NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mwita Waitara ametoa wito kwa wananchi na wadau wa maendeleo kushirikiana na serikali katika kukarabati nyumba za walimu nchini. Anaripoti Danson Kaijage … (endelea).
Waitara ametoa wito huo leo tarehe 12 Aprili 2019 bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje aliyehoji mpango wa serikali katika kuboresha nyumba za walimu pamoja na shule kongwe katika jimbo lake.
Akijibu swali hilo, Waitara amesema nyumba za walimu zinazohitaji kufanyiwa ukarabati ni nyingi na kwamba uwezo wa serikali si mkubwa, na kuwaomba wadau kutoa michango yao katika kufanikisha ukarabati wa nyumba za walimu nchini.
Hata hivyo, Waitara amesema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2019/2020 wizara yake imetenga kiasi cha fedha , kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za walimu na shule kongwe nchini.
“Si kweli kwamba tunakarabati shule tu, isipokuwa ukweli ni kwamba tunakarabati shule nyingi kuliko nyumba za walimu, hata kwenye kitabu cha bajeti ya mwaka huu tunachojadili sasa yako maeneo ya kupitia katika majimbo mbalimbali,” amesema na kuongeza Waitara.
“Tumetaja maeneo hayo na fedha zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za walimu. Uwezo wa serikali si mkubwa sana tunaomba mheshimiwa mbunge na wadau mbalimbali tushirikiane katika jambo hilo ili kupunguza shida ya walimu.”
Aidha, Waiatara amesema serikali itaendelea kukarabati miundombinu ya elimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Leave a comment