Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Sera kabambe ya wanawake, wenye umelavu na vijana yaandaliwa
Habari Mchanganyiko

Sera kabambe ya wanawake, wenye umelavu na vijana yaandaliwa

Spread the love

JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata) na Ushiriki Tanzania wanaandaa sera ya kitaifa ya ushiriki wa wanawake, wenye ulemavu na vijana kwenye siasa na uteuzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Sera hiyo ambayo itakapokamilika itawasilishwa serikalini, ina lengo la kuweka uwiano sawa wa makundi hayo kwenye nyanja za siasa ili kuwawezesha kugombea kwenye nafasi mbalimbali na kuteuliwa kushika nafasi kadhaa pasina kubaguliwa.

Akitoa mada kwa wahariri wa vyombo vya habari kuhusu sera hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Deus Kibamba alisema, wamepita kuzungumza na makundi mbalimbali ikiwemo Serikali ili kuandaa sera itakayokuwa na ufumbuzi wa tatizo lililopo sasa.

Alisema, tatizo la kukosekana kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu katika harakati za kisiasa ni kubwa ukilinganisha na wanaume.

Kibamba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jukata alisema “wanawake wanatamani kugombea wenyewe katika majimbo, lakini wametuambia wenyewe kwamba wanaambiwa subirini, wanapigwa pini, wanaaambiwa ninyi mna viti maalum jambo ambalo ni kuwabagua.”

Baadhi ya wahariri wakifuatilia mada

Alisema, walipofika visiwani Zanzibar kuzungumza na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), walibaini tayari wana sera kama hiyo lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hawana.

“Haitoshi kama ZEC ina sera na NEC haina, inahitajika sera ya kitaifa itakayotumika na wote,” alisema Kibamba

Alisema Katiba Ibara ya 13 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazuia ubaguzi wa aina yoyote, lakini hili limekuwa likiendelea ndani ya vyama vya siasa kutotoa kipaumbele kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Kibamba alisema, watu wenye ulemavu walipozungumza nao, wamekuwa wakishuhudia nafasi walizokuwa nazo mathalani za kisiasa kama wabunge, pindi wanapopoteza sifa za ubunge, anayeteuliwa baadaye anakuwa si kutoka kundi lao.

Safu ya juu ya Uongozi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)

“Kama mmetoa nafasi ya kundi la wenye ulemavu kushika nafasi fulani, inapotokea mmoja amepoteza sifa, mbadala wake inabidi awe kundi la watu wale wale lakini hili kwa wenye ulemavu limekuwa halifanyiki,” alisema Kibamba

Kuhusu ushiriki wa vijana, Kibamba alisema “wamebaini k viko vyama ambavyo vimeteua vijana lakini kwenye uamuzi wapo tu, wameingia kujaza nafasi. Sera hii inakwenda kuweka usawa na kumaliza tatizo hili.”

“Hatujaelewa kwa nini NEC na ZEC wakipokea majina kutoka CCM, Chadema, ACT isiombe na kuona kama hayo majina yamefikia asilimia 30.”

“Ikikuta hakuna asilimia 30 ya vijana, wanawake au wenye ulemavu inawarudisha hili halifanyiki. Lakini hata ukiangalia viongozi wa juu wa vyama hivi na vingine, wote wanaume, msajili wa vyama anapaswa kulisimamia hili ili kuwa na uwiano sawa,” alisema Kibamba.

Safu mpya ya Uongozi wa Chadema

Akihitimisha mada ya uchambuzi wa sera hiyo, Kibamba alibainisha mapendekezo nane yatakayopaswa kuzingatiwa ikiwemo, vyama vya siasa vina wajibu wa kuteua wanawake, vijana na wenye ulemavu kama wagombea katika nafasi za majimbo ambayo kwa sasa ni 264.

“Kumekuwa na shida, wagombea vijana, wanawake na wenye ulemavu wakiteuliwa wanaachwa kama yatima. Sera inasema, vyama vya siasa kwa sababu vinapokea ruzuku ya kuendesha kampeni, vina wajibu wa kuwawezesha,” alisema

Kibamba alisema, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, wana wajibu wa kuandaa taratibu ya kulazimisha vyama vya siasa kuendana na kuheshimu matakwa ya Katiba Ibara ya 13 na zinginezo na sheria ya vyama vya siasa kama ilivyorekebishwa 2019.

Alisema, vyombo vya habari kutoa uwiano sawa katika kuripoti kwa watu wenye walemavu, vijana na wanawake na kuacha matusi, kejeli ya wagombea wanaotukana ili kudumisha amani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!