May 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shule 753 Tanzania zapewa vifaa vya wenye mahitaji maalum  

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imetumia Sh. 2.3 bilioni katika mwaka wa fedha 2019/20 kununua vifaa vya kielemu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule za msingi 708 na sekondari 45. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Jumanne tarehe 7 Julai 2020 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Ave Maria Semakafu  wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa hivyo jijini Dar es Salaam.

Amesema, vifaa hivyo vinalenga kuimarisha ujifunzaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum waliopo katika shule za msingi na sekondari nchini humo.

Dk. Semakafu amesema pamoja na kugawa vifaa hivyo, wizara iliendesha mafunzo kwa walimu wa  lugha ya alama wanaofundisha  shule za sekondari ili waweze kutekeleza jukumu la ufundishaji.

Pia, amesema, mbali na mafunzo hayo, walitengeneza Kamusi ya lugha za alama ya kufundishia shule za msingi na sekondari.

“Tunashukuru maono ya Serikali ya awamu ya tano kwa kuwa baada ya kuingia madarakani (tarehe 5 Novemba 2015) imefungua fursa za  elimu kwa kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinasababisha watoto kufaidika na fursa hizo,” amesema.

“Katika kuhakikisha tunatekeleza hilo, wizara ya elimu iliandaa mkakati wa kujibu ombwe hilo ambao ni kuwapatia vifaa wezeshi na vya kielimu watoto wenye mahitaji maalum,” amesema Dk. Semakafu

Dk. Semakafu amemtaka Mkurugenzi wa Elimu maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Magreth Matonya kuwa na eneo la kipaumbele la kushughulikia  kila mwaka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Amesema, kwa mwaka wa fedha unaoanza 2020/21 kipaumbele kielekezwe kwa wanafunzi wenye usonji ili kuwezesha upatikanaji wa elimu bila changamoto.

Kwa upande wake, Dkt. Magreth ametaja baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa  ni mashine kubwa ya kuchapa maandishi ya wasioona, mashine 27 za kurudufisha maandishi ya nukta nundu, mashine 60 za kupima kiwango cha usikivu na vifaa 60 vya kufundishia matamshi kwa wanafunzi wenye changamoto ya matamshi.

Vingine ni miwani 5,167 za kuzuia mionzi ya jua, vioo 2,067 vya kukuzia maandishi kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu, vifani 5,720,  abakasi 9,909, pazo 2,260 za kufundishia stadi za kujimudu na hisabati kwa watoto wenye ulemavu wa akili na wenye usonji pamoja na vitimwendo kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo.

Naye, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Maulid Maulid amemuhakikishia Dk. Semakafu  kuwa vifaa hivyo vitafika shuleni kwa wakati na vitatumika ipasavyo badala ya kufungiwa stoo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Selemani Joseph kutoka shule ya Sekondari Pugu ya jijini Dar es Salaam ameishukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa hivyo na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia kusoma bila changamoto yoyote.

error: Content is protected !!