SHEIKH wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amewataka Watanzania kuishi maisha ya kulinda na kutunza amani. Anaripoti Danson Kaijage … (endelea).
Ameyasema hayo wakati akitoa ujumbe wa Sikukuu ya Eid katika msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma, kuwa amani iliyokuwa imetawala kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani inatakiwa kuendelezwa kila siku.
Aidha amesema, Watanzania wanatakiwa kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa kuacha kufanya mambo mabaya ikiwemo wizi, mauaji, kupora na kufanya yale mazuri yanayoleta maendeleo katika ngazi ya familia hadi ngazi ya Taifa.
“Wakati tunafanya mashindano ya Quran pale uwanja wa Jamhuri tulimuomba kamanda wa polisi (Gilles Muruto) ulinzi tukihofia kutokea matukio ya kihalifu, lakini chakufurahisha lile gari la polisi lilikuwa sehemu moja mpaka tukamaliza mashindano hayo, hiyo ni ishara ya kuwa kila mtu anajua umuhimu wa kufanya yale yanayompendeza Mwenyezi Mungu,” amema Sheikh Rajabu.
Pia aliongeza kuwa Waislamu wanatakiwa kuishi maisha ya kusaidiana kama ilivyokuwa kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, huku akisema wapo ambao baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuisha watarudia kufanya yale waliyokuwa wakiyafanya kipindi cha nyuma.
Awali akizungumza, sheikh alisema maisha ambayo watanzania watanakiwa kuishi maisha ya kutobaguana kwa sababu ya dini au kabila, akisema katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani hata wale ambao sio Waislamu walishiriki kwenye matukio mbalimbali mfano kufuturisha, ikiwa ni ishara ya kuonyesha Watanzania ni kitu kimoja.
Akizungumza mmoja ya waamini wa dini ya kiislamu, ambae pia ni mkazi wa Dodoma alisema watayaenzi yale waliyokuwa wanayafanya katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuwasaidia watoto yatima pamoja na watu wengine wenye uhitaji maalumu.
Leave a comment