Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali ya Tanzania yaipa THRDC siku saba kujieleza
Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Tanzania yaipa THRDC siku saba kujieleza

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Spread the love

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umepewa siku saba  na Serikali kujieleza kwa nini usichukuliwe hatua za kisheria, kutokana na kukiuka Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, jana Jumatano tarehe 24 Juni 2020, THRDC wanatakiwa kuwasilisha utetezi huo ndani ya siku saba, kuanzia jana.

Pia, THRDC imetakiwa kuacha mara moja shughuli zinazokwenda kinyume cha sheria za nchi.

“THRDC wanatakiwa kuacha mara moja shughuli hizo kuanzia siku ya kutolewa kwa barua hii na imepewa siku saba kueleza kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria kutokana na ukiukwaji waliyofanya,” inaeleza barua hiyo.

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Kwa mujibu barua hiyo, THRDC wanadaiwa kukiuka sheria , kutokana na kutowasilisha nyaraka za usajili wa wanachama wake wote, ili ikamilishe usajili.

“THRDC walitakiwa kuwasilisha orodha na nakala za vyeti vya usajili vya wanachama wake wote, ili kukamilisha usajili. Hata hivyo hadi leo Ofisi ya Msajili haijapokea nyaraka kama ilivyoagiza,” inaeleza barua hiyo.

Pia, THRDC wanadaiwa kutowasilisha kwa Ofisi ya Msajili wa NGO’s, mikataba au makubaliano ya fedha za ufadhili, kinyume cha Kifungu Na. 13 (B) na (C) cha Sheria ya NGO’s , iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2018.

“Kwa kuongezea THRDC kama ilivyo mashirika mengine yanayopokea fedha za misaada kutoka kwa wafadhili, inatakiwa wawasilishe mikataba ya ufadhili kwa ajili ya kupewa ruhusa kabla ya utekelezaji wa mradi husika, “ inaeleza barua hiyo.

Wadau wa THRDC

“Lakini hadi leo hawajawasilisha mkataba wowote wa ufadhili au makubaliano, licha ya kwamba imepokea baadhi ya fedha za misaada, hii ni kinyume cha sheria, inayotaka mashirika kuwasilisha mikataba ya ufadhili yenye thamani zaidi ya Sh. 20 milioni  ndani ya siku 10 baada ya makubaliano ya mikataba hiyo kufanyika.”

Sambamba na hayo, barua hiyo ya Ofisi ya Msajili inadai kwamba, mara kadhaa imeshuhudia THRDC ikiratibu shughuli mbalimbali za NGO’s,  kwa kivuli cha kwamba wamepoteza  usajili au hazijasajiliwa, kinyume cha  Sheria ya NGO’s  Na. 24 ya mwaka 2002, inayotaka mashirika husika kusajiliwa na msajili wa NGO’s.

“Ofisi ya msajili imeona NGO’s  zilizo chini ya THRDC, zinashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa  na ya ndani, kinyume cha sheria,” inaeleza taarifa hiyo.

MwanaHALISI ONLINE  leo Alhamisi tarehe 25 Juni 2020, imemtafuta kwa simu Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa THRDC kwa ajili ya ufafanuzi wa suala hilo.

Olengurumwa amesema, wameipokea barua hiyo na kwamba wanaifanyia kazi, ikiwemo kupeleka sababu kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria kutokana na sakata hilo.

Kuhusu tuhuma zilizotolewa na Ofisi ya Msajili wa NGO’s, Olengurumwa amesema atazungumzia suala hilo, baada ya kupeleka majibu yao kwa msajili huyo.

“Barua imetufukia nadhani labda kwa sasa hivi tunajaribu kuifanyia kazi, kwa hiyo kwanza tuandike hiyo barua, ikifka siku saba tutawapa majibu na kutoa ufafanuzi wa makosa yaliyoainishwa kwenye barua hiyo,” amesema Olengurumwa na kuongeza:

“Tutafanyia kazi na kuwajibu baada ya hapo tujue wanataka nini, hivyo watakapotujibu tutawaita (wanahabari) ili kuja kueleza kitu gani kimetokea, baada ya hapo kama kutakuwa na kingine tutawaeleza,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

error: Content is protected !!