JOSEPH Mbilinyi ‘Sugu’ Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini (Chadema) ameing’ang’ania serikali kwenye suala la mustakabali wa mafao ya askari Magereza. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Sugu akiuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri wa Fedha Dk. Ashatu Kijaji amesema kuwa askari magereza wanafanya kazi ngumu ya kulinda wahalifu lakini wanapostaafu serikali inawacheleweshea stahiki zao zaidi ya miaka miwili.
“Mheshimiwa spika, serikali inasema kuhusu askari hawa ambao wamekuwa wakisumbuliwa kutolipwa stahiki zao baada ya kustaafu wakati polisi wanaotukamata na kutupiga wanalipwa mapema lakini wahalifu wote wanarundikwa magereza kwa hiyo hawa wanakuwa na kazi ngumu,” amesema Sugu.
Spika wa Bunge Job Ndugai amesema kuwa swali hilo licha ya kuwa ni refu lakini ameamua kuliacha lijibiwe kwani limeulizwa na mtu mzoefu kuliko maswali mengine yanayoulizwa kwa ubabaishaji.
Akijibu swali hilo na swali la msingi kutoka kwa mbuge wa Viti Maalum, Lucy Mlowe (Chadema), Naibu Waziri wa Fedha Dk. Ashatu Kijaji amesema Serikali inalipa mafao kwa wastaafu wote bila ya upendeleo na kuwa katika kipindi cha hivi karibuni, zililipwa jumla ya Sh 282 bilioni kwa wastaafu mbalimbali.
Naibu waziri amewaondoa hofu pia watumishi wote walioajiriwa katika miaka ya 1980 kupitia Serikali Kuu lakini wakati ule hapakuwa na makato ya mfuko wa kijamii.
Leave a comment