SERIKALI ya Tanzania imesema, ada za shule nchini humo zilipwe kulingana na makubaliano yaliyofikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaaam … (endelea).
Kauli hiyo ya Serikali, imetolewa leo Ijumaa tarehe 26 Juni 2020 na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikielezea maelekezo ya ulipaji ada za shule binafsi baada ya janga la corona.
Maelekezo hayo yanatolewa kipindi ambacho kumekuwa na mivutano kwa baadhi ya shule binafsi na wazazi au walezi juu ya gharama wanazopaswa kulipwa pindi shule zitakapofunguliwa Jumatatu ya tarehe 29 Juni 2020.
Shule zote za msingi na sekondari zinafunguliwa baada ya kufungwa kuanzia tarehe 17 Machi 2020 ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).
“Wizara inaelekeza na kusisitiza, wanafunzi wote wapokelewe kwa ajili ya kuendelea na masomo ifikapo tarehe 29 Juni 2020,” inaeleza taarifa hiyo ya wizara iliyotolewa na Sylvia Lupembe, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara hiyo.
Sylvia amesema, kulinga na ratiba iliyotolewa na wizara, wanafunzi wanatarajiwa kukamilisha masomo kama inavyoelekezwa na mihtasari ya madarasa waliyopo.
“Hivyo, ada za shule zilipwe kulingana na makubaliano yaliyofikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo. Wizara inaendelea kusisitiza maelekezo ya awali kwamba kusiwepo na nyongeza yoyote katika kiwango cha ada,” amesema
Katika taarifa hiyo, inasema “wazazi pia wanatakiwa kuzingatia kiwango cha ada huwa kinakadiriwa kwa kuzingatia gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule, gharama ambazo ziliendelea kuwepo hata muda ambao shule zilikuwa zimefungwa.”
“Gharama hizi ni pamoja na mishahara ya watumishi, Ankara za umeme na maji,” amesema Sylvia.
Kuhusu malipo ya chakula na usafiri, “wizara inazielekeza kamati/bodi za shule kufanya uchambuzi wa gharama inayopaswa kupungua kwa siku ambazo wanafunzi hawakuwa shuleni. Tathimini hii izingatie ratiba mpya ya mihula iliyotolewa na wizara.”
Taarifa hiyo imesema, kulingana na Sheria ya Elimu, Sura Na. 353 (RE 2002), uendeshaji wa shule unasimamiwa na kamati/bodi za shule, vyombo ambavyo vimeundwa kwa mujibu wa sharia hiyo.
“Hivyo, wamiliki wa shule wanaelekezwa kuzingatia sharia hiyo na kuzipa nafasi bodi/kamati za shule kutekeleza majukumu kulingana na sharia iliyoziunda.”
“Kwa kuzingatia kwamba, Serikali ilifunga shule wakati muhula wa masomo ukiwa unaendelea, wizara inaelekeza kwamba wanafunzi wote wapokelewe na kuendelea na masomo yao bila kikwazo chochote ili kukamilisha muhula huo,” imeeleza
Tahadhari kuhusu virusi vya Corona
Ni kunawa mikono tu? Au pia na kuvaa barakoa na kutokukaribiana? Wataalamu wa afya wanasemaje?