Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Samia awanyooshea kidole watendaji kero za muungano
Habari za Siasa

Samia awanyooshea kidole watendaji kero za muungano

Spread the love

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinachelewa kutatuliwa kutokana na uzembe wa watendaji wanaoshughulikia masuala ya muungano huo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mama Samia amesema hayo leo Jumamosi tarehe 17 Oktoba 2020 katika hafla ya ufutaji hoja tano za muungano zilizopatiwa ufumbuzi, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Makamu huyo wa Rais amesema, mara nyingi michakato ya utatuaji wa kero hizo hukamilika mapema, isipokuwa utekelezwaji wake hukwamishwa na watendaji.

“Wakati mwingine kuna mambo tunayazungumza, tunayamaliza lakini tunapokwenda kwenye utendaji, bado watendaji wanasimama kabla ya kero kutatuliwa, watu wanalaumu muungano kumbe ubovu wa utendaji wa watendaji wetu,” amesema Mama Samia.

Mama Samia amekemea baadhi ya wanasiasa wenye dhana potofu ya kwamba changamoto za muungano huo zitatatuliwa ukivunjwa, akisema kwamba uwezo wa kutatua changamoto hizo ndani ya muungano upo.

“Hakuna shaka ndani ya muungano changamoto zipo na zitakuwepo ila tuliowengi, hatuamini kuvunja muungano ndio njia sahihi ya kuondokana changamoto zilizopo, hatuamini hivyo kwa kuwa tuna uwezo wa kutatua changamoto hizo na zitakaoibuka kwani amani, maendeleo na ustawi wa Taifa uko katika muungano huo,” amesema Mama Samia.

Hoja tano zilizofutwa leo ni, ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika masuala ya kimataifa na kikanda. Ushirikishwaji wa SMZ katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na gharama ya kushusha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam inayotoka Zanzibar.

Nyingine ni, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi na utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja na Serikali ya Muungano wa Tanzania na SMZ.

Kuhusu ufutwaji wa hoja hizo, Mama Samia amewaagiza mamlaka husika kuanza mara moja utekelezwaji wa hatua hiyo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya Watanzania.

“Kwa hiyo ni vema tunapomaliza kuzisaini na kutoa kwamba sio kero za muungano, kuweka mkazo kusimamia katika ngazi ya utendaji ili mambo yanyooke, ni imani yangu kusainiwa hati hii ni kutoa hamasa ya kutafuta ufumbuzi wa hoja zilizobaki kwa manufaa ya muungano wetu,” amesema Mama Samia.

Makamu huyo wa Rais wa Tanzania amesema, hatua hiyo itachochea Zanzibar kuwa na maamuzi katika kujadili masuala yake ya kimaendeleo katika nyanja za kimataifa na kikanda.

“Hatua hii itaipa fursa Zanzibar kujadili masuala yake ya kimaendeleo kimataifa na kikanda, nia ni kulinda na kudumisha muungano wetu,” amesema Mama Samia.

Mama Samia amesema, kuibuka kwa changamoto mpya katika muungano ni suala la kawaida, hivyo inatakiwa zipatiwe ufumbuzi wa haraka kila zinapojitokeza.

“Hapa naomba nitoe rai changamoto zilizotatuliwa na zitakazoendelea kutafutiwa ufumbuzi na zitakazojitokeza haimaanishi muungano wetu una tatizo bali kurekebishwa kwa kasoro na changamoto hizo. Kasoro zinapojitokeza haimaanishi muungano wetu si muhimu, ni muhimu kabisa,” amesema Mama Samia.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya ufutaji wa hoja hizo, amesema utaratibu wa pande zote mbili kukutana kila mara kujadili changamoto zinazojitokeza utasaidia kuimarisha muungano.

“Utaratibu huu wa kufanya mapitio ya maeneo yenye changamoto katika muungano wetu ni utaribu mzuri zaidi kuliko kuvunja muungano wetu,” amesema Waziri Majaliwa.

Majaliwa amesema, Serikali ya Tanzania itaendelea kubaini changamoto za muungano kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.

“Naahidi tutaendelea kuyabaini maeneo yenye changamoto, kuyapitia na kuweka utaratibu wa kuyamaliza ili muungano wetu uende sawa, tuendelee kuhamasisha uwepo wa muungano na si kuuvunja,” ameahidi Majaliwa.

Mjumbe wa Kamati ya pamoja ya kushughulikia masuala ya Muungano, Dk. Hussein Mwinyi amesema, Serikali zitakazoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Tanzania na Zanzibar baada ya chama hicho kushinda Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, zitakamilisha utatuzi wa changamoto zilizosalia.

“Leo nichukue fursa hii kuwaaga rasmi kwenye kamati hii (Kamati ya pamoja ya kushughulikia masuala ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar) najua baada ya uchaguzi huu sitakuwa tena mjumbe wa kamati hii,” amesema Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi ambaye ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM amesema “nataka niwahakiksihie Serikali zote mbili za awamu ijayo chini ya CCM zitakamalisha zile changamoto chache sana zilizobaki (za muungano) kama tulivyoeleza hapa.”

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Tanzania, Balozi John Kijazi amesema Serikali itaendelea na utatuzi wa changamoto zilizojitokeza.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Abdul Hamid Yahaya amesema, serikali zote mbili zimejitahidi kusaini hati nyingi za kufuta kero za muungano katika kipindi cha mwaka mmoja na kushauri nguvu iliyotumika ielekezwe hadi katika masuala yasiyokuwa ya muungano.

“Leo tunashuhudia matunda haya kusaini hati nyingi katika kipindi cha mwaka mmoja, ningependa kutoa wito hali hii tuiendeleze katika awamu inayokuja, tumebaini vikao hivi ni muhimu sana, hata katika hoja si za muungano ushirikiano ni muhimu,” amesema Yahaya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!