SERIKALI imetoa tahadhari kwa umma kuhusu uwepo wa tishio la ugonjwa wa Ebola kufuatia ugonjwa huo kulipuka nchi ya jirani ya Uganda. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Ummy ametoa tahadhari hiyo kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu baina ya nchi ya Uganda na Tanzania kupitia mipaka rasmi na isiyo rasmi. Huku akisema kwamba mikoa ya Kagera, Mwanza na Kigoma iko kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na mlipuko wa Ebola.
Kufuatia tishio hilo, Ummy ameiagiza mikoa na halmashauri zote nchini kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wizara yake katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.
“Hivyo ninaitaka Mikoa na Halmashauri zote nchini kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na @wizara_afyatz katika kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola. Aidha ninawataka wananchi ktk mikoa yote kuchukua hatua stahiki za kujikinga na ugonjwa huu ili usiingie nchini. #TishioLaEbola,” inaeleza taarifa ya Ummy.
Aidha, Ummy amefanya ziara katika Uwanja wa Ndege Mwanza na Kituo kipya cha kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kilichopo Buswelu, Ilemela jijini Mwanza.
“Leo nimefanya ziara katika uwanja wa ndege Mwanza na Kituo kipya cha kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kilichopo Buswelu, Ilemela jijini Mwanza. Lengo ni kupima utayari wetu wa kukabiliana na ugonjwa huu nchini,” amesema Ummy na kuongeza.
“Hata hivyo, kwa hali ilivyo na kutokana na ukweli kuwa ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na haraka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine ni kwamba takribani nchi nzima iko katika hatari ya kupata mlipuko wa ugonjwa huu.”
Ninatoa Tahadhari kwa Umma kuhusu uwepo wa tishio la Mlipuko wa Ebola nchini kwetu kufuatia kuwepo kwa ugonjwa huu Uganda. Hii ni kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu baina ya nchi hizi kupitia mipaka rasmi na isiyo rasmi. Mikoa ya Kagera, Mwanza na Kigoma ipo ktk hatari zaidi. pic.twitter.com/B9N14Sa15g
— Ummy Mwalimu MP (@ummymwalimu) June 15, 2019
Leave a comment