Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Shahidi mlenga shabaha (Sniper): Sijui kilichomuua Akwelina
Habari za SiasaTangulizi

Shahidi mlenga shabaha (Sniper): Sijui kilichomuua Akwelina

Viongozi wa Chadema wakiwa mahakamani
Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeendelea na usikilizaji wa kesi namba 112 ya mwaka 2018 inayowakabali viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo Shahidi wa nne amemaliza kutoa ushahidi wake. Anaripoti Faki Sosi … (endelea). 

Shahidi huyo wa nne ambaye kwa taaluma ya kijeshi ni mlenga shabaha (Sniper) ni PC Fikiri askari wa Jeshi la Polisi aliyefika katika mahakama hiyo kutoa ushahidi wake. 

Ushahidi huo umetolewa leo tarehe 4 Juni, 2019, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa Utetezi uliongozwa na Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala, John Mallya na Hekima Mwasipu, huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi, Paul Kadushi na Salimu Msemo.

Upande wa utetezi umeendelea kumhoji Shahidi huyo wa Jamhuri walipoishia tarehe 31 Mei mwaka huu kama ifuatavyo:-

Kibatala: Pengine kuna taarifa ya daktari taarifa za kuumia kwako, sasa ulimuonesha Hakimu sehemu ambayo umeumia kwa nje jeraha kovu?

Shahidi: Sikuonesha.

Kibatala: Ulizungumzia pia wewe kupoteza saa sehemu eneo la tukio, tusaidie uliwahi kuizungumzia angalau umepoteza saa ya aina gani?

Shahidi: Sijaonesha.

Kibatala: Ulitoa risiti ya hiyo saa?

Shahidi: Sijaitoa.

Kibatala: Unasema wewe ulipigwa na jiwe, baada ya kupigwa na jiwe ulizimia au ulikuwa na fahamu zako?

Shahidi: Sikuzimia.

Kibatala: Kwa kuwa haukuzimia, unajua mahala ambapo hilo jiwe, lilidondoka na ulitoa au hukutoa mahakamani hilo jiwe?

Shahidi: Sijatoa.

Kibatala: Ulisema zilitumika fimbo na chupa, ulitoa mahakamani?

Shahidi: Sijatoa chochote.

Kibatala: Shahidi unasema wewe na mwenzako, Koplo Rahim mlisafirishwa kwenda hospitali ya Kilwa Road, ulikumbuka kusema gari iliyowapeleka hospitali?

Shahidi: Nilichoeleza mimi nilipelekwa hospitali na gari ya polisi.

Kibatala: Bila shaka ni gari ya Polisi, haiwezi kuwa daladala ulieleza gari gani?

Shahidi: Mheshimiwa Hakimu mimi nilikuwa mhanga wa kwenye hilo tukio sikuweza kujua gari ya aina gani.

Kibatala: Mueleze hakimu kwamba hilo gari ulitambulishwa.

Shahidi: Nafikiri nimeshajibu hilo swali sijui kwanini anang’ang’ania majibu anayotaka yeye.

Hakimu Simba: Ulilizungumia kwenye ushahidi wako?

Shahidi: Mheshimiwa hakimu magari ya Polisi yanafahamika.

Kibatala: Mwambie mheshimiwa hakimu baada ya kuzimia Koplo Rahim, wewe ukishuhudia amezimia akatolewa akawekwa kwenye gari, wewe ulitumia muda gani kusubiriwa uumie?

Shahidi: Kama dakika tatu.

Kibatala: Ushahidi wako ni kwamba Koplo Rahim ameumia akachwa kwa dakika tatu.

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Wewe binafsi ulitoa maelekezo kwamba umeumia upelekwe hospitali ya Kilwa Road?

Shahidi: Sikutoa maelekezo.

Kibatala: Unaufahamu umbali wa kutoka eneo la tukio hadi Kilwa Road hospitali?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Mlitumia muda gani?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kwa ushahidi wako Koplo Rahim hapa, mkiwa mnaelekea Kilwa Road alikuwa amezimia?

Shahidi: Alikuwa amezimia.

Kibatala: Unakumbuka cheo cha Ofisa wa Polisi ambaye amekuwa mkuu wa msafara wakuwapeleka Kilwa Road.

Shahidi: Simfahamu.

Kibatala: Kwa kumbukumbu zako ulikuwa wewe Koplo Rahim na dereva au kulikuwa na mtu mwingine wa zaida?

Shahidi: Kulikuwa na mtu mwingine.

Kibatala: Mtu huyo mwingine ulimzungumzia kwa namna yoyote katia ushahidi wako?

Shahidi: Sikumzungumzia.

Kibatala: Alikaa na dereva au alikaa na nyie?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Unakumbuka majukumu yake yalikuwa nini?

Shahidi: Majukumu yake yalikuwa ni kutusaidia wagonjwa.

Kibatala: Kwa hiyo alikuwa akiwasaidia lakini wewe humkumbuki?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Wakati unatoa ushahidi wako ulizungumza chochote kuhusu Koplo Rahim kupewa huduma ya kwanza wakati amezimia?

Shahidi: Sikuzungumza.

Kibatala: Si sahihi kwamba kutoka eneo la tukio kuna hospitali kubwa tu inaitwa Mwananyamala unaifahamu au huifahamu?

Shahidi: Siifahamu.

Kibatala: Kwa ufahamu wako askari wanatibiwa Mwananyamala kwa dharura?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Ukitoka pale Mkwajuni karibu kuna hospitali kubwa ya Muhimbili?

Shahidi: Nafahamu.

Kibatala: Ni sahihi kwamba pale Muhimbili wanatibiwa maofisa wakubwa wa serikali ikiwemo maofisa wa Polisi?

Shahidi: Nafahamu.

Kibatala: Tukumbushe cheo chako?

Shahidi: Koplo

Kibatala: Unakumbuka chochote kwenye safato yenu ya Kilwa Road hospitali?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Ulisema chochote kuhusu gari ile kupiga honi au kupiga ving’ora?

Shahidi: Sikusema chochote.

Kibatala: Umesema chochote namna ulivyopokelewa pale hospitali?

Shahidi: Sikusema.

Kibatala: Nasema hivi siyo kwamba nakuonea wewe na mwenzako mmetajwa kwenye shtaka la nne.

Shahidi: Nilisema sikusema chochote.

Kibatala: Shahidi unakumbuka kutaja majina ya muuguzi au daktari aliyewahudumia?

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala: Ulitaja jina la wodi ambayo umelezwa?

Shahidi: Kimya.

Kibatala: Sisi tumeshafanya kazi tumepita kote huko kuna wodi fulani umetaja au hujataja?

Hakimu Simba: Jibu

Shahidi: Sijataja.

Kibatala: Umetaja jina la daktari alikuruhusu?

Shahidi: Sijataja.

Kibatala: Wewe na Koplo Rahim mlilazwa wodi moja au tofauti?

Shahidi: Wodi moja.

Kibatala: Unafahamu muda ambao Koplo Rahim alipopata fahamu?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Wewe na Koplo Rahim mliongea muda gani na tarehe ngapi alipopata fahamu?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Ni sahihi kwamba yeye na Koplo Rahim mnafahamiana kabla ya tukio la Mkwajuni na kabla hamjapelekwa hospitali?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Ni sahihi wewe na Koplo Rahim mlikuwa mnafanya kazi kwa pamoja?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Ni sahihi wewe tukio la Koplo Rahimu lilikustusha?

Shahidi: Sahihi

Kibatala: Lakini unasisitiza kwamba pamoja na kustuka na tukio hilo hukuwahi kuongea na Koplo Rahim?

Kibatala: Mpaka leo hii umewahi kuzungumza na Koplo Rahim?

Shahidi: Koplo Rahim ni mfanyakazi mwenzangu nimewahi kuzungumza naye lakini sio tukio hilo.

Kibatala: Ndio nilipokuwa napataka hapo hapo, tukio la kukustua hujazungumza naye hadi leo?

Shahidi: Sikuwahi kuzungumza naye.

Kibatala: Ni sahihi kwamba kwa kuwa PF3 hii ilikufuata hospitali baada yeye kumwambia Mwandishi wa PF3 hii muda wa tukio hili?

Shahidi: Sikuwahi kumwambia.

Kibatala: Muda gani kwa mara ya kwanza ulifikishwa pale Kilwa Road hospitali?

Shahidi: Nilivyofikiswa hospitali.

Kibatala: Ni muda gani?

Shahidi: Ilikuwa jioni.

Kibatala: Shahidi nivumilie hapa kuna muda umejazwa.

Hakimu Simba: Nimesharekodi jioni.

Kibatala: Lakini haikuwa saa tano?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Jiwe lilikupiga wewe lilikuwa lina ncha kali?

Shahidi: Sikumbuki ila mimi najua ni jiwe.

Kibatala: Shahidi ulifanyiwa upasuaji na kushonwa?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Haya huyu aliyejaza huku itakuwa katuongopewa? Kibatala: Ulitoka damu au hukutoka damu?

Shahidi: Damu nilitoka.

Kibatala: Uliwahi kuzungumzia hatua za awali za kitabibu za kuzuia damu isitoke?

Shahidi: Sikupata huduma yoyote.

Kibatala: Hukupata huduma yoyote au hukuzungumzia?

Hakimu Simba: Nimeandika hakupata.

Kibatala: Ni sahihi kwamba ulivuja damu kutoka Mkwajuni hadi hospitali?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Huku inaonesha kidonda chako kilikaa saa tatu bila hudumu, ieleze mahakama mwenyewe juu ya hili.

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Ulizungumza chochote juu ya kuwekewa damu?

Shahidi: Sikuzungumza.

Kibatala: Ulivyofika hospitali kuna ndugu yako yoyote aliyefika?

Shahidi: Ndugu yangu alifika baadaye sana.

Kibatala: Kama muda gani?

Shahidi: Kesho yake.

Kibatala: Unalifahamu kundi lako la damu?

Shahidi: O

Kibatala: O ni O positive au O negative?

Shahidi: O Plus.

Kibatala: Uliongozewa damu ulipofika hospitali au hukuongozewa?

Shahidi: Sikuongozewa.

Kibatala: Shahidi lini ulitoka hospitali?

Shahidi: Tarehe 18 mwezi wa pili, mwaka 2018.

Kibatala: Nakuonesha kwa ajili ya utambuzi daktari aliyekuhudumia wewe kama kweli hiyo, karatasi haikuchora anasema uliruhusiwa tarehe 20 mwezi wa pili, unasemaje?

Shahidi: Mimi nakumbuka hivyo.

Kibatala: Kwa kumbukumbu yako ulipewa mapumziko ya muda gani?

Shahidi: Wiki mbili.

Kibatala: Sasa shahidi hebu tusaidie pale Kilwa Road ulipewa kadi ya mahudhurio?

Shahidi: Ndio nilipewa.

Kibatala: Ni sahihi ulipewa kadi ya mahudhurio, ulikaa nayo na ulikuwa chini yako?

Shahidi: Nilikabidhiwa.

Kibatala: Kadi hiyo umeitoa mahakamani kama kielelezo kuthibitisha kama kweli ulirudi kwa matibabu?

Shahidi: Sijaitoa.

Kibatala: Ulitoa maelezo yoyote kuhusu kilichofanya?

Shahidi: Sijatoa.

Kibatala: Ni ofisa gani wa Polisi aliyetoa maelekezo ya kufyatuliwa kwa risasi pale Mkwajuni?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Koplo Rahim alirusha risasi ngapi kabla hajazimia?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu kuwa kuna tuhuma wewe na Koplo Rahim ndio mliofyatua risasi mkamuua Akwelina?

Shahidi: Sijawahi kusikia.

Kibatala: Kati ya moja wapo ya mashtaka kuwa Akwelina Akwilini alikuwa katika maandamano, uliwahi kutoa ushahidi kuwa kati ya waandamanaji walikuwa na silaha za moto?

Shahidi: Sikuwahi kutoa.

Kibatala: Ni kweli Akwelina Akwelini alikuwa katikati ya barabara?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Ni sahihi kuwa Marehemu Akwelina Akwelini alifariki kwa majeraha ya risasi?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Shahidi umetaja majina ya dereva aliyewapeleka wewe Koplo Rahim hospitali?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Shahidi kwa mujibu wa sheria ukiumia kuna maelezo kama muhanga unaandika nachotaka kufahamu kama uliandika maelezo ya muhanga?

Shahidi: Niliandika.

Kibatala: Uliondoka mnamo tarehe ngapi, mwezi wa ngani?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Ni ofisa gani wa polisi aliyeandika maelezo ya wewe kuwa ni muhanga uliyeumizwa na jiwe?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Maelezo hayo kwa kuwa wewe ndiye uliyetamka uliyatoa mahakamani?

Shahidi: Sikuyatoa.

Kibatala: Ulikumbuka kuzungumzia chochote juu ya wewe kutoa hayo maelezo?

Shahidi: Sikuzungumzia.

Kibatala: Unafahamu Koplo Rahim aliruhusiwa lini kama kweli ulilazwa naye?

Shahidi: Sifahamu alilazwa lini?

Kibatala: Nani alianza kuruhusiwa yeye au wewe?

Shahidi: Siwezi kuongelea.

Hakimu Simba: Muulize swali.

Kibatala: Ni nani kati ya wewe na Koplo Rahim alianza kuruhusiwa?

Shahidi: Sijui.

Kibatala: Ukiwa hospitali kitanda chako na Koplo Rahim vilikuwa karibu au mbali?

Shahidi: Vilikuwa mbali.

Kibatala: Ulikuwa baada ya vitanda mia kumi?

Shahidi: Siwezi kukadiria.

Kibatala: Mlikuwa wewe na Koplo Rahim au mlikuwa wengi?

Shahidi: Tulikuwa wengi.

Kibatala: Unamkubuka uliyekuwa naye jirani?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Ukiacha tukio la wewe kuwa muhanga uliwahi kuchukuliwa maelezo juu ya maandamano?

Shahidi: Niliwahi.

Kibatala: Nani ofisa wa polisi aliyerekodi mazungumzo yako?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Ni sahihi kwenye maelezo yako, ndio tulikuta taarifa za wewe kuwatambua watuhumiwa?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Umeyatoa maelezo hayo kama kielelezo?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili Kibatala alimaliza kumhoji shahidi na kumpisha wakili Mallya.

Mallya: Shahidi ni sahihi matumizi ya saa ambayo ulikuwa nayo siku hiyo madhumuni yake ni kutazama muda?

Shahidi: Sahihi.

Mallya: Ulitazama wakati huo ilikuwa inafanya kazi?

Shahidi: Ilikuwa inafanya kazi.

Mallya: Tuambie ilikuwa saa ngapi wakati ulipoitazama?

Shahidi: Muda huo sikuitazama inasoma saa ngapi.

Mallya: Kwa hiyo hukuitazama?

Shahidi: Sikuitamaza saa ngapi labda imepotea.

Mallya: Ilikuwa saa ngapi mahakama irekedi?

Shahidi: Nimesema sikujua muda.

Mallya: Kujua inafanya kazi ulitazama nini maana yake mimi natazama mishale au ulitazama mikanda?

Shahidi: Ukiwa saa yako lazima uijue ila mimi niliangalia inafananya kazi.

Mallya: Ukitaka kujua inafanya kazi unafanya nini?

Shahidi: Unaangalia mishale inatembea.

Mallya: Yako ilikuwa ya mshale au ya namba?

Shahidi: Ilikuwa ya mshale.

Mallya: Kwa hiyo saa yako ya mshale umeengalia inafanya kazi lakini hukujua saa ngapi?

Hakimu Simba: Nisharekodi

Mallya: Wakati unapigiwa simu ulikuwa Mwananyamala?

Shahidi: Sikupigiwa simu ilipigiwa radio call kwa kiongozi wetu.

Mallya: Wakati huo Ngichi alikuwa wapi?

Shahidi: Mkwajuni.

Mallya: Shahidi mzoefu wa kuvaa saa kwa makadirio kutoka kwa Kopa Mwananyamala hadi pale Mkwajuni mlitumia muda gani?

Shahidi: Sikumbuki.

Mallya: Sasa tayari Ngichi amewapigia Radio Call mkiwa Mwananyamala lakini mlimkuta Ngichi anatangaza Ilani?

Shahidi: Ndio.

Mallya: Nataka kujua wakati anakupigia Radio Call Ngichi alitumia muda gani?

Shahidi: Sijawahi kurekodi muda siwezi kufahamu.

Mallya: Huwezi kufanya kadirio, hiyo doria mliyoifanya siku hiyo ilikuwa ya uchaguzi au ya kawaida tu?

Shahidi: Ilikuwa ya kawaida tu.

Mallya: Siku hiyo ulikuwa umebeba bunduki ya aina gani?

Shahidi: Nilibeba SMG.

Mallya: Wakati mnafanya hiyo doria mlipita njia gani?

Shahidi: Wakati tunafanya doria huwezi kujichagulia njia, njia yoyote inapita.

Mallya: Uliwahi kupita uwanja wa Buibui?

Shahidi: Hapana.

Mallya: Kabla ya tukio mlipata kupita barabata ya Kawawa?

Shahidi: Sikumbuki.

Mallya: Wenzako walisema walipotoka kwenye kampeni walipita njia ya lami kwenye hizi njia za lami za Mwananyamala kuna mawe?

Shahidi: Njia hakuna mawe.

Mallya: Kwenye njia ya mwendokasi hata kama hukupita lakini unaifahamu kuna mawe?

Shahidi: Hakuna mawe.

Mallya: Sasa hawa waandamanaji uliosema wakirusha mawe wametoka nayo wapi, wameokota barabara au wemetoka nayo nyumbani?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Huwezi kufahamu wewe unakumbuka hizo fimbo ulizosema wamebeba wamezitoa wapi?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Bahati nzuri shahidi wewe ulikuwa kwenye doria siku hiyo na bahati nzuri mkutano ulitangaza ulipata kusikia Mbowe akitangaza njooni na mawe leo kwenye mkutano?

Shahidi: Sikuwahi kusikia.

Mallya: Fimbo na chupa?

Shahidi: Sikuwahi kusikia.

Mallya: Shahidi umesema jiwe lilikupiga kwenye mkono wako na saa imepotea?

Shahidi: Ni sahihi.

Mallya: Unasemaje saa imepotea ilivunjika au kupotea?

Shahidi: Ilivunjika na kupotea.

Mallya: Ni sahihi ulisema kwamba alilalamika kwa maumivu kabla ya kuzimia?

Shahidi: Rudia.

Mallya: Ni sahihi ulisema kwamba alilalamika kwa maumivu kabla ya kuzimia?

Shahidi: Alilalamika kwa vitendo.

Mallya: Alilalamikaje?

Shahidi: Alikuwa akigusa sehemu alizoumia.

Mallya: Na wewe ulishuhudia?

Shahidi: Ndio.

Mallya: Ilichukua muda gani?

Shahidi: Siwezi kukadiria.

Mallya: Alikuambia kwamba amezimia?

Shahidi: Hajaniambia.

Mallya: Wewe umeishia form four umejuaje huyu mtu amezimia na huna taaluma ya kidaktari, ulijuaje alikuwa akuogopa maandamano akijifanya amelala?

Mallya: Ulijuaje?

Shahidi: Nilimuona amelala.

Mallya: Usiku wa jana ulilala?

Shahidi: Ndio.

Mallya: Ulikuwa unaongea?

Shahidi: Sikuongea.

Mallya: Shahidi ni sahihi kwamba kwa kuwa wewe sio tatibu huwezi kujua tofauti ya mtu aliyelala na aliyezimia?

Shahidi: Najua.

Mallya: Unajuaje?

Shahidi: Ukiwa umelala unakuwa chumbani kwako

Mallya: Siwezi kulala kwenye tukio?

Shahidi: Huwezi labda uwe na matatizo ya akili.

Mallya: Unaijua akili ya Koplo Rahim?

Shahidi: Siwezi kuijua akili ya Koplo Rahim.

Mallya: Bwana Ngichi alitangaza ilani na watu waligomea ilichukua muda gani hilo tukio?

Shahidi: Siwezi kukadiria ilichukua muda gani.

Mallya: Shahidi wewe ulikuwa wapi mbele ya askari wanaopiga mabomu?

Shahidi: Rudia.

Mallya: Ulisimama sambamba na askari waliombiwa na Ngichi wapige mabomu?

Shahidi: Nilikuwa nyuma yao.

Mallya: Kwa hiyo kwa shahidi wako waandamanaji walirusha jiwe wakakupata wewe uliokuwa nyuma?

Mallya: Unaweza kufananisha jiwe lilikupiga wewe na Koplo Rahim?

Shahidi: Siwezi kufananisha.

Mallya: Kwanini huwezi kufananisha?

Shahidi: Kwa sababu mimi siwezi kupima ukubwa wa mawe.

Mallya: Lakini uliyaona?

Shahidi: Niliyaona.

Mallya: Unasema uliyaona mawe, unaweza kutuambia muonekano wa yale mawe?

Shahidi: Siwezi kujua.

Mallya: Mawe yapo mengi utuambie aina ya jiwe labda kokoto?

Shahidi: Siwezi kukumbuka.

Mallya: Lilikuwa na shape gani?

Shahidi: Lilikuwa kubwa.

Mallya: Lilikuwa limechongoka?

Shahidi: Hapana.

Mallya: Shahidi unakumbuka jina la mwandamaji aliyejaribu kukunyang’anya bunduki yako?

Shahidi: Siwezi kukumbuka.

Mallya: Lakini yupo hapa?

Shahidi: Hayupo.

Mallya: Shahidi turudishe pale hospitali Kilwa Road, wewe mgonjwa uliyepata jeraha na yule mwengine aliyepoteza fahamu mliwekwa wodi moja?

Shahidi: Tulikuwa wodi moja.

Mallya: Ni sahihi kwamba hukutaka kumjulia hali, hukutaka kuzungumza naye kabisa kwa sababu uligundua yeye ndiye aliyekuibia saa yako?

Shahidi: Sio sahihi.

Mallya: Simu mlipopokea mliichukulia ni dharura au ni taarifa ya kawaida tu?

Shahidi: Ilikuwa dharura.

Mallya: Mheshimiwa naomba tambuzi namba mbili (D2) shahidi wakati unaulizwa na wakili Kibatala ulisema uliacha damu zikitoka sababu ni kwamba kulikuwa hakuna boksi la huduma ya kwanza?

Shahidi: Hakuna.

Mallya: Umepiga X-ray ya kichwa tarehe ngapi?

Shahidi: Sikumbuki.

Mallya: Hukumbuki tarehe au hujapigwa X-ray ya kichwa?

Shahidi: Nilipigwa?

Mallya: Shahidi tusaidie wewe kama mlenga shabaha, unaweza kutueleza bunduki ya Ak41 ikipigwa inakwenda umbali gani?

Shahidi: Siwezi kuelezea.

Mallya: Huwezi kueleza, hutaki au hujui?

Shahidi: Sijui.

Mallya: Na bunduki ya SMG inaruka umbali gani?

Shahidi: Sijui.

Wakili: Ulipopigwa jiwe la kichwa kitu gani kilitokea?

Shahidi: Kizunguzungu.

Wakili: Baada ya hapo?

Shahidi: Nilipelekwa hospitali.

Mallya: Uliandika maelezo kuzungumzia kuwa ulipotelewa mali siku hiyo?

Shahidi: Nilieleza.

Mallya: Kwenye shtaka na nne kilichofanya wewe PC Fikiri na Koplo Rahim. Ni maandamano sio mawe ni sahihi?

Shahidi: Sahihi.

Hakimu Simba: Amesemaje?

Mallya: Nimemuuliza kwa mujibu wa shtaka la nne ambalo washtakiwa wanashitakiwa nalo ni sahihi kuwa wewe na Koplo Rahim mliumia kutokana na maandamano?

Shahidi: Mawe.

Mallya: Mpaka unapigwa jiwe wewe umekaa tu au ulifanya nini?

Shahidi: Nilikuwa natuliza maandamano.

Mallya: Ulikuwa unatulizaje maandamano unabunduki mkononi, ulienda kutuliza maandamano au kutawanya?

Shahidi: Nilifuata amri ya kiongozi.

Wakili: Amri ya Ngichi ni kupiga risasi hewani, ulirusha risasi hewani?

Shahidi: Sio sahihi.

Mallya: Kazi yako ni kutawanyisha maandamano na unabunduki kiongozi wako utawanye maandamano.

Shahidi: Siwezi kuzungumzia nilipigwa jiwe.

Mallya: Kwa hiyo ulifika ukapiga jiwe hakuna chochote ulichofanya na uliyotuhadithia yote uliyapata wapi?

Hakimu nimemaliza.

Baada ya kumaliza Mallya alimuachia kijiti Wakili Mwasipu.

Mwasipu: Umeiambia mahakama ulikuwa mita 20 kutoka kwa waandamanaji?

Shahidi: Sahihi.

Mwasipu: Ni sahihi kwamba waandamanaji waliokuwa ni hawa waliokuwa mbele yako?

Shahidi: Sahihi.

Mwasipu: Ni sahihi uliwatambua watuhumiwa wanne Mdee, Mbowe, Msigwa na Mwalimu?

Shahidi: Niliwatambua hao kwa majina wengine niliwaona.

Wakili: Hao washtakiwa uliowaona walikuwa wanatembea kwa miguu au kwenye gari?

Shahidi: Walikuwa wanatembea kwa miguu.

Mwasipu: Wote?

Shahidi: Ndio niliowaona.

Mwasipu: Je, ni sahihi au sio sahihi hadi sasa hivi hujui sababu ya maandamano?

Shahidi: Sahihi.

Mwasipu: Je, kuna raia yoyote aliyekuja kuripoti kwako parnal kwamba ameathirika na maandamano?

Shahidi: Hakuna.

Mwasipu: Kwa watuhumiwa waliokuwepo mahakamani hapa nani aliyetamka hatupoi?

Shahidi: Simfahamu.

Mwasipu: Hatutishwi?

Shahidi: Simfahamu.

Mwasipu: Hatuogopi bunduki?

Shahidi: Simfahamu.

Mwasipu: Mashabiki 10 wa Simba wakiongozana kwenda Uwanja wa Taifa wanafanya kosa au hawatafanya kosa?

Shahidi: Hahajafanya kosa.

Mwasipu: Wanachama 20 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiongozana kwenda kwa Mkurugenzi kwenda kuchukua kiapo chao wanakuwa wamefanya kosa au hawajafanya kosa?

Shahidi: Sio kosa.

Mwasipu: Hawajafanya kosa?

Mwasipu: Wanachama wa CCM wakiwa 20 wakiongozana kwenda kwa Mkurugenzi wakiwa wanaimba hatupoi hatutishwi wanakuwa wamefanya kosa?

Shahidi: Inategemea wapo katika hali gani?

Mwasipu: Wanafuraha? 

Shahidi: Sio kosa.

Mwasipu: Wakiwa na hasira watakuwa wemafanya kosa?

Shahidi: Itakuwa wamefanya kosa.

Mwasipu: Hawa washktakiwa walivaa mizura au hawakuvaa?

Shahidi: Sikumbuki.

Mwasipu: Ni sahihi hukumbuki alishika mawe au aliyeshika chupa?

Shahidi: Sikumbuki.

Mwasipu: Ni shahidi waliorusha mawe hawapo kwenye mahakama hii?

Mwasipu: Hayo mawe ulitoa kama kielelezo

Shahidi: Sikutoa.

Baada ya hapo Profesa Safari alimalizia

Prof. Safari: Ulisema ulikuwa na SMG

Shahidi: Ndio.

Prof. Safari: Ilikuwa na risasi ngapi?

Shahidi: 3o.

Prof. Safari: Uliwahi kutumia.

Shahidi: Sikuitumia.

Prof. Safari: Ulibeba tu hukuitumia.

Shahidi: Sikuitumia.

Prof. Safari: Askari wenzako waliitumia au hukuitumia.

Shahidi: Sikumbuki.

Prof. Safari: Unafahamu kwenye tukio hilo alikufa Akwelina?

Shahidi: Ndio.

Prof. Safari: Unajua kilichomuua?

Shahidi: Sijui.

Prof. Safari: Unatumia pombe?

Shahidi: Situmii.

Prof. Safari: Sigara unavuta?

Shahidi: Sivuti.

Prof. Safari: Sigara kali unavuta?

Shahidi: Sivuti.

Kicheko Mahamakamani

Kesi hiyo imehairishwa mpaka tarehe 1, 2, 3 na 4 mwezi Julai, 2019.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!