Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Sakata la Nape latikisa
Habari za SiasaTangulizi

Sakata la Nape latikisa

Spread the love

SAKATA la Nape Nnauye, aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kutishiwa kwa bastola na askari asiyevalia sare, limeibua mshituko kwa umma unaoshangaa inafanyikaje hiyo kwa mtu ambaye juzi tu alikuwa waziri katika serikali ya Rais John Magufuli, anaandika Hamisi Mguta.

Nape alitishiwa bastola jana na askari kanzu waliokuwa wakitaka arudi ndani ya gari alilowasili nalo Hoteli ya Protea, Oysterbay, Dar es Salaam, alipokwenda kukutana na waandishi wa habari. Aliitisha mkutano ili kueleza hisia zake baada ya kusikia Rais amemteua mtu mwingine kuwa Waziri wa Habari.

Katika nchi inayosifika na kutambulika kuwa ni ya kidemokrasia ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, Tanzania haijafikiriwa kutokea tukio kama hilo na kwa mtu aitwaye kiongozi serikalini? Kama Nape ambaye jana tu alikuwa Waziri, anatishiwa bastola, wananchi wa kawaida wasiokuwa na cheo chochote itakuaje?

Ni tukio lililomgusa kila raia mpenda haki na mzalendo nchini. Ndio maana limechukua nafasi kubwa katika masuala yanayojadiliwa katika mitandao ya kijamii na magazetini. Wanaojadili ni pamoja na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho Nape amekuwa kiongozi na amekipigania kwa kujitoa mhanga, kama alivyoeleza mwenyewe jana.

Nape, mbunge wa Mtama, mkoani Lindi, aliwaambia waandishi wa habari hana kinyongo kuondolewa uwaziri. “Hakuniita aliponiteua, sasa kama anateua Mtanzania mwingine , hakuwa na sababu ya kuniuliza… hii nchi ni huru, ya nini sasa vyombo kupaniki, watu wanapaniki… jambo la kawaida, vijana lazima waachwe na uzalendo wao na kuutetea ukweli ndani ya nchi yao,” alisema Nape.

Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) akizungumzia kitendo hicho, amesema kinatishia amani nchini hasa kinapowakuta viongozi.

Dk. Bisimba amezungumza hayo jana na waandishi wa habari dakika chache baada ya mazungumzo ya Nape na waandishi yaliyolazimika kufanywa viwanja vya hoteli badala ya ukumbini kutokana na amri ya jeshi la polisi kuzuia mkutano huo.

“Kwanza ni tukio la kutisha na linapaswa kukemewa kwasababu kwa nchi yetu tunayojivuna ni ya kidemokrasia na amani, Nape alikuwa waziri mpaka leo asuhubi (jana) halafu ghafla unaona anatishiwa bastola.”

Amesema mkutano alioufanya Nape ulikuwa ni kawaida kama alivyoitisha mkutano wakati anapokea ripoti ya uchunguzi kutoka kwa kamati aliyounda dhidi ya sakata la mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, hivyo hakukuwa na sababu ya vitisho kama alivyofanyiwa na mamlaka iliyofanya hivyo imewakosea Watanzania.

“Nimepata simu ya mwananchi hata simjui amekasirika ananiambia kwanini Watanzania tusitoke nje tufanye kitu, sasa hapo utaweza kusema ni uchochezi lakini uchochezi unafanywa na mamlaka kwasababu itafanya Watanzania ambao hawakuwa na hasira walipuke kwa hasira itakuwa mbaya sana,” amesema.

“Kwani huyu mtu ana nini kinachomfanya alindwe hivyo, maana yake hata kama kuna watu watakufa ilimradi alindwe tu, hii ni hatari kwa nchi,” amesema bila kutaja jina la mtu huyo.

Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani, na mbunge wa Iramba Magharibi, ameandika kupitia ukurasa wake wa Facebook na Twitter, kuwa amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu kumtafuta na kumwajibisha aliyemtishia Nape.

“Mh, Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni Mtanzania, mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana record ya uhalifu. Kitendo cha mtu kumtolea bastola, sio cha kiaskari… Nahusika na usalama wa raia wote namuelekeza IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyenuia kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya kiaskari,” amesema.

Deus Kibamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKWATA), anayeandika makala magazetini za uchambuzi wa masuala ya utawala bora, amesema kupitia mahojiano ya moja kwa moja na televisheni ya Azam Two kwamba ameshangaa kuona tukio la Nape kutishiwa bastola hadharani.

“Nilishangaa kuona risasi ambayo ilitakiwa itumike katika mazingira muhimu sana inatumika kumrudisha mtu kwenye gari, kwa hiyo ile ripoti ya Umoja wa Mataifa inayosema Watanzania furaha yetu ipo chini naanza kuiona,” amesema.

Kuhusu kuporomoka kwa chama baada ya tukio hilo, la kada mkubwa wa chama hicho Kibamba ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania amesema, Chama cha mapinduzi kina mbinu nyingi sana za kutenda kazi kati kati ya uchaguzi na uchaguzi, harafu kuja kuleta ulaini hivi na sukari na supu kwa wanachama wakati uchaguzi unakaribia.

“Lakini kwa wakati huu kuna mteteleko ambao umeshatokea nafikiri wanahitaji kufikiria bila kusubiri uchaguzi,”amesema.

Akihutubia hafla ya kuapishwa mawaziri aliowateua, Rais Magufuli amesema leo kuwa kitendo cha magazeti kuonesha tukio lililofanywa na mtu mmoja kama vile limefanywa na serikali yote, si jambo jema.

“Nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari ‘be careful’ kama mnafikiri mna uhuru wa namna hiyo ‘not to that extent’ (sio kwa kiwango hicho),’ amesema.

Wakati huohuo rais Magufuli amesihi vyombo vya habari kuitanguliza Tanzania kwenye taarifa zao wakati huo kukiwa na sintofahamu ya kuminywa kwa uhuru wa habari kwa kumuondoa aliyekuwa waziri wa wizara husika aliyeonesha kuipigania tasnia.

Nape ameondolewa uwaziri siku moja tu baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tukio la uvamizi kwenye kituo cha habari cha Clouds Media Group, ikithibitisha kuwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesimamia uvamizi huo usiku wa saa 5 Ijumaa ya 17 Machi.

Imeelezwa kuwa alifanya uvamizi huo akitumia askari wenye silaha. Hata hivyo, ilielezwa kuwa kilichomsukuma kwenye kashfa hiyo ni suala lenye maslahi binafsi kwake.

Nape aliahidi kuwa ataifikisha ripoti hiyo kwa mamlaka za juu yake akitaja Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais Magufuli. Haijajulikana mpaka sasa kama ripoti hiyo aliwahi kumkabidhi rais. Nape ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Idara ya Uenezi ya CCM, amesema atapata nafasi nzuri ya kutumikia wananchi wa jimboni kwake.

Nafasi yake ameteuliwa Dk. Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye badala yake, Rais Magufuli amemteua Prof. Palamagamba Kabudi kuziba nafasi yake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!