June 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sheikh Ponda ‘watu wasiojulikana’ wanaichafua nchi

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa Ponda

Spread the love

SHEIKH Issa Ponda, Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, amesema kuwa vitendo vya utekaji vinavyodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana vinaichafua taswira ya nchi. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akizungumza kwenye baraza la Eid Al-Hajji jana tarehe 12 amesema kuwa vitendo hivyo vinaviweka vyombo vya dola lawamani kutokana na watu kukosa uhakika wa usalama wao ilhali vyombo hivyo vipo.

“Watu wanauawa, wanatekwa, tunasikia watu wanatekwa na tunaambiwa hawa watu wanatajwa kuwa ni watu wasiojulikana, wanateka na kuua watu na wanapewa jina kabisa ni watu wasiojulikana,” amesema.

“… nani anawajibika kulinda uhai wa raia. Hakuna mamlaka ya kulinda uhai wa raia? Kama mamlaka haiwezi kulinda uhai wa raia, ina sababu gani ya kujiita mamlaka kama katika taifa kuna watu wanawapoteza watu wengine?” anahoji Sheikh Ponda.

Amesema kuwa  zipo taarifa za watu kupotea katika jamii bila kupatikana ikiwa wafanyaji vitendo hivyo kuwa hawajulikani.

Amesema kuwa wakati wa sikukuu ni muafaka wa kuzingatia mambo ambayo yanayolitokea taifa, kwani wakati wengine wanasherekea, wengine wamepotea, wameuawa na ndugu zao wahajui lini watawapata au kuwaona.

https://www.youtube.com/watch?v=ytcw7Ue7hIU

Wakati huo huo, Sheikh Ponda amesema kuwa kigezo cha uvunjifu wa amani kisitumike kuwazuia watu wasikutane kwenye viwanja vya wazi kwa kuwa kinawanyima watu uhuru wa kubadilishana mawazo.

Amesema kuwa watu wameswali swala ya Eid katika viwanja vya wazi na wengine misikitini kwa idadi kubwa na kwamba watu wameondoka kwenye viwanja hivyo kwa amani bila ya kuwepo kwa ulinzi wowote.

“Hii tafakari yake ni kwamba dhana inayotumika sasa nchini ya kuwanyima watu haki ya kukutana katika viwanja vya wazi kwa madai ya kwamba mikutano inayofanyika katika viwanja hivyo inavuruga amani na utulivu, dhana hii siyo ya kweli na kwamba kipimo ni mkutano wa swala ya Eid katika viwanja vya wazi.

“… lakini leo hii hapa Tanzania wananchi wanazuiliwa kukutana hoja inayotumika ni kwamba mikutano ya wazi inavuruga amani na utulivu huko ni kuwanyima watu haki za msingi kwa maana hiyo nakusudia kuliinua hili tukio ili liwe mafundisho watu wasinyimwe haki ya kuzungumza kwa dhana  ya kuvuruga amani,” amesema Sheikh Ponda.

Amesema kuwa watu wana haki ya kuzungumza kwa pamoja masuala yao ya kijamii na kwamba wasinyimwe uhuru huo.

Pia Sheikh Ponda amesema kuwa wakati waislamu wanasherehekea sikukuu hiyo wakumbuke kuwa kuna viongozi  wa dini hiyo wanasota mahabusu kwa miaka sita bila upelelezi wa shauri lao kukamilika na kwamba watu hao wanashikiliwa kinyume cha sheria.

Amesema kuwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar aliwahi kusema kuwa masheikh hao wameshikiliwa kinyume cha sheria na utaratibu.

“Wakati sisi tunasherehekea Eid na familia zetu kuna watu wenye haki kama sisi hawako kwenye furaha, ukienda katika magereza mbalimbali utakuta watu wa namna hiyo hawako huru na kwa hakika hawajafanya kosa lolote  kwa sababu wale waliowaweka ndani hawajaweza kuthibitisha makosa yao muda mrefu,” amesema Sheikh Ponda.

error: Content is protected !!