Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Simulizi msisimko waliofukiwa mgodini 
Habari MchanganyikoTangulizi

Simulizi msisimko waliofukiwa mgodini 

Juhudi za kuokoa wachimbaji wadogo 15 wa madini katika mgodi wa RZ huko Geita zilipokua zikiendelea
Spread the love

MATOPE, magome ya miti pia maji machafu ndivyo vilikuwa vyakula vikuu katika siku tano tulizoishi chini ya kifusi huku hofu ya kupoteza maisha ikitutawala, anaandika Mwandishi Wetu.

Ni kauli ya watu waliookolewa baada ya kufukiwa kwenye mgodi wa dhahabu wa RZ uliopo Nyarugusu mkoani Geita. Wachimbaji hao 15 waliokolewa wote jana wakiwa hai.

Wachimbaji hao wa Kampuni ya RZ walifunikwa na kifusi Jumatano saa nne usiku. Baada ya kufunikwa kwenye kifusi hicho juhudi za kuwaokoa zilianza ambapo ndugu na jamaa walikuwa wakiendesha ibada kuombea ndugu zao.

Matuamini ya waliofukiwa na kufusi chini ya ardhi yalianza kurejea baada ya juhudi za kuwafikishia chakula na vinywaji kule walipo kufanikiwa.

Waokoaji kabla ya kuanza kuwasaka walipo, walifanya juhudi za kupeleka bomba kwa lengo la kusaidia kufikisha chakula laini, maji, biskuti, uji pia dawa na kufanikiwa.

Mgalula Kayanda, mmoja wa wachimbaji 15 waliookolewa kwenye mgodi huo anasema “Biskuti, uji na maji tulivyoshushiwa chini ndio vilirejesha matumaini ya uhai wetu.”

Anaeleza kuwa, kadiri siku zilivyokuwa sikienda ndivyo matumaini yalikuwa yakipotea na kwamba, mmoja kati yao alikuwa amekata kauli kutokana na mazingira, hewa na njaa.

“Baada ya kufikishiwa maji, tulipata nguvu upya na matumaini,” anasema Kayanda na kuongeza “niliamini sitakufa hata nisipotoka leo.”

Akisimulia hali ilivyokuwa Kayanda amesema baada ya kuingia ndani ya mgodi huo saa nne usiku wa Jumatano na kuanza shughuli za uchimbaji, walisikia kishindo na baada ya sekunde chache walisikia sauti za wenzao wakiwataka watoke nje.

“Sauti zilizotoka nje zilituhabarisha kwamba, kulikuwa kunatitia na hapo ndipo kujikusanya sehemu moja.

“Dakika chache baada ya kujikusanya pamoja ghafla umeme ukakatika na hapo giza likatawala huku hewa nayo ikakata sambamba na mawasiliano ya nje,” anasema Kayanda.

Kayanda amesema kwamba, hali hiyo iliwapotezea mwelekeo ambapo walishindwa hata kujua majira kutokana na giza kutawala eneo hilo.

“Baadaye mpira mmoja ukaanza kupitisha hewa,” anasema Kayanda na kwamba, hali hiyo iliwapa matumaini katika hatua za awali “lakini changamoto kubwa ikawa njaa.”

Ndani ya mgodi huo wanaeleza kuwa, changamoto nyingine ilikuwa harufu mbaya iliyotokana na kinyesi walichojisaidia eneo walilojibana kwa pamoja.

“Tulijisaidia pembeni kidogo ya eneo tulilokuwa kutokana na kuwa kwenye mazingira hayo, kwa pembeni kidogo ndio tulikuwa tunakunywa maji yaliyokuwepo mgodini ingawa yalikuwa machafu,” anaeleza Jackson Lucas.

Jana saa 11 asubuhi harakati za kuwafikia watu hao waliokuwa wamefukiwa na kifuzi zilifanikiwa na kuanza kuwatoa mmoja mmoja huku ndugu na jamaa zao wakiwa wanawasubiri. Zilitumika dakika 19 kumaliza kuokoa idadi ya watu 15 waliokuwa wamefukiwa.

Baada ya kuokolewa, madaktari kutoka katika Hospitali ya Waja waliendelea na jukumu la kuwachunguza na kuwapa huduma na kisha kuwapeleka kwenye Hospitali ya Mkoa.

Baada ya uokozi huo Dk. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Meja Jenerali Mstaafu, Elias Kyunga ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Geita waliwaeleza wananchi kwamba, wachimbaji hao wote wameokolewa wakiwa hai.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!