Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akizindua Sera Mpya wa Elimu na Ufundi

Sera mpya ya Elimu: Mashua za matumaini zapelekwa shuleni

MNAMO 13 Februari 2015, Rais Jakaya Kikwete alizindua sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014. Kwa kulinganisha sera ya zamani na sera mpya, tunaona kwamba sera mpya inayo maeneo kadhaa yenye mambo mapya kisera.

Kwa mfano, sera inaelekeza kufundishwa kwa baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafundishwi hapo kabla. Haya ni pamoja na elimu ya amani na utatuzi wa migogoro, elimu ya mazingira, na elimu ya stadi za kujikinga na VVU.

Je, elimu ya stadi za kujikinga na VVU ni kitu gani? Katika makala hii napenda kujibu swali hili katika mipaka ya sheria, kanuni na taratibu za elimu Tanzania.

Mwishoni nitapendekeza mambo machache ya kisheria ambayo lazima yawekwe sawa kama kinga dhidi ya walimu watakaotoa elimu hii.

Stadi za kujikinga na VVU ni sehemu ya elimu ya ujinsia wa binadamu. Hivyo basi, kwa kiasi fulani, sera mpya inapendekeza elimu ya ujinsia wa binadamu kufundishwa shuleni na vyuoni.

Kuhusu elimu hii, sera mpya inasema yafuatayo: “Elimu itolewayo shuleni na vyuoni haina budi kuzingatia umuhimu wa kumwelimisha mwanafunzi katika umri mdogo ili kumjengea tabia na mwenendo stahiki kuhusu kujikinga na maambukizi ya VVU na UKIMWI.”

Kwa hiyo, sera imeweka lengo la, “kutoa elimu kwa wanafunzi, walimu na jamii ili kupunguza kasi ya kuenea kwa maambukizi ya VVU na UKIMWI, pamoja na kutoa huduma na faraja kwa walioathirika.”

Kwa ajili ya kufikia lengo hili, sera imetamka kwamba: “Serikali itajumuisha stadi za kujikinga na VVU na UKIMWI katika mitaala ya elimu na mafunzo katika ngazi zote” (Tamko Na. 3.7.2).

Tangu mgonjwa wa kwanza wa UKIMWI alipogunduliwa Tanzania mwaka 1983, wataalam wametufundisha kwamba “stadi za kujikinga na VVU” zinahusu ufundi wa kupanda mashua tatu za matumaini.

Kwanza, kuna stadi za kupanda mashua ya “useja,” kwa maana ya stadi za kujitenga na mahusiano ya kimapenzi. Pili, kuna stadi za kupanda mashua ya “uaminifu,” kwa maana ya stadi za kuwa mwaminifu katika mahusiano ya kimapenzi. Na tatu, kuna stadi za kupanda mashua ya “ukondomizaji,” kwa maana ya stadi za kuendesha mahusiano ya kimapenzi yaliyo salama.

Sera mpya inazihusu ngazi zote za elimu kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu. Hivyo, elimu ya stadi hizi inawalenga watu ambao wako ndani ya ndoa na wale walio nje ya ndoa pia.

Uamuzi huu wa serikali ni wa kupongezwa. Ni muhimu sana vijana wetu wakapata elimu sahihi, kwa wakati sahihi na kwa njia sahihi. Hata hivyo, wigo wa sera mpya unatulazimisha kutafakari zaidi ya kinacho pendekezwa katika sera hii mpya.

Kwa mfano, hapa Tanzania, sheria ya ndoa, sheria ya mtoto, sheria ya kanuni ya adhabu na sheria ya makosa ya ujinsia zikisomwa pamoja mambo kadhaa yanaonekana kuhusiana na sera hii mpya ya elimu.

Kwa mujibu wa sheria hizi, mtoto ni mtu yeyote mwenye miaka chini ya 18; mtu mzima ni mtu yeyote mwenye miaka 18 au zaidi; mvulana mwenye umri chini ya miaka 18 haruhusiwi kuoa na msichana mwenye umri chini ya miaka 15 haruhusiwi kuolewa.

Pia, kwa mujibu wa sheria hizi, mvulana mwenye miaka chini ya 12 anahesabiwa kisheria kwamba hana uwezo kufanya ngono; msichana mwenye umri wa miaka 14 au zaidi anahesabiwa kisheria kwamba anao uwezo kuridhia tendo la ngono; na kufanya ngono na msichana aliye chini ya miaka 14, hata kama ameridhia mwenyewe, ni ubakaji kisheria.

Kadhalika, kwa mujibu wa sheria hizi, kusema maneno au kufanya ishara yenye kuudhi kijinsia mbele ya mwanamke ni unyanyasaji wa kijinsia.

Pia, mtu yeyote mwenye mamlaka mahali pa kazi, au mahali pengine kokote, akipendekeza mahusiano ya kimapenzi, ama kwa maneno au kwa vitendo, kwa mwanamke, na mwanamke huyo akakataa, basi huo ni unyanyasaji wa kijinsia.

Elimu ya kujikinga na VVU inahusisha kufundisha stadi za kupanda mashua ya “uaminifu” na “ukondomizaji.” Ni wazi kuwa “wahitimu” wa elimu hii watapenda kuweka katika vitendo nadharia waliyopewa darasani. Katika mazingira haya, ufahamu wa mipaka hii ya kisheria ni muhimu. Elimu kuhusu sheria hizi lazima itolewe.

Lakini liko jambo jingine ambalo lazima lifafanuliwe katika elimu ya kujikinga na VVU. Katika elimu hii maneno “mahusiano ya kimapenzi” yatatumika sana. Hata hivyo, maneno haya hayana fasili rasmi katika sheria zetu hapa Tanzania.

Kitabu kiitwacho Black’s Law Dictionary, kinataja maana mbili za maneno “mahusiano ya kimapenzi” au tusema “sexual relations.” Maana ya kwanza ni “Sexual intercourse.” Na maana ya pili ni hii: “Physical sexual activity that does not necessarily culminate in intercourse.

Sexual relations usually involve the touching of another’s breast, vagina, penis or anus. Both persons, the toucher and the person touched, engage in sexual relations.”

Kuhusu maana ya kwanza, yaani “kufanya ngono” au tusema “sexual intercourse” kama sio “carnal knowledge,” kitabu hiki cha Black’s Law Dictionary, kinasema yafuatayo: Coitus; copulation; the act of a man having sexual bodily connections with a woman; sexual intercourse… While penetration is an essential element, there is ‘carnal knowledge’ if there is the slightest penetration of the sexual organ of the female by the sexual organ of the male … It is not necessary that the vagina be entered or that the hymen be ruptured; the entering of the vulva or labia is sufficient.”

Kwa maoni yangu, sio watu wengi wanayaelewa haya. Hivyo, maarifa haya yote lazima yawe ni sehemu ya elimu inayokusudiwa na serikali. Vinginevyo, “wahitimu” wa elimu ya kujikinga na VVU wanaweza kujikuta wako kizimbani kujibu tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia au ubakazi. Hata walimu watakaotoa elimu hii wanaweza kujikuta katika matatizo hayo hayo.

Baada ya kusema hayo, nirudie kusisitza kuwa pendekezo la serikali kuhusu elimu ya kujikinga na VVU ni muhimu na limechelewa sana.

Makala hii imeandikwa na Deusdedit Jovin

About Mwandishi Wetu

Visit Us On FacebookVisit Us On TwitterVisit Us On Youtube