Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Serikali yatoa majibu sintofahamu zao la korosho
Habari Mchanganyiko

Serikali yatoa majibu sintofahamu zao la korosho

Spread the love

SERIKALI yatoa majibu kuhusu sintofahamu ya zao la korosho, iliyojitokeza kufuatia hatua yake ya kuingilia kati uuzaji wa korosho ghafi za msimu wa mwaka 2018/2019. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Akizungumza na wanahabari jana tarehe 20 Septemba 2019 jijini Dar es Salaam, Japhet Hasunga, Waziri wa Kilimo alikiri kwamba hatua hiyo ya dharula ilileta changamoto katika tasnia ya zao la korosho, ikiwemo baadhi yao kutolipwa fedha zao, na kusua sua kwa zoezi la uandaaji wa mashamba.

Lakini pia, hatua hiyo ilisababisha soko la korosho kuvurugika katika msimu wa 2018/2019.

Kufuatia changamoto hizo, Hasunga amesema serikali imekuja na majibu yake, ili kuhakikisha hazijirudii kwenye msimu ujao wa korosho wa mwaka 2019/20.

“Serikali iliamua kununua korosho zote toka kwa wakulima kutokana na kuyumba au kushuka kwa bei ya korosho katika soko la minada, hatua hii ilikuwa ya dharula. Ilichukuliwa ili kulinda masilahi ya wakulima. Mtakumbuka kwamba tulipoenda kwenye hilo zoezi utekelezaji wake tulikutana na changamoto nyingi na hivyo hatukuweza kwenda kama ilivyotaratijiwa,” ameeleza Hasunga.

Hata hivyo, Hasunga amesema serikali iliwakopesha pembejeo wakulima, hasa wale waliochelewa kulipwa fedha zao, na kuwa ilifanya hivyo ili kuwawezesha kuandaa mashamba yao kwa ajili ya kupata korosho nyingi.

“Sasa hivi wakulima wengine walikuwa hawajalipwa, na upatikanaji pembejeo ilikuwa ni shida, tulikuwa na utaratibu wa kukopesha pembejeo wakulima. Tumetoa mikopo ya pembejeo kwa wakulima na hiyo imesaidia sana kuhakikisha uzalishaji unaongezeka,” amesema Hasunga.

Hasunga amesema serikali imepatia majibu changamoto zilizojitokeza hasa ya soko kuvurugika, akieleza kwamba, msimu ujao ununuzi utafanyika kwa njia ya mnada iliyoboreshwa, ambapo wanunuzi wa nje ya nchi watashiri minada kwa njia ya kidigitali.

Hasunga amesema minada hiyo ya wazi itasimamiwa na Jukwaa la Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), huku wageni wakishiriki kwa kutumia Mfumo wa Wizara ya Kilimo wa Kusimamia Biashara za Kilimo (ATMIS).

Akifafanua kuhusu mfumo huo, Hasunga amesema wanunuzi wa nje watakao taka kushiriki katika minada hiyo, lazima wajisajili na kupatiwa msimbo maalumu (Code) watakaoutumia kuingia kwenye mfumo wa ATMIS, kwa ajili ya kushiriki.

“Kampuni inayotaka kushiriki katika minada tunayoendesha kununua korosho za Tanzania, ni kipindi cha kuanza usajili kwa kuingia katika mfumo wa wizara ya kilimo. Wataonesha kiasi cha korosho wanachohitaji upande wa tani, bei hawataonesha,” amefafanua Hasunga.

Hasunga amesema minada itafanyika mara mbili kwa wiki, na itaoneshwa kupitia mfumo wa ATMIS. Lakini pia, serikali itaweka ubao wa kidigitali kwenye maeneo ya wakulima wa korosho ili na wao waone minada inavyoendeshwa kwa uwazi.

“Tumetoa nafasi katika huo mfumo, wakulima kuwa na bei yao elekezi, ambayo watakuwa nayo wao. Kama bei haijafika kiwango hiki sisi mzigo wetu hatuuzi. Bei hiyo wateja hawatajua lakini serikali kupitia vyama vya msingi watajua,” amesema Hasunga na kuongeza;

“Wakati minada inaendeshwa tutaweka ‘screen’ kwenye komputa katika maeneo mbalimbali ya wakulima wa korosho. Uwazi utakuwepo, wakulima watajua nini kinaendelea sokoni.”

Hasunga amesema serikali itatoa kipaumbele kwa wanunuzi wa ndani ya nchi, ili viwanda viweze kujiendesha na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.

“Tunakuja na utaratibu mpya wa kuhakikisha kwamba, viwanda vyetu kwanza vinapewa nafasi ya kununua malighafi zinazotumika katika kuongeza thamani. Kama tunavyojua viwanda vyetu kwa muda mrefu vilikuwa vinashindwa kufanya ubanguaji kwa kushindwa kushindana kwenye bei,” amesema Hasunga na kuongeza;

“Fedha za kununua mzigo wa kutosha wa mwaka mzima havina, kutokana na hilo tumeamua kutoa upendeleo kwa wenye viwanda kwanza kupewa mzigo ili kila mtu kwa kadri anavyohitaji kupata mzigo wa kutosha. Kwa kufanya hivyo, itatusaidia kuongeza thamani, la pili kutengeneza ajira nyingi hapa nchini.”

Hasunga amesema uzalishaji wa korosho katika kipindi cha miaka miwili ijayo utaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya mikoa inayolima zao hilo, kutoka mikoa 5 hadi kufikia mikoa 17 ambayo serikali imetoa pembejeo kwa wakulima kuanzia msimu wa 2019/20.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

DAWASA waanza utekelezaji agizo la Samia

Spread the loveMamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam...

Habari MchanganyikoKimataifa

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the loveTUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais wa...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

error: Content is protected !!