Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Shahidi abanwa, Dk. Mashinji augua ghafla kizimbani
Habari za SiasaTangulizi

Shahidi abanwa, Dk. Mashinji augua ghafla kizimbani

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imeahairisha kusikiliza ushahidi wa shahdi wa tatu wa upande wa mashitaka katika kesi inayowakabili viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufuatia kuugua ghafla kwa Katibu Mkuu wa chama hiko, Dk. Vincent Mashinji.  Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Dk. Mashinji, ni mshtakiwa wa sita kwenye kesi hiyo ya uchochezi namba 112 ya mwaka 2018, inayowakabili viongozi wandamizi wa Chadema, wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo, ni pamoja na Salum Mwalim, naibu katibu mkuu Zanzibar; John Myika, naibu katibu mkuu (Bara); Esther Matiko, mbunge wa Tarime Mjini na John Heche, mbunge wa Tarime Vijijini.

Wengine, ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya na Mbunge wa Kawe na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema taifa, Halima Mdee.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, mmoja wa mashahidi wa Jamhuri, Koplo Rahim Msangi, aliiambia mahakama kuwa aliwaona baadhi ya washitakiwa waliwashambuliwa maofisa wa polisi kwa mawe.

Aliwataja waliokuwa wamebeba mawe na kuwashambulia polisi, kuwa ni pamoja Mbowe, Mdee, Dk. Mashinji, Mnyika na Matiko.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Wankyo Simoni, shahidi huyo alidai kuwa yeye binafsi, alishambuliwa na moja ya mawe yaliyorushwa na baadhi ya washitakiwa.

Alisema, jiwe lililorushwa na washitakiwa hao ambao walikuwa katika maandamano, lilimpiga yeye kichwani na kumuumiza vibaya; jambo ambalo lilimlazimisha kupatiwa matibabu katika hospitali ya jeshi la Polisi, iliyopo eneo la Kilwa Road, wilayani Temeke.

Shahidi huyo alidai kuwa shambulizi hilo la jiwe lilimfanya kupoteza fahamu, kuongezwa maji mwilini, na alipozinduka alijikuta yuko kitandani kwenye hospitali hiyo ya jeshi la polisi. 

Alidai katika kadhia hiyo, yeye binafsi, alipoteza bunduki aliyokuwa amekabidhiwa aina ya Sub Machine Gun (SMG).

Alisema, “hawa watu (akiwaonyesha washitakiwa), walikuwa wakirusha mawe kama mvua, huku baadhi ya waandamanaji wakiwa wamefunika nyuso zao ili wasioneakane.”

Katika kesi hiyo, Jamhuri inawakilishwa mahakamani na Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi; Wakili Mkuu wa Serikali, Paul Kadushi na wakili wa serikali, Wankyo Simon; huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Prof. Abdallah Safari, Hekima Mwasipu, Peter Kibatala, John Mallya na Jeremiah Mtobyesa.

Hata hivyo, katika mahojiano yake na wakili wa utetezi – Peter Kibatara – shahidi huyo alikiri kutomtaja askari aliyerudisha silaha kituoni baada ya yeye kuumia na kukimbizwa hospitali na wala namba ya silaha aliyokabidhiwa.

Mahojiano kati ya Kibatala na Koplo Rahim, yalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Tuanze eneo la silaha ndio maana tukaita kitabu cha mwongozo cha Polisi (PGO) Silaha anatakiwa arudishe nani au inarudishwa kiholela?

Shahidi: Inategemea.

Kibatala: Vifungu vya (PGO) vinavyohusiana na silaha unavifahamu?

Shahidi: Navifahamu.

Kibatala: Isaidie mahamakama ni PGO ipi inaruhusu silaha iliyochukuliwa na Kibatala irudishwe na Mallya?

Shahidi: Inategemea.

Kibatala: Isaidie mahamakama ni PGO ipi inaruhusu silaha iliyochukuliwa na Kibatala irudishwe na Mallya ikiwa kibatala hajafa?

(Wakili Wankyo Simon anaingialia)Kibatala anarudia swali.

Shahidi: Inategemea.

Hakimu Simba: Shahidi unatakiwa ujibu unakijiua au hukijui.

Shahidi: Sikijui.

Kibatala: Mpaka leo unakuja kutoa ushahidi wako unafahamu kwamba SSP Ngichi ameshakuja kutoa ushahidi wake?

Shahidi: Nafahamu.

Kibatala: Ni sahihi ulifahamu utakuja kutoa ushahidi kuhusu silaha?

Shahidi: Sikuja kutoa ushahidi kuhusu SMG.

Kibatala: Kwa hiyo unasema hukuja kutoa ushahidi kuhusu SMG swali langu lipo palepale kwamba ulifahamuutaulizwa kuhusu silaha ni sahihi?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Lakini ni sahihi ulitoa ushahidi wako katika maeneo matatu kuhusu SMG la kwanza…kitandani ulipozinduka, alipokuja Afande Mzelenge Hospitali, tatu kuhusu ufahamu wako juu ya askari mwenzako aliyerejesha silaha Osterbay baada ya wewe  kuumia?

Shahidi: Kuhusu silaha ilirejesha Polisi.

Hakimu Simba: Kwanza jisikie huru anakuuliza kwamba hivi vipelengele ulivizungumza hapa mahamakama. Kadushi Muelekeze shahidi.

Kibatala anarudia swali.

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Ni sahihi unapopewa silaha unasaini kwenye kitabu maalum?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Ni unasainishwa ili Jeshi la Polisi ilijue ilipo ile silaha, risasi zilipotumika na inaporudi?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Ni sahihi mtu anayepewa silaha lazima ikagiliwe silaha yenyewe kisha risasi kama zilikuwa 30 na zimerudi 30?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Ni sahahi zoezo hili jeshi la Polisi na Umma kuhakisha silaha inatumika kwa mujibu wa sheria?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Ni sahihi kwamba yule anayetumia Silaha vibaya anatakiwa achukuriwe hatua.

Shahidi: Inategemea.

Kibatala: Labda nirejee swali kwamba Ofisa wa Polisi anayetumia silaha yake vibaya anachukuliwa hatua au hachukuliwa hatua yoyote?

Shahidi: Askari ana akili ndio maana anapewa.silaha.

Hakimu: Jibu swali

Shahidi: Ni sahihi.

Hakimu Simba ametoa onyo kwa watu waliohudhuria kwenye kesi hiyo kuwa  wawe wavumilivu kutokana na mijadala asiyoielekeza hakimu.

Kibatala: Ni sahihi kwamba namba ya bunduki hii ya SMG  haujaitaja?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Ni sahihi kila bunduki inayowepewa askari inakuwa na namba?

Shahidi: Sijakuelewa.

Kibatala: Ni sahihi mimi askari Kibatala nakwenda lindo sipewe silaha kama pipi?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Huyu askari aliyerudisha silaha kwa niaba yako ulimtaja majina yake?

Shahidi: Sijamtaja.

Kibatala: Umeongozwa kusema chochote kuhusu hali ya silaha kwamba irudishwa kama ilivyochukuliwa?

Shahidi: Niliambiwa kuwa silaha imerejeshwa Polisi  Osterbay.

Hakimu Simba: Nilisharekodi.

Kibatala: Sijamuuliza kuhusu kurejeshwa kwa silaha nilimuuliza kuhusu yeye kuongozwa hali juu ya silaha.

Hakimu Simba:  inawezekana mashahi hawajui maana ya kuongozwa ni maneno ya kishera zaidi  wakili jitahidi sio shahidi ni mwanasheria.

Kibatala:Kabla mimi kukuuliza maswali nataka kukuuliza hali ya silaha ilivyorudishwa silaha?

Shahidi: Labda naomba ufafanuzi wa hali…

Kibatala: Acha nibadili swali… Ni sahihi kwamba mahakama haijui idadi ya  risasi zilizorudi?

Wakili Kadushi: Naomba irekodi  majibu ya shahidi sio anacholishwa na wakili.

Kibatala: Swali langu lipo pale pale mahakama inaufahamu kwamba bunduki ilirudishwa na risasi au haina. 
Mahakama haikuweza kufahamu kuwa bunduki ilikuwa na risasi au laa.
 Tumekubaliana hapo awali umesema mwenyewe silaha ni kitu nyeti sana umetoa nyaraka yoyote kwenye mahakama kuhusu kurejeshwa kwa silaha?

Shahidi: Silaha ilirejeshwa ndio maana sijashtakiwa.

Kibatala:Umetoa nyaraka yoyote kwa mahakama kuhusu kurejesha kwa silaha?

Shahidi:
 Utaratibu wa silaha…

Hakimu Simba: umetoa nyaraka au hukutoa?

Shahidi: Hakuna nyakata ya silaha.

Kibatala:
 Hospitali ulipelekwa lini?

Shahidi:
 Nilipelekwa tarehe 16 Februali mwaka 2018 nikatibiwa hadi tarehe 18 Februali nikarudi kambini kujiuguza.

Kibatala:
 Tunakubalina kwamba tarehe 18 hukuwa kituo cha kazi.

Shahidi:
 Naomba ujue maana ya kuwa kambini na kuwa kituo cha Polisi.

Hakimu Simba: Acha hayo unakwenda mbali…

Kibatala:
 Ni sahihi kwamba kuanzia tarehe 16 Februali hukurudi kwenye doria ya nguvu na nyingine mpaka tarehe 18 Februali na kuendelea ulivyorudi kambini.

Shahidi:
 Sahihi.

Kibatala:
 Ni terehe ngapi ulirudi kazini?

Shahidi: Nilirudi baada ya kumaliza matibabu.

Kibatala: Ni tarehe ngapi shahidi?

Shahidi: Sikumbuki.

Hakimu Simba: Tunakwenda vizuri sasa.


(Kicheko kidogo wote mahakamani).

Kibatala: Ulijiuguza kwa siku ngapi?

Shahidi:
 Sina kumbukumbu kwa sababu nilikuwa natumia dawa na kufanya kazi ndogo ndogo.

Kibatala: Hivi Ofisa wa Polisi kama wewe huwa anakuwa na mapumziko  anavyotaka yeye au?

Shahidi: Askari hupumzika kwa kujiuguza huku akiangaliwa hali yake na viongozi mpaka anapatakiwa kurejea kazini.

Kibatala: Ni sahihi mapumziko yako kama kweli ulipumzika na uliumia ni sawa: mapumzika yako yalibebwa na cheti ulichokuja nacho?

Shahidi: Sikumbuki hiyo D1 si ipo pale.

Hakimu Simba:
 Hakuna ugomvi na wakili msikilize vizuri.

Kibatala: Unafahamu kwamba hiyo nyaraka aliyoandika Daktari alieleza upumzike kwa siku ngapi?

Shahidi: Mimi naomba nieleze kwamba…

Hakimu Simba: Shahidi nishakueleza hii mara ya kumi, kazi yako kujibu maswali.

Kibatala: Nakuuliza tena shahidi unafahamu kwamba hiyo nyaraka aliyoandika Daktari alieleza upumzike kwa siku ngapi?

Shahidi: Mimi sio daktari.

Kibatala: Unafahamu kwamba hiyo nyaraka aliyoandika Daktari alieleza upumzike kwa siku ngapi?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Unafahamu kwenye tukio hilo alifariki mtu anayeitwa Akwelina Akwelin.

Shahidi: Mimi nimesikia kama wewe ulivyosikia.

Kibatala:
 Nakuuliza swali kama unafahamu sema kama hufahamu sema, unafahamu kwamba marehemu alifariki kwenye tukio hilo uliloliita maandamano?

Shahidi:
 Nilisikia.

Kibatala: Unafahamu kwamba hadi leo hii hakuna mtu aliyefikishwa mahakama kwa kumuua Akwelina kwa makusudi au bahati mbaya?

Shahidi:
 Siwezi kujua maana mimi sio mpelelezi.

Kibatala: Unafahamu pia kwamba kuna Askari Polisi wawili wanahusishwa na kifo cha Akwelina?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu au hufahamu kwamba risasi 90 zilipigwa siku ya terehe 16 Februali mwaka 2018 eneo la Mkwajuni.

Shahidi: Siwezi kufahamu kwa kuwa niliumia.

Kibatala: Nimeomba ruhusa ya mahakama kushika hati ya mashitaka na kuangalia shtika la Nne,
Kuna mtu anaitwa PC Fikiri unamfahamu.

Shahidi:
 Namfahamu.

Kibatala: Ni sahihi kwamba PC Fikiri naye kama ulivyo wewe hakuwepo kazini ni sahihi?

Shahidi: Hakuwepo kazini au aliumia?

Kibatala: Vyovyote alikwenda kuogelea vyovyote nachotaka kufahamu alikuwepo kazini siku ya tarehe 16 mwezi wa pili?

Shahidi: Hakuwepo kazini tarehe 16 hadi 18.

Hakimu Simba:
 Muulize vizuri hata sisi tulifeli pengine kwa sababu hatukuelewa maswali ya mwalimu.

Kibatala:
 Ni sahihi kwamba PC Fikiri hakuwepo kazini kuanzia tarehe 16 Februari.

Shahidi: PC Fikiri tarehe 16 Februali alikuwepo kazini baada ya kuumia naye alilazwa hadi tarehe 18 Februari.

Kibatala:
 Shahidi kama unafahamu au unafahamu sema, unafahamu muda wa PC Fikiri kwa muda gani hakuwa kazini?

Shahidi: Siwezi kufahamu kwa muda gani.

Kibatala: Shahidi tusaidie kwanini ulipelekwa Hospitali ya Polisi ya Kilwa Road?

Shahidi: Siwezi nikajua nilijistukia ni pale.

Kibatala: Kuna sheria yoyote ile inayokataza Askari aliyejeruhiwa kutibiwa kwenye hospitali ya Serikali kama Muhimbili au Mwananyamala.?

Wakili Nchimbi: Shahidi aliyekuwepo hapa sio mjuzi wa sheria.

Hakimu Simba: Ukisema tu kuna sheria yoyote tayari umeingia kwenye suala la sheria tulishasema hapo awali

Kibatala: Nabadilisha swali
 kuna kitu chochote kile kinachokataza askari aliyejeruhiwa kutibiwa kwenye hospitali ya Serikali kama Muhimbili au Mwananyamala.

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Ni sahihi kuwa Hospitali ya Mwananyamala ipo kilometa zisizozidi tano kutoka eneo la tukio Mkwajuni?

Shahidi:
 Sio mzoefu wa kupima umbali.

Kibatala: Tukubaliane kwa muda hasa Polisi mkiwa na dharura kwenye gari lenu mnaweza kupenya na kufika kwa haraka sehemu wanayotaka tofauti na mimi Kibatala nikienda kwangu Goba?

Shahidi:
 Sahihi.

Kibatala: Kama ukiondoka pale eneo la Mkwajuni kwa gari la Polisi kuelekea Mwananyamala utatumia muda gani?

Shahidi:
 Siwezi kufahamu mimi sio dereva.

Kibatala: 
Na hivyo hivyo ukiondoka pale eneo la Mkwajuni kwa gari la Polisi kuelekea Muhimbili

Shahidi: Pia Sifahamu.

Kibatala:
 Ni sahihi kuwa Hospitali ya Muhimbili ni kubwa kuliko Hospital ya Kilwa Road?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Kutoka Mkwajuni kwenda Kilwa Road hospitali kuna umbali gani?

Shahidi: Siwezi kufahamu.

Kibatala:
Kutoka Mkwajuni kwenda Mwananyamala na kutoka Mkwajuni kwenda Kilwa Road wapi ni mbali.

Shahidi:
 Siwezi nikajua.

Kibatala: Shahidi kisheria nyaraka ikitolewa naweza kuiuliza maswali unafahamu chochote kuhusu hiyo nyaraka au tumsubiri daktari aje?

Shahidi: 
Tumsubiri daktari.

Kibatala:
 Hii uliyoitoa ni kama ID wakati unatoa ushahidi wako ulitoa nyaraka yoyote iliyokunyesha wewe ulilazwa Kilwa Road?

Shahidi: Kimya

Hakimu Simba: Umetoa hujaitoa.

Shahidi:
 Sijaitoa.

Kibatala:
 Admission form umeitoa au hujaitoa?

Shahidi: Imebaki kumbukumbu hospitalini.

Kibatala: Huyu Koplo Fikiri alitibiwa wapi?

Shahidi: Kilwa Road hospitali.

Kibatala: Mukiwa pale hospitali mlilazwa karibu karibu au kila mmoja pekee yake?

Shahidi:
Tulilazwa wodi ya wanaume.

Kibatala: Fikiri alizimia au aliumia huku akiwa hajazimia.

Shahidi:
 Sikuweza kujua mimi nilizimia.

Kibatala: Mliruhusiwa siku moja au tofauti.

Shahidi: Siku moja.

Kibatala: Siku gani?

Shahidi: Tarehe 18 Februari.

Kibatala: 
Majira ya saa ngapi?

Shahidi:
 Jioni.

Kibatala:
 Shahidi ni sahihi kule Kilwa Road kuna kituo cha Polisi kikubwa  na salama kabisa?

Shahidi:
 Sahihi.

Kibatala:
 Bila shaka umewahi kufika na unakifahamu?

Shahidi:
 Nakifahamu.

Kibatala:
 Na rumande yake unaifahamu?

Shahidi: Siifahamu.

Kibatala: Ulisema mlitoka barabara ya ITV saa na 11 na robo hivi nilivyokurekodi sahihi?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Na mlifika Buibui muda huo huo 11 na robo.

Shahidi: Saa 11 kuelekea 12.

Kibatala: Unakumbuka kusema chochote kuhusu kilipo kiwanja cha Buibui?

Shahidi: Mwananyamala.

Kibatala:
Unakumbuka wakati ushahidi wako ulisema kipo wapi?

Shahidi:
 Nakumbuka nilisema kipo Mwananyamala.

Kibatala:
 Unakumbuka kusema chochote kwamba wale watuhumiwa pale uwanjani walikuwa wakifanya nini?

Shahidi: 
Nilisema.

Kibatala:
 Mwambie ulisema walikuwa wanafanya nini mmoja mmoja.

Shahidi:
 Kimya.

Kibatala:
 Shahidi ulisema kulikuwa na watu saba mtu uliyemtaja hasa Mbowe hawa wengine ulisema wanafanya nini pale Buibui?

Shahidi:
 Nilimuoma Mgombea wa Chadema na baadaye akachukua maiki Feeman Mbowe.

Kibatala: Hebu taja tena jina la Mwenyekiti?

Shahidi: Mbowe

Kibatala: Jina la kwanza?

Shahidi:
 Silifahamu.

Kibatala: Ulipotoa ushahidi awali na ulisema Mbowe ameshika maiki hawa wengine walikuwa wanafanya nini tuanze na Mdee?

Shahidi: 
Niliwaona kwenye viti.

Kibatala: Ulisema awali kwenye ushahidi wako?

Shahidi: Nilisema.

Kibatala: Kwa hiyo ulisema?

Shahidi: Nilisema.

Kibatala:
 Huyu wa katikati pale akionesha walipo (watuhumiwa) alikuwa akifanya nini?

Shahidi:
 Walikuwa wamekaa pale mkutanoni kwenye viti.

Kibatala:
 Shahidi nakuuliza mambo uliyoyasema awali wakati ukitoa ushahidi,
ulisema kwamba hawa wengine ulikuwa wapi?

Shahidi:
 Mimi nilimshuhudia Mbowe na wengine walikuwa washaongea tayari.

Kibatala: Ulimtaja mgombea wakati unaongozwa uliweza kumtambua kumuonesha Mgombea?

Shahidi:
 Niliweza kumtambua.

Kibatala:
 Ni yupi uliyemtambua wakati unaongozwa ulienda ukamshika bega?

Shahidi:
 Hakuna mahala niliposema kuwa huyu ndio mgombea.

Kibatala: Ni sahihi kuwa hukumshika mgombea lakini pia hukumshika mtuhumiwa huyu hapa (Bulaya)?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: 
Uliomba hati mashataka utajiwe na majina na wakili wa Serikali ukaomba majina yao amtaje mmoja mmoja?

Shahidi:
 Nilielekezwa na nimguse mmoja mmoja.

Kibatala: Je uliomba utajiwe majina yao mmoja mmoja?

Shahidi: Sijaomba.

Kibatala: Shahidi wakati unatoa ushahidi wako ulisema kuwa ulimsikia Mbowe ameshika maiki na kuwataja mmoja mmoja kwamba Mdee na fulani twendeni kwa mkurugenzi ulisema?

Shahidi:
 Mbowe hakuwataja kwa majina.

Kibatala: Ukiacha hawa washtakiwa unamkumbuka mtu yoyote kati ya wale 700 iliwataja angalau mmoja?

Shahidi: 
Hapana.

Kibatala: Ulitoa ushahidi ukasema kwamba Mbowe alisema twendeni kwa Mkurugenzi ulisema chochote kwamba wale ni wanachama wa Chadema?

Shahidi:
 Nilisema.

Kibatala:
 Shahidi unapenda mpira wa Uingereza?

Shahidi: Sipendi.

Kibatala:
Uingereza kuna timu inaitwa Crystal Palace  unaifahamu?

Shahidi: Siifahamu.

Kibatala: 
(Jezi zake zinafanan na sare za chadema),Ukitoa askari kanzu askari wote ni lazima wavae sare fulani?

Shahidi: 
Sahihi.

Kibatala:
 Unafahamu kuna sheria inayowataka wanachama wa Chadema wavae sare?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala:
 Ulisema kama nimekusikia vizuri wale watu walibeba fimbo?

Shahidi: Hujanisikia vizuri.

Kibatala:
 Ni sahihi kwamba ulijua kuwa viongozi wa Chadema kuanzia walipokuwa wanatoka pale jukwaani uliposema walikuwa wanahasira wanakwenda wapi?

Shahidi: 
Eee! walitangaza palepale wanapokwenda.

Kibatala:
 Askari uliokuwa nao wangapi?

Shahidi:
 Sita

Kibatala:
 Na SSP Dotto alikuwa na askari wangapi?

Shahidi: Siwezi kujua.

Kibatala:
 Na walikuwa wana mabomu ya machozi?

Shahidi:
 Siwezi kujua.

Kibatala:
 Wewe hapo ulikuwa na mabomu ya machozi:

Shahidi: 
Sikuwa nayo.

Kibatala:
 Ulikumbuka kusema kuwa wewe ulipewa mabomu ya machozi mlipofika pale Mkwajuni kwa maana hukuwa na mabomu ulisema?

Shahidi:
 Sijakumbuka.

Kibatala:
 Ni sahihi mkubwa wako alikuwa SSP Dotto?

Shahidi: Ndio.

Kibatala:
 Ni sahihi kwamba ulipewa oda amri usizuie maandamano palepale viwanja vya Buibui?

Shahidi: Hapana tulikuwa tunaoda kutoka Mzelengi.

Kibatala:
 Unakumbuka kusema kuwa ulipewa amri yoyote kutoka kwa Mzelengi kwa sababu ya moja ama nyengine?

Shahidi: Sikusema.

Mahahakama imekwenda mapumzika ya dakika 20 na baada ya muda huo ikarejea na Wakili Profesa Abdallah Safari anaaga kuwa mahakama ikirejea hatokuwepo kutokana na dharura aliyokuwa nayo.

Ameanza wakili wa Serikali Faraja Nchimbi alieleza mahakama kuwa  safu ya utetezi imepungua ambapo kiongozi wa Jopo Prof. Safari ameondoka  ikiwa safu yao ipo sawasawa…Kibatala anaendelea.

Kibatala:
 Shahidi nilikuuliza iwapo ulisema mahakamani kama ulipewa maelekezo na Inspeta Mzelengi au Afande Dotto juu kuzuia maandamano .

Shahidi: Sijasema lolote.

Kibatala:
 Hivi Shahidi uwanja wa Buibui kuna magari yanapita pale?

Shahidi: Hapana.

Kibatala:
 Pale Buibui uliposema watu 700 wamekusanyika ni uwanja au Barabara?

Shahidi: Ni Uwanja .

Kibatala: 
Na huko Mkwajuni ni uwanja au Barabara?

Shahidi: Barabara

Kibatala:
 Ni sahihi mara baada ya kushika maiki Mbowe maandamano yalianza pale?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala:
 Tueleza kuzuia maandamano Buibui au Kule Barabarani ipi ina madhara?

Shahidi: Ina madhara pale viwanja vya Buibui.

Kibatala:
 Ule uwanja wa Buibui upoje unaweza kumudu watu wa ngapi?

Shahidi: Ule uwanja ni sehemu za michezo.

Kibatala:
 Mle ndani ya uwanja kuna maduka?

Shahidi: Sijayaona.

Kibatala:
 Pale Buibui gari za kubeba wagonjwa Amburance uliziona au hujaziona?

Shahidi: Sijaziona.

Kibatala:
 Je kituo cha mabasi ya Mwendokasi kipo hakipo.

Shahidi: Hakuna kituo cha Mwendokasi?

Kibatala:
 Na tunakubaliana kuwa basi la Mwendokasi haliwezi kupita pale Buibui?

Shahidi: Haliwezi kupita.

Kibatala:
 Tunakubalina mabasi ya kawaida hayapiti pale uwanjani.

Shahidi: Ndio

Kibatala:
 Tunakubaliana Shahidi kwamba maandamano hamkuyazuia pale Buibui?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala:
 Bali kwa ushahidi wako mlikwenda kuyazuia maandamano kwenye barabara ya Kawawa?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: 
Ni sahihi nilikusikia wewe na askari wenzako mlipita njia za vichochoroni kuelekea Mkwajuni?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: 
Ni sahihi nyie mliyafuata maandamano nyuma nyuma?

Shahidi: Hapana

Kibatala: 
Kwa hiyo wewe yale maandamano yalipita wapi hujui?

Shahidi: Maandamano nilisema tangu mwanzo yalianzia Buibui kupitia barabara ya Mwananyamala mpaka barabara Kawawa.

Kibatala:
 Wewe na wenzako mliruhusu ule mkusanyiko uondoke. Ndio maana hamkujua kama waandamanaji walipita njia gani kwa vile hamkuwa nyuma yao?

Shahidi: Hatukuongozana.

Kibatala:
 Kwa hiyo wewe maandamano hujui yalipita wapi?

Shahidi: Nafahamu walipita njia ya Mwananyamala.

Kibatala:
 Kwa hiyo kwa kile kilichotokea katikati hukifahamu?

Shahidi: Sikifahamu labda aje askari mwengine.

Kibatala:
 Mimi nakuuliza wewe simuulizi mwengine. Sasa hiyo barabara ya pembeni mlizopita ulimtajia Hakimu?

Shahidi: Nilitaja.

Kibatala:
 Majina ya hizo barabara ulitaja?

Shahidi: Sikuweza kuzitaja.

Kibatala: 
Turudi Buibui uwepo wako pale kwangu mimi ni muhimu sana na mlisema kwamba mlikuwa na gari hilo gari ulilitaja?

Shahidi: Tulikuwa na Land lover…

Kibatala:
 Uliitaja au hukulitaja?

Wakili Kadushi: (amesimama) Sio vizuri kumuiingilia shahidi kuna maswali yanahitaji ufafanuzi?

Kibatala: 
(Anaendelea), Hilo gari umetaja au haukutaja?

Shahidi: Nilitaja gari sikutaja aina ya gari.

Kibatala:
 Kuna usajili wa gari na kuna usajilinwa kipolisi ulitaja code name (namba ya utambulisho maalumu ya gari) ya gari la polisi mlilotumia. Shahidi ulitaja namba ya usaji wa hiyo gari?

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala:
 Unasema baada mkafika pale Mkwajuni unakumbuka kusema chochote kuhusu hali iliyoluwa pembeni ya barabara?

Shahidi: Sikusema.

Kibatala:
 Ulisema chochote kuhusu hali ya wananchi waliokuwepo pale.

Shahidi: Sijasema.

Kibatala: 
Naposema wananchi simaanishi wale waliokuwa wanaandamana namaanisha Wazee, Watoto na wale Wafanyabiashara wa eneo hilo. Ulisema chochote kuhusu watoto au wazee waliokuwepo?

Shahidi: Sijawataja.

Kibatala:
 Shahidi wewe ndio uliyekuwepo pale kama kweli ulikuwepo unakumbuka kusema chochote kuhusu basi au mabasi ya Mwendokasi?

Shahidi: Nilisema.

Kibatala:
 Ulisema nini?

Shahidi: Nilisema wakati watu walivyoandamana mabasi yalikuwa yamesimama.

Kibatala:
 Unakumbuka kusema chochote kuhusiana na gari za wagonjwa (Amburance)?

Shahidi: Sikusema.

Kibatala:
 Ulisema chochote kuhusu washtakiwa wakirusha mawe waliosema kurusha jiwe?

Shahidi: Sikuona.

Kibatala:
 Nimesema hivyo kwa sababu shtaka la nne limawakabili watuhumiwa ni kukujiruhi wewe. Mlifanikiwa kumkamata aliyekurushia jiwe?

Kibatala: 
Hatujawahi kumkamata.

Kibatala:
PC Fikiri alipata madhara ya kiafya kutokana na nani?

Shahidi: Mimi siwezi nikajua.

Kibatala:
 Pale mkwajuni kama kweli ulikuwepo Fikiri ulikuwa naye karibu?

Shahidi: PC Fikiri alikuwepo.

Kibatala:
 Kwa ushahidi wako wewe na wenzako PC Fikiri mlimuona au hamjamuona?

Shahidi: Nilimuona.

Kibatala:
 Mlikuwa umbali wa kiasi gani?

Shahidi: Hatukuwa na umbali wowote.

Kibatala:
 Shahidi umbali ulipokuwepo wewe na PC Fikiri unaufahamu au huufahamu?

Shahidi: hakuwa mbali.

Kibatala:
 Nani alianza kuumia kati yako wewe na PC Fikiri?

Shahidi: Siwezi nikajua.

Kibatala:
Ulishuhudia Fikiri akiumia?

Shahidi: Aaaa! sijashuhudia.

Kibatala:
 Hebu tukubaliane kwenye mambo ya msingi..hebu tusaidie makadirio ya umbali unayafahamu au huyafahamu… kukadiria mbali huwezi au unaweza?

Shahidi: Sina utaalamu huo.

Kibatala: 
Shahidi hebu chagua mwenyewe nikuulize au nisikuulize kuhusiana na umbali?

Hakimu Simba: Chagua wewe.

(Kicheko kidogo)

Kibatala:
 Unakumbuka hapo awali ulipokuwa ukitoa ushahidi mambo ya umbali uliyazungumzia kwa usahihi?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala:
 Unafahamu wasomi wenzangu walipokuwa wakikuhoji walikuwa wakiuliza kuhusiana na umbali ili kujua kipengele cha utambuzi?

Hakimu: Unapojibu ujibu kwa sauti

Watuhumiwa wote walieleza na wao hawamsikii shahidi akijibu maswali.

Kibatala:
 Mara kadhaa Wankyo (wakili wa Serikali) alisisitiza suala la umbali kati yako na washtakiwa unafahamu kwanini?

Shahidi: Siwezi kukumbuka.

Kibatala:
 Unakumbuka kusema chochote kuhusiana na gari lenu lilipaki eneo gani hasaa pale Mkwajuni?

Shahidi: Yalipaki sehemu ya mteremko sehemu kama unaelekea Magomeni.

Kibatala:
 Kuna barabara mbili huku mbili huku na katika kati Mwendokasi ulieleza gari yenu ilipaki barabara ipi?

Shahidi: Tulikuwa tumepaki katika ya barabara ya Mwendokasi.

Kibatala:
 Hiko ndicho ulichomwambia hakimu?

Shahidi: Nilisema.

Kibatala:
 Ni sahihi kwamba SSP Ngichi alikuwa ndio msimamizi Mkuu pale?

Shahidi: Ndio.

Kibatala:
 Ni sahihi kuwa yeye ndiye aliyekuwa anapanga msimame wapi?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala:
 Sahihi Ngichi ndiye anayejua umbali?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala:
 Shahidi mnasema mlirushiwa mawe na chupa za maji?

Shahidi: Chupa za maji na mawe.

Kibatala:
 Chupa za maji kama hii (alionesha chupa ya maji ya ujazo wa nusu lita akiwa tupu)?

Shahidi: Kama hiyo ilikuwa ina maji.

Kibatala:
 Unasema mlikuwa askari wangspi eneo hilo?

Shahidi: Sina kumbukumbu.

Kibatala:
 Hata kukadiria huwezi?

Shahidi: Sitakuwa na uhakika wa ididi ya askari.

Kibatala:
 Wewe binafsi ulihifadhi chupa, jiwe au fimbo mlizorushiwa kama ushahidi?

Shahidi: Sikujifadhi.

Kibatala:
 Jiwe ambalo limekupiga mpaka unakuja kutoa ushahidi uliliona?

Shahidi: Sijawahi kuliona.

Kibatala:
 Wakati unatoa ushahidi hawa watuhimiwa tisa uliweza kusema chochote walifanya chochote kwa mmoja mmoja?

Shahidi: Sijasema.

Kibatala:
 Na ni ushahidi wako kama ulivyosema awali kwamba hawa watuhumiwa walikuwa mbele kabisa?

Shahidi: Kimya.

Kibatala:
 Shahidi hebu twende kwenye ufyatuaji lengo hasa ni  kuwadhuru ili kuwazuia waandamanaji wasiendelee.

Shahidi: Mabomu ya machozi yanapigwa eneo ambalo…

Hakimu Simba: Sikiliza swali hatuhutaji elimu.

Kibatala:
 Shahidi lengo lake ni kudhibiti watu  ndio maana yakaitwa  mabomu ya machozi?

Shahidi: Sahihi kabisa.

Kibatala:
 Shahidi unakumbuka sehemu ambayo hilo jiwe limekupiga na ukamuonesha Hakimu?

Shahidi: Nilimuonesha Dokta hapa sijamnesha Mheshimiwa.

Kibatala:
 Kabla ya PF3 (fomu ya polisi ya matibabu) hii kukufikia wewe uliwahi kuongea na Ofisa wa Polisi?

Shahidi: Hapana.

Kibatala:
 Mwambie hakimu hiyo PF3 imekufikia muda gani, siku gani saa ngapi?

Shahidi: Tarehe 16 Februari mwaka 2018.

Kibatala:
 Saa ngapi?

Shahidi: Siwezi kukumbuka saa ngapi.

Kibatala:
 Wewe ulifahamu kama kuna PF3 siku gani?

Shahidi: Siku ya tatu.

Kibatala:
 Ambayo ilikuwa tarehe ngapi?

Shahidi: Tarehe 18 mwezi wa pili, kuhusiana na suala la PF3 tarehe hiyo wakati naruhusiwa kuondoka nikagundua kuna PF3 kwenye file.

Kibatala:
Nataka uninyooshee maelezo vizuri daktari alikupa. Je hiyo PF3 ulipata nafasi ya kusoma maudhui yake?

Shahidi: Sikupata kuisoma kwa sababu mimi sio mtaalam.

Kibatala:
 Kilichokufanya ugundue hiyo ni PF3 ni nini?

Shahidi: Kwa sababu niliona namba yangu ya kijeshi na jina langu.

Kibatala:
 Unataka kututhibitishia  kwamba ulioona na kuijua baada ya kuona namba yako ya Jeshi na Jina lako?

Shahidi: PF3 haitolewi kwa askari tu hata kwa raia.

Hakimu Simba: limafahamika hilo jibu swali?

Kibatala:
nakuuliza shahidi kwamba ulijua kuwa hiyo ni PF3 baada ya kuona namba yako ya Jeshi na Jina lako?

Shahidi: Ndio nilitambua.

Kibatala:
 Wewe binafsi hukuwahi kuishika kuisoma na haijawahi kupita mikononi mwako kwa namna yoyote ile?

Shahidi: Wakati natibiwa ilikuwa kwenye file na irejeshwa kwenye file.

Hakimu Simba: Muulize tena.

Kibatala: 
Hiyo PF3 iliwahi kupita mikononi mwako.

Shahidi: Sijawahi kuiona.

Kibatala:
 Kule Polisi unamfahamu Polisi aliyejaza hiyo PF3?

Shahidi: Imejazwa na Dokta Mkuu .

Kibatala:
 Ofisa wa Polisi aliyejaza PF3 unamfahamu au humfahamu.

Shahidi: Kule Polisi au hospitali.

Hakimu anakuuliza kule Polisi.

Shahidi: Afande kule Polisi simfahamu.

Kibatala:
 Ni sahihi kilichojazwa mle hukifahamu?

Hakimu Simba: Amesema anachokifahamu alisema ni namba zake.

Kibatala: 
Mwambie Hakimu ni sahihi kwamba mimi wakili ambaye sijawahi kupigwa bomu la machozi nikipigwa bomu la machozi naweza kuzimia mpaka nikalazwa?

Muda huo huo Mtuhumiwa namba sita Mashinji anaomba ruhusa anamueleza Hakimu kuwa anajisikia kichefuchefu anaruhusiwa kutoka nje kesi inasimama.

Hakimu Simba anatoa dakika 10 kwa ajili ya kuangalia hali ya Mashinji kama ataweza kuendelea na kesi.

Zilipofika Dakika 10 na Mashinji ameshindwa kurejea kwenye chumba cha mahakama.

Kibatala sasa hivi ni saa 10 na dakika 10 na tumeshauriana na mawakili wa Serikali ambao wanajua hali ya Mshitakiwa wa sita Mashinji kuwa sio mzuri na mimi bado nina maswali mengi tumeona kesi hii iahilishwe mpaka siku nyingine.

Wakili Nchimbi amesema upande wa mashtaka hauna pingamizi kutokana na hali iliyoelezwa.

Hakimu Simba ameahilisha kesi hiyo mpaka tarehe 31 Mei mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!