October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali za Mitaa zaonywa matumizi ya fedha

Spread the love

MAMLAKA za Serikali za Mitaa nchini zimetakiwa kuhakikisha kuwa fedha zote zinazokusanywa katika mapato zinawekwa benki na fedha hizo zitumike katika kutekeleza matumizi husika. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhandisi Joseph Nyamhanga katika hafla ya upokeaji wa mashine za Kielektronic POS270 kutoka kwa Serikali ya Dernmark leo jijini Dodoma katika Ukumbi wa Reforms uliopo katika ofisi za OR-TAMISEMI.

Alisema makatibu Tawala wa Mikoa wawe makini katika ukusanyaji wa mapato ili  kutimiza azma ya serikali ya kuongeza udhibiti na kuleta tija katika ukusanyaji wa mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha fedha ilokusanywa inahifadhiwa benki kabla ya matumizi yoyote.

Aidha Mhandisi Nyamhanga ameongeza kuwa jitihada hizi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano zitasaidia kuongeza kipato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kupunguza utegemezi na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa watanzania wote.

Lakini pia Mhandisi Nyamhanga ameeleza kuwa matumizi ya mashine hizo yataziba mianya ya upotevu wa mapato unaosababishwa na watumishi wasio waadilifu katika nyazifa zao.

Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa Halmashauri 18 zilizopata kunufaika na mashine hizo ni halmashauri ya mikoa ya Kigoma na Dodoma.

Kwa kuongezea Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt.Charles Muhina amesema kuwa hafla hiyo ya kukabidhi mashine hizo kwa mikoa hiyo ni mwendelezo wa kuziwezesha Halmashauri kuwafikia walipa kodi waliopo kwenye maeneo yao na kuongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao.

“Sisi OR-TAMISEMI jukumu letu ni kufanya ufuatiliaji na tathimini ya utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha kuwa mradi husika unatekelezwa  kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za nchi hii” Ameongezea Dkt. Muhina

Kwa  upande wake Mkurugenzi wa TEHAMA OR-TAMISEMI Erick Kitali ametoa wito kwa halmashauri kuwa na kifaa maalumu cha kuzuia radi ili kutatua changamoto ya mitandao ya mifumo ya mapato kaharibiwa radi kipindi cha mvua  katika halmashauri hizo.

Naye Kiongozi wa Mradi Maboresho ya Mazingira ya Biashar Flemming Olsen ametoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano waTanzania  kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa ufasaha kwani kuna wafanya biashara wanabidhaa ya thamani kubwa lakini wanalipa ushuru mdogo.

Wakati huo huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Rashid Mchatta amesema kuwa atakwenda kusimamia vyema mashine hizo ili zifanye kazi ipasavyo na itasaidia kuongeza mapato katika maeneo yao ya kazi.

Katika hafla hiyo Mhandisi Nyamhanga amehitimisha kwa kutoa shukurni za dhati  kwa niaba ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi wa Serikali ya Denmark kupitia Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania na kusema kuwa ushirikiano wa nchi hizi mbili utaleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla.

error: Content is protected !!