SERIKALI imetupia mzigo vyama vya ushirika kwa kutofanya kazi yao ipasavyo ya kuwasajili na kuwatambua wakulima wa korosho. Anaripoti Mwandishi Maalum…(endelea)

Japhet Hasunga, Waziri wa Kilimo ndiye aliyetoa malalamiko hayo na kukiri kuwa, malipo ya wakulima yamekuwa yakikumbana na changamoto.

Akizungumza jana tarehe 19 Februari 2019 wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Hasunga amesema “vyama vya ushirika ndivyo vinapaswa kuwajua na kuwatambua wakulima wake katika mazao yote yanayouzwa kupitia mfumo huo.”

Amesema “vinginevyo kutofanya kazi kwa weledi kumetuchelewesha kwa kiasi kikubwa. Hata sheria yetu ya maghala haikufanya kazi vizuri, vyama vya msingi havikutekeleza majukumu yake.”

Aidha, Hasunga amesisitiza kwamba, serikali haitalipa wafanyabiashara wa zao la korosho wasiotambulika maarufu kama ‘Kangomba’.

Akifafanua kuhusu msisitizo huo ameeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria ya korosho kifungu cha 12, mtu yeyote asiyesajiliwa na kutokuwa na leseni ya biashara ya korosho haruhusiwi kufanya biashara hiyo.

Katika hatua nyingine, Hasunga amesema serikali haitawavumilia wanaofanya biashara hiyo kinyume na sheria badala yake watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.