May 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sheikh Ponda ataja sababu kumuunga Lissu

Spread the love

SHEIKH Issa Ponda, Katibu Shura ya Maimamu Tanzania amesema, anamuunga mkono Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kwa kwa sababu, ana uwezo wa kusimamia ajenda na masilahi ya wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Sheikh Ponda ametoa kauli hiyo jana Jumatatu tarehe 19 Oktoba 2020 katika mkutano wa kampeni wa Lissu uliofanyika Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro.

“Sisi viongozi, tulikaa tukafanya tathimini na kuona, hakuna mtu mwingine anayefaa isipokuwa  Lissu, tunahitaji ushirikiano na mtu mwenye uwezo wa kusimamia ajenda za wananchi, alitaka kupoteza maisha lakini kwa sababu ya baraka alizokuwa nazo leo yuko pale. Alitaka kupoteza maisha kwa ajili ya masilahi ya Watanzania,” amesema Sheikh Ponda. 

Aidha, Ponda amesema, tatizo la Tanzania kutofikia maendeleo linatokana na mfumo mbovu wa uongozi uliotokana na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwashauri wananchi kutumia Uchaguzi Mkuu wa Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 kurekebisha dosari hiyo kwa kuchagua wagombea wa vyama vya upinzani.

“Tatizo letu sisi sio rasimirimali, tatizo letu ni mfumo wa nchi, shida kubwa tuna tatizo la uongozi. Mfano hai CCM tumewapa ridhaa tangu 1964 hawajafanya kitu.  Sasa wanaomba tena  wanaweza kuongoza nchi?”alihoji Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda aliwashauri Watanzania kufanya tathimini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, kabla ya kwenda kupiga kura ili wapate majibu kama serikali hiyo inafaa tena kupewa ridhaa ya kuongoza nchi.

“Tunapoingia katika uchaguzi baada ya  miaka mitani, mnapewa fursa ya kufanya tathimini ya uongozi uliopita, hali ya utawala ilikuaje? Mnaangalia biashara na usalama wa nchi ulikuwaje, mkiona wale wenye madaraka wamefanya vizuri wanachaguliwa tena. Mkiona wamefanya vibaya hamuwachagui,” alisema Sheikh Ponda.

Rais Magufuli anayemalizia awamu yake ya kwanza ya uongozi aliyoianza tarehe 5 Novemba 2015 amepitishwa tena na CCM kutetea kiti cha Urais wa Tanzania ambapo anachuana na wagombea wenzake 14 akiwemo Lissu.

error: Content is protected !!