaita hao viongozi watendaji wa serikali bila ya kuwepo ripoti ya ukaguzi ambayo imeonesha kasoro hii na ile za matumizi ya fedha?

Mfungamano wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Bunge kama taasisi mhimili wa kuisimamia Serikali wala si wa kuku na yai.

Ukweli ni kuwa, kwenye eneo la kuichunga, fedha ya serikali, Bunge huwa tegemezi kwa Mdhibiti na Mkaguzi.

Kazi yake ndio dira ya kiutendaji kwa Bunge. Zile kamati za Bunge hufuatilia yaliyobainishwa na ripoti za ukaguzi. Bunge linamhitaji sana Mdhibiti na Mkaguzi.

Hiyo ni hali ya kwanza. Sasa kuna na hii hali ya pili ambayo kwa maelezo ya jana ya Spika Ndugai, imenijengea hofu fulani kwamba, lipo jambo kubwa zaidi la kutarajiwa kutokea katika kipindi kisichokuwa kirefu cha uhai wa Bunge kabla ya kuvunjwa kwake.

Napata hofu kuwa, yumkini huyu Spika Ndugai ana mawasiliano ya karibu mno na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naona hivi kwa sababu ya kauli ya Spika Ndugai kuwa, Prof. Assad asipoondoka anampa wakati mgumu Rais. Ana maana kuwa, kuna jambo rais anataka kulifanya lakini anakwamishwa na Prof. Assad.

Au kwamba, Rais anafanya jambo fulani – liwe zuri kwa taifa au baya – na kukusudia kuliendeleza lakini kuwepo kwa Prof. Assad kunamzuia.

Hapa pana shida kwelikweli. Kwamba hatujui ni jambo gani hilo analolifanya rais au analotaka kulifanya rais? Ndio. Ni jambo gani hilo?

Maelezo ya Spika Ndugai yanaonesha anaujua moyo wa rais kuhusu nini anachokusudia kufanya kwa taifa au anachokifanya.

Hivi nikiuliza Spika Ndugai anajua zilivyo fikra za Rais John Magufuli, kwa hilo jambo analolifanya au analotaka kulifanya, naweza kupata jibu? Natamani kumuuliza hivi.

Mpaka nitakapopata jibu nabaki na yaleyale tuliyomsikia Rais Magufuli akiyasema hadharani siku ile kwamba; “… wewe washughulikie huko bungeni na wakiwa huku nje nitawashughulikia.”

Mengi yanaonekana kuwasibu wabunge wa upinzani kiasi cha kumfahamisha Mtanzania mwenye akili ya kuona mbali, kutambua kuwa, ni kweli rais ameazimia kutokomeza upinzani ifikapo mwaka 2020.

Ona maandishi ya kumnasibisha Prof. Assad na wabunge makini… tena yanavyomnasibisha profesa pia na viongozi mahiri na makini wa siasa wa upinzani. Na haya maandishi kukuta yanasomeka tu kwenye magazeti ya nyumbani.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!