January 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Simba yaipiga Kagera Sugar, yatuma salamu Jangwani

Spread the love

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar. Anaripoti Kelvin Mwaipunga, Dar es Salaam…(endelea).

Simba imeibuka na ushindi huo kwenye mchezo uliochezwa leo Jumatano tarehe 4 Novemba 2020 Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Magoli ya Simba yamefungwa na dakika ya 42 na John Bocco kwa mkwaju wa penati baada ya Hamis Dilunga kuangushwa eneo la hatari.

Goli la pili lilipatikana dakika ya pili kati ya tatu za nyongeza ya kipindi cha kwanza likifungwa na Said Ndemla kwa shuti kali akipokea pasi kutoka kwa Clatous Chama.

Ushindi huo wa pili mfululizo wa Simba, umewafanya kufikisha pointi 19 ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Yanga yenye pointi 23 na Azam FC ikiwa na pointi 22 zote zikiwa zimecheza michezo tisa.

Ushindi huo unawafanya Simba kwenda katika mchezo wao dhidi ya watani Yanga utakaochezwa Jumamosi tarehe 7 Novemba 2020 Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa na molari ya ushindi.

Watani zao, Yanga wenyewe jana walijikuta wakitoka droo na Gwambina FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Gwambina ulkipo Misungwe jijini Mwanza.

Nahodha wa mchezo huo wa Simba, Shomari Kapombe amesema, mchezo ulikuwa mgumu kwani Kagera walikuja wamejiandaa “na sisi tukawa tumejiandaa na ndiyo sababu tumepata ushindi.”

Kuhusu mchezo ujao wa Simba na Yanga, Kapombe amesema “tunajua ni mchezo mkubwa, kila mmoja anatamani kuuangalia na sisi kama wachezaji tunapenda michezo mikubwa na tumejiandaa, huu tumemaliza, tunakwenda kujiandaa na mchezo unaofuata.”

“Sisi kila mchezo tunajiandaa kwani tunatetea ubingwa wetu na mashabiki zetu, waje uwanjani siku zote kwani sisi tunawategemea wao na wao wanatutegemea sisi,” amesema Kapombe

Kwa upande wake, mchezaji wa Kagera Sugar, Abdul Kassim amesema, “tunamshukuru Mungu kwa kumaliza mchezo huu salama na haikuwa bahati yetu, tumefungwa.”

Wakati huo huo, kwenye michezo mingine iliyochezwa leo Jumatano, Mwadui FC baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo, imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting huku Namungo FC wakifungana 2-2 na JKT Tanzania.

error: Content is protected !!