Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi SAKATA LA MADED KUSIMAMIA UCHAGUZI: Mahakama ya Rufaa yajiweka mtegoni
Makala & Uchambuzi

SAKATA LA MADED KUSIMAMIA UCHAGUZI: Mahakama ya Rufaa yajiweka mtegoni

Mahakama ya Rufaa Tanzania
Spread the love

JUZI Jummane, tarehe 30 Julai 2019, Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano, ilisikiliza rufaa iliyokatwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake wawili, kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu, kuwazuia wakurugenzi wa halmashauri, majiji na manispaa kusimamia uchaguzi.

Shauri hilo la Kikatiba limesikilizwa na jopo la majaji watano, wakiongozwa na Jaji Augustino Mwarija. Wengine, ni Jaji Stella Eshete Mugasha, Richard Mziray, Rehema Mkuye na Jacob Mwambegele.

Katika kesi ya msingi, Bob Chacha Wangwe, aliwasilisha maombi mahakamani, kupinga wakurugenzi wa halmashauri (DED), kusimamia uchaguzi kwa kuwa ni watu ambao wanateuliwa na rais ambaye ni mwenyekiti wa chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi huo; na au yeye mwenyewe kuwa mgombea katika uchaguzi huo.

Ikumbukwe kuwa Machi mwaka jana, Bunge la Jamhuri lilikataa kujadili hoja binafsi ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, iliyotaka Bunge kupitia Azimio la kuitaka Serikali kuleta bungeni Muswada wa kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ya taifa.

Kubenea aliwasilisha hoja hiyo, chini ya Kanuni ya 54 (1) (2)na (3)] ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januri, 2016. Kwa faida ya wasomaji wetu; na kwa maslahi mapana ya taifa, tumeamua kuchapisha hapa hoja hiyo neno kwa neno.

______________________

A: MAELEZO YA HOJA

Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali utawala wa sheria, kujali na kutetea haki za binadamu ambayo ni miongoni mwa misingi mikuu ya demokrasia, sifa nyingine kuu ya demokrasia duniani ni chaguzi huru na za haki. Chaguzi huru na za haki ndizo zinazodhihirisha mamlaka ya wananchi katika kuamua namna wanavyotaka utawala wa nchi yao uwe. Kwa maneno mengine, chaguzi huru na za haki ndizo kitambulisho halisi cha demokrasia ya kweli.

Mheshimiwa Spika, mamlaka yoyote inayopataikana kwa njia nyingine bila kupitia chaguzi huru na za haki; mamlaka hiyo haiwezi kuwa ya kidemokrasia. Kwa vyovyote vile, mamlaka hiyo itakuwa ni ya ki-imla yenye kujali na kusimamia maslahi ya wachache na sio maslahi ya wananchi au maslahi ya taifa.

Mheshimiwa Spika, ili chaguzi ziweze kufikia malengo yaliyokusudiwa – ya kuweka uongozi au mamlaka halali inayokubalika na wananchi walio wengi – ni lazima chaguzi hizo ziratibiwe na chombo kinachoaminika na pande zote zinazoshiriki katika chaguzi hizo; chombo ambacho ni huru kisichoegemea upande wowote ili  kujenga muafaka wa kitaifa na mustakabali mwema wa nchi. Chombo hicho si kingine bali ni Tume Huru ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1991aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi aliunda  Tume ya kuangalia mfumo bora wa siasa nchini iliyoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Francis Nyalali. Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na taarifa ya Tume ya Jaji Nyalali iliyopendekeza kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ilipendekeza pia kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Taarifa hiyo, ilitoa mifano ya nchi nyingi ambazo Tume zao za uchaguzi sio huru na jinsi ambavyo kukosekana kwa uhuru wa tume hizo kulivyosababisha madhara makubwa ya mauaji, machafuko na kudidimia kwa ustawi wa nchi hizo.  Taarifa hiyo ilieleza pia kwamba; Watu wakijua kuwa chaguzi zinazofanywa nchini mwao ni za kughushi/bandia basi lazima kutatokea fujo ambayo haijulikani itaishia wapi.

Mheshimiwa Spika, ili kuepukana na madhila yanayotokana na chaguzi zisizo huru na haki; Tume ya Jaji Nyalali ilisisitiza katika taarifa yake (Ibara ya 591), kwamba ni lazima Muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ubadilike ili kukidhi haja ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Aidha, Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kuzifanyia mabadiliko makubwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar. Mengi ya mapendekezo ya Tume hii hayakukubaliwa na Seriakali isipokuwa pendekezo kuu la kuachana na mfumo wa utawala wa chama kimoja cha siasa kwenda kwenye mfumo wa vyama vingi.  Hiki ni kiini macho tu kwani uwezi kuwa katika mfumo wa siasa za vyama vingi wakati Tume ya Uchaguzi ipo kwa muktadha wa chama kimoja.

Mheshimiwa Spika, kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapo Julai, 1992 kulifanyika bila mabadiliko makubwa ya Katiba. Haya yalikuwa ni mabadiliko ya Nane ya Katiba yaliyofuta rasmi mfumo wa siasa wa chama kimoja cha siasa.

Hata hivyo, Katiba ile ile ya Chama Kimoja ililazimishwa kwa kuwekewa “viraka” na “mapengo” kuubeba mfumo mpya wa siasa. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Tanzania kuingia katika mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992.

Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania

Mheshimiwa Spika, kutokana na ushauri wa Tume ya Nyalali, Sura ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ilirekebishwa na kuifanya Tanzania kuwa nchi inayofuata mfumo wa Vyama vingi vya Siasa. Sheria ya Vyama vya  Siasa, (Na. 5 ya mwaka 1992), ilirekebishwa ili kuwezesha kuandikishwa kwa vyama vya siasa. Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Na.1 ya mwaka 1985), Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa,(Na. 4 ya  mwaka 1979) na sheria zinazoendana pia zilirekebishwa ili kuondokana na matakwa ya chama kimoja na kuruhusu mchakato wa kufanyika kwa Uchaguzi chini ya Mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1993 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilianzishwa chini ya Ibara ya 74 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Wajumbe wa Tume waliteuliwa kwa mara ya kwanza tarehe 14 Januari 1993.

Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba;

“Kutakuwa na Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na wajumbe wafuatao watakaoteuliwa na Rais:-

(a) Jaji wa Mahakama Kuu au Jaji wa Mahakama ya Rufani, ambaye atakuwa mwenyekiti;

(b) Makamu Mwenyekiti ambaye atakuwa mtu anayeshika, aliyewahi kushika au anayestahili kuteuliwa kushika madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu au Jaji wa Mahakama ya Rufani;

(c) Wajumbe wengine watakaotajwa na sheria iliyotungwa na Bunge.

(2) Rais atamteua Makamu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwa kufuata kanuni kwamba endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka sehemu moja ya Muungano, Makamu wake atakuwa ni mtu anayetoka sehemu ya pili ya Muungano.”

Mheshimiwa Spika, Aidha, Kwa mujibu wa Ibara ya 74(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Na. 1 ya mwaka 1985 na kufanyiwa marejeo mwaka 2010), Mkurugenzi wa Uchaguzi ndiye Katibu wa Tume ambaye pia huteuliwa na Rais.

Tukumbuke kwamba sheria hii ya uchaguzi ni ya mwaka 1985, wakati huo Tanzania ilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa na hivyo sheria hii ilikuwa mwafaka kwa mfumo wa chama kimoja cha siasa, na kwa mfumo wa sasa kifungu hiki kinatakiwa kibadilishwe ili kutoa uhuru kwa mtendaji huyo.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Ibara hiyo ya 74 (7) ya Katiba na sheria ya Taifa ya uchaguzi ni dhahiri kwamba Tume ya Uchaguzi iliyopo sasa, haiwezi kuwa huru kwani viongozi wake wakuu ni wateule wa Rais, kwa maana hiyo hata utendaji kazi wake unategemea matakwa ya mamlaka yao ya uteuzi.

Kwa mfano, hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuamua binafsi kufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015, Visiwani na matokeo yake, hasa baada ya mgombea wa upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad, kuonekana kushinda kwenye uchaguzi huo, ni ushahidi mwingine kuwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi, vinaingiliwa na walioko madarakani na hivyo haviko huru.

Bwana Jecha alidai katika taarifa yake kwa umma kuwa uamuzi wake wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake, umetokana na kuwapo kwa dosari kadhaa ambazo zilijitokeza katika zoezi zima la upigaji kura na uhesabuji wa matokeo.

Mheshimiwa Spika, Kitendo cha Jecha kufuta uchaguzi Visiwani Zanzibar, kilishangaza mataifa mengi ulimwenguni, ikiwamo Marekani. Hii ilitokana na ukweli kuwa wakati yeye akitangaza kufuta uchaguzi huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano, iliyatambua matokeo ya uchaguzi wa wabunge na Rais ambao ulifanyika kwenye vituo vilevile na uliosimamiwa na watu walewale.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba madhaifu haya ya Katiba kuhusu tume ya Uchaguzi yanajulikana hata kwa viongozi wake wakuu. Gazeti la Mwananchi la Tarehe 27 Desemba 2013 lilichapisha taarifa chini ya kichwa cha habari: “KUUNDWA KWA TUME HURU YA UCHAGUZI KUNASUBIRI KUWEPO NA MACHAFUKO?

Sehemu ya taarifa hiyo ilisomeka hivi:-“…..Ndiyo maana siyo wananchi wengi walioshangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa TUME hiyo Jaji Damian Lubuva alipokiri miezi michache iliyopita wakati akitoa maoni ya TUME yake mbele ya TUME ya Mabadiliko ya Katiba, kwamba TUME YAKE sio Huru. Alishauri kwamba katika mchakato wa kupata Katiba mpya iundwe TUME HURU YA UCHAGUZI ili chombo hicho kipate mwafaka wa kitaifa ili kiweze kusimamia mchakato mzima kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chini ya Katiba Mpya.”

Mheshimiwa Spika, ushuhuda mwingine kwamba TUME YA UCHAGUZI sio HURU ni pale Vyama vyenye wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chombo chao cha Tanzania Center for Democracy (TCD), walipofikia Makubaliano na Mheshimiwa  Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa awamu ya nne  katika kikao kilichofanyika tarehe 8 Septemba 2014, Ikulu ndogo ya Dodoma, pamoja na mambo mengine, kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya  Mwaka  1977 ifanyiwe marekebisho muhimu ili kuwa na TUME HURU YA UCHAGUZI.

Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa na Tume ya mabadiliko ya Katiba, ambao iliundwa kwa kiasi kikubwa na watumishi waandamizi wa taasisi za  serikali,  ulibaini kwamba mfumo wa uchaguzi ulipo sasa pamoja na vyombo vya uchaguzi vinapingwa au havikubaliki kwa wadau wakuu na muhimu wa uchaguzi kwani kuna kutokuaminiana kwa hali ya juu kuhusu sheria na mfumo mzima wa kitaasisi kwa taasisi zinazosimamia uchaguzi nchini Tanzania[1].

Utafiti huo umebainisha kwamba uendeshaji wa mifumo ya kiuchaguzi yenye tija inahitaji taasisi endelevu zenye uwakilishi wa kutosha, zenye kutenda haki, na zenye kujitegemea kimamlaka na kimaamuzi. “Effective management of electoral systems requires institutions that are inclusive, sustainable, just and independent.”

Mheshimiwa Spika, Katika mfumo ambao Tume za Uchaguzi zinawajibika moja kwa moja kwa mamlaka za uteuzi, ni nadra sana kwa tume hizo kuwa huru, kwa maana nyingine ni kwamba maana halisi ya demokrasia itakuwa ni ndoto.  Where democratic institutions are weak, elections are easily used by violent and dictatorial political groups to manipulate the will of the people and seize control of the government.”

Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo wangu na maandiko ya wanazuoni mbalimbali yanaonesha kwamba mataifa mengi ambayo viongozi wake au vyama vinavyojitanabaisha kuwa vyama vya ukombozi ving’ang’anizi wa utawala wanatumia mbinu ya kutumia mabilioni ya shilingi ya walipa kodi kwa ajili ya uchaguzi wakati huohuo wanatumia vyombo vya dola kupanga matokeo wanayoyataka.

Katika mfumo wa kidikteta mara zote uchaguzi hutumika kama kiinimacho tu cha kuridhisha wadau wa maendeleo, lakini ukweli ni kwamba matokeo mara zote hupangwa kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika. Uchakachuaji wa matokeo ili kuhalalisha ushindi ni njia za kawaida kwa viongozi ving’ang’anizi wa madaraka, na kama wakiona jamii haikuridhika na matokeo, wanachokifanya ni kuzidisha ulinzi kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Spika, mifano mizuri ni uchaguzi wa Urais wa mataifa ya Chile mwaka 1988, Poland mwaka 1989, Serbia mwaka 2000, Ukraine mwaka 2004, Belarus mwaka 2006[2]. Kwa upande wa mataifa ya Kiafrika, hatuwezi kuiacha Burundi, Zimbabwe, Uganda na Tanzania kwa chaguzi zilizofanyika miaka ya hivi karibuni.  Haya yote yanafanyika kutokana na udhaifu wa Tume zetu za uchaguzi na mfumo mzima wa kisiasa unaokuwa chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 74(14) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kwamba;

“Itakuwa ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kwamba kila mmoja wao atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika Ibara ya 5 ya katiba hii.”

Aidha Ibara ya 74 (15) inasema kwamba;

kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (14) watu wanaohusika na uchaguzi ni;- (e) Wasimamizi wote wa Uchaguzi katika miji na wilaya zote.”

Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa, ambapo wakurugenzi walioteuliwa na Mhe Rais ni makada walioshindwa katika kura za maoni ndani ya CCM na wengine ni wale walioshindwa kwenye uchaguzi kupitia CCM; kuwapa dhamana watu hao ambao ni wanachama wa  CCM kusimamia uchaguzi, kunakwenda kinyume kabisa na matakwa ya ibara ya 74(14) inayopiga marufuku wasimamizi wa uchaguzi kuwa wanachama wa chama cha siasa.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira kama hayo, tume ya uchaguzi haiwezi kujidai kwamba iko huru kwa kuwa maafisa wake wana mafungamano na chama cha siasa – CCM. Kwa mfano kisa cha Jaji Augustine Ramadhani, Jaji George Liundi waliokuwa viongozi wakuu wa Tume ya Uchaguzi, baada ya kuondoka katika Tume ya Uchaguzi (NEC) walijitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM kinatoa picha ya wazi kwamba hawa wote wakati wakiwa watumishi/wasiamamizi wakuu wa Tume walikuwa ni wanachama wa CCM. Hatua ya Jaji Ramadhani kujiingiza kwenye siasa, mara baada ya kustaafu kupitia chama kilichoko Ikulu, ni ushahidi tosha kuwa NEC na ZEC siyo vyombo huru na hivyo haviwezi kutenda haki katika chaguzi; lakini mbaya zaidi vinatenda kazi kinyume na Katiba.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 ambayo  ilifanyiwa marekebisho mwaka 2010, kwenye kifungu cha 7(1) kinasema  kuwa “kwa madhumuni ya uchaguzi utakaofanyika chini ya usimamizi wa sheria hii, wasimamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi wa Jiji, wakurugenzi wa Manispaa, Wakurugenzi wa Miji na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya.

Kifungu cha 7(2) kinasema kuwa, “Na Tume yenyewe pia inaweza kuteua idadi ya maafisa wengine kuwa wasimamizi wa uchaguzi au wasaidizi wa usimamizi wa uchaguzi.”

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa sheria hiyo ya uchaguzi, wasimamizi wa Uchaguzi katika Wilaya au Majimbo ni wakurugenzi watendaji wa Halmashauri, Miji na Majiji na katika ngazi za Kata wasimamizi wa uchaguzi ni Watendaji wa Kata na watendaji hawa wote ni watumishi wa Serikali na hivyo ni wateule wa Rais au Waziri Mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambao kwa sasa Rais ndiye mwenye dhamana na Serikali za mitaa, hivyo wakurugenzi wote na watendaji wa kata wako chini yake.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Katiba na sheria ya uchaguzi ni kwamba wajumbe wote wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Mtendaji wake Mkuu na Maafisa wengine wote wa Tume hiyo huteuliwa na Rais wa nchi na hakika wote ni waajiriwa wa Serikali ya Chama Tawala. Kwa mantiki hiyo Rais anaweza kumuondoa katika madaraka mjumbe yeyote wa Tume ya Uchaguzi akipenda kufanya hivyo wakati wowote. Na tukumbuke kwamba Katika mchakato wa Uchaguzi Rais naye anakuwa na maslahi kwa kuwa naye ni mgombea mtarajiwa.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuliona hili la mapungufu ya Tume ya Uchaguzi yanayosababisha uchaguzi kutokuwa huru na Haki, Tume ya Jaji Nyalali kwenye taarifa yake, katika Ibara ya 592 ilisema kwamba, “Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi sharti wachaguliwe na Bunge au Baraza la Wawakilishi…. Wakurugenzi wa uchaguzi ambao watakuwa ni Makatibu wa Tume ya Uchaguzi nao sharti wachaguliwe na Bunge au Baraza la Wawakilishi baada ya kupendekezwa na Tume za Ajira zinazohusika.”

Mheshimiwa Spika, sambamba na msisitizo huo wa Tume ya Jaji Nyalali, Mwaka 1999 iliundwa kamati nyingine ya kuratibu maoni kuhusu Katiba iliyoongozwa na Mheshimiwa Jaji Robert Kisanga. Nayo Tume ya Jaji Kisanga ilisema yafuatayo:

“Muundo wa Tume ya Uchaguzi hauzingatii uwakilishi wa vyama vya siasa na kwamba wajumbe wa Tume huteuliwa na Rais ambaye pia anaweza kuwa ni kiongozi wa chama cha siasa kinachotawala. Kwa sababu hiyo, wajumbe wa Tume katika utendaji kazi wao ama watakuwa na upendeleo kwa chama husika au watakuwa wanalipa fadhila kwake. Wanaotoa hoja hii wanapendekeza kwamba kuwe na ama uwakilishi wa vyama vya siasa, ama kuwe na chombo kitakachochuja majina ya wajumbe wa Tume kabla Rais hajawateua”.

Mheshimiwa Spika, Rasimu ya Pili ya Katiba pamoja na Katiba Pendekezwa kwenye ibara za 190 na 211 kwa mfuatano huo, zinaongelea kuhusu kuundwa kwa Tume huru ya Uchaguzi, na jinsi tume hiyo itakavyopatikana. Huo ni ushahidi mwingine kwamba Tume ya uchaguzi iliyopo ina mapungufu makubwa na inaweza kuwa ndio chanzo cha kuliangamiza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ni chombo cha kufanya maamuzi. Vyombo hivi, kama ilivyo mahakama, huundwa kwa namna ambayo huaminiwa na wadau kuwa viko huru na haviwezi kuwa na upendeleo. Kwa hivyo kigezo cha kwanza na cha msingi ni namna gani UTEUZI wao unafanyika. Mchakato wa uteuzi unatakiwa uwe huru na wa haki, wa wazi na ulio shirikishi.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani Mwenyekiti na Mtendaji wake Mkuu kuteuliwa kisirisiri na mtu mmoja tu na  ambaye naye ni mgombea mtarajiwa, na chama chake kina wagombea kwa chaguzi ngazi zote, halafu  tume ikatangaza kuwa yenyewe ni tume huru na kwamba haiingiliwi na mamlaka yoyote.

Mheshimiwa Spika, Kigezo kingine cha Tume Huru ni uhuru wa rasilimali fedha iliyonayo Tume husika. Tume ambayo kila mara inaomba fedha za kutekeleza majukumu yake kwa mamlaka ambayo Tume inatakiwa iisimamie katika mchakato wa uchaguzi, ni dhahiri jambo hilo linaondoa uhuru wa Tume.

Mheshimiwa Spika, Tume huru ni lazima iwe na Mfuko wake wa Fedha ili iweze kuwa uhuru wa kifedha (financial independence) na kwamba haipigi magoti kwa yoyote kuomba fedha. Hiki nacho nikigezo muhimu cha uhuru wa Tume. Kinyume na hapo uhuru wa Tume unakuwa umewekwa rehani na hivyo haki kwa vyama shindani haiwezi kutendeka. Aidha, nimuhimu kwamba Tume ya Uchaguzi ikawa na wafanyakazi wake yenyewe wa kutosha na ikawa wanawajibika kwa Tume na wala sio Mamlaka nyingine, kusimamia shughuli za uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, kwa ushahidi ulioneshwa hapo awali ni kwamba kuna umuhimu mkubwa hasa katika mfumo huu wa vyama vingi vya siasa kuwa na Tume huru ya uchaguzi ili kuziba uwezekano wowote ambao unaweza kuitumbukiza nchi yetu katika machafuko yatokanayo na chaguzi.

 

Mheshimiwa Spika,  kwa mujibu wa Taarifa ya awali kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Tanzania oktoba 2015, iliyotolewa na timu ya uangalizi wa uchaguzi ya TEMCO pamoja na ushauri mwingine ilisema kwamba;

 

“…. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kusimamia chaguzi za Jamhuri ya Muungano. Wajumbe wa tume huteuliwa na rais wa Jamhuri ya Muungano na wanatekeleza majukumu yao kama inavyoelekezwa katika sheria za uchaguzi. Baadhi ya wadau wa uchaguzi hawaridhishwi na sheria zinazotawala chaguzi Tanzania. Kuna hisia na mashaka kuwa sheria ina upungufu, mkubwa zaidi ikiwa:

  1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina mamlaka ya kutosha ya kutekeleza majukumu yake bila upendeleo. Mashaka haya yanatokana na ukweli kuwa Mwenyekiti wa Tume, makamu wake, makamishna, na mkurugenzi wa uchaguzi huteuliwa na rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha siasa na wakati mwingine mgombea katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano;
  2. Tume haina wafanyakazi na maafisa wake mahsusi ukiacha wale walioko makao makuu Dar es Salaam. Inategemea kiasi kikubwa wafanyakazi wa serikali ambao huwepo kwa ridhaa ya rais. Utii wa wafanyakazi hawa uko kwa mwajiri wao na sio Tume” 

Mheshimiwa Spika, Kwa maelezo hayo yanayoonesha udhaifu wa Tume ya Uchaguzi jinsi inavyokosa uhuru katika utendaji wake wa kazi, ni wazi kuwa kuna umuhimu mkubwa hasa katika mfumo huu wa vyama vingi vya siasa, taifa letu linalosifika kwa amani na utulivu kuwa na Tume huru ya uchaguzi, ili kuliepusha  kuingia kwenye machafuko yanayoweza kuepukika. 

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo
  1. HOJA YENYEWE

KWA KUWA, Ibara ya (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 1992 inaitaja Tanzania kuwa ni nchi ya kidemokrasia, na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa;

NA KWA KUWA, mfumo wa vyama vingi vya siasa sio tu kusajili vyama bali unaendana na kujenga mazingira sawa ya ushindani – na hasa chaguzi zilizo huru na haki;

NA KWA KUWA, chaguzi huru na za haki zinategemea sana umadhubuti na uhuru wa Tume za Uchaguzi zinazosimamia chaguzi hizo;

NA KWA KUWA, chombo kinachotakiwa kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi kinatakiwa kiwe kinaaminika na wananchi pamoja na vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki chaguzi mbalimbali zinazosimamiwa na TUME YA UCHAGUZI;

NA KWA KUWA, historia inaonyesha kwamba pale ambapo haki hakikutendeka katika chaguzi katika nchi mbalimbali duniani; nchi hizo zilikumbwa na machafuko ya kisiasa jambo lililosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na hivyo kuleta  madhara makubwa katika nchi hizo;

NA KWA KUWA, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania inaonekana kushindwa kutenda haki katika chaguzi ilizosimamia kutokana na Tume hiyo kukosa uhuru wa kimamlaka na kifedha[3]

NA KWA KUWA, matukio ya  uhalifu wa kiuchaguzi (election fraud) hapa nchini yanazidi kuongezeka – ambapo imeshuhudiwa mgombea fulani anashinda uchaguzi lakini anatangazwa aliyeshindwa; au matokeo ya uchaguzi kutangazwa wakati bado kura zinahesabiwa; mambo ambayo yanajenga hasira na uhasama baina ya wananchi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi;

NA KWA KUWA, Ibara ya 74 (12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kwamba:“Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka  ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii;

NA KWA KUWA, Tume ya Uchaguzi inaongozwa na watu ambao wanaweza kufanya makosa ya kukusudia yatakayoweza kuingiza nchi katika mgogoro wa kisiasa, itakayoweza kuondoa utulivu na amani ya taifa na watu hao wasishitakiwe katika mahakama yoyote hapa nchini.

NA KWA KUWA, amani na utulivu wa nchi yetu vipo katika hatari ya kusambaratika kutokana uhalifu wa kiuchaguzi kuendelea kufanyika chini ya usimamizi wa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo sasa – rejea hali ya kisiasa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na madonda ya chaguzi za marudio za udiwani na Ubunge Tanzania Bara – Taifa limegawanyika!!

NA KWA KUWA, Udhaifu wa TUME YA UCHAGUZI au kutokuwa HURU kwa TUME mzizi wake umetokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 74(1) inayompatia Rais mamlaka ya kuteua Mwenyekiti wake, Makamu wake pamoja na wajumbe. Aidha sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 na marejeo yake ya mwaka 2010 kifungu cha 6(1) kinachompata Rais mamlaka ya kuteua Katibu Mtendaji wa Tume na kifungu cha 7(1) kinachowapa wateule wa Rais kuwa wasimamizi wa chaguzi kwenye maeneo yao ya kiutendaji.

NA KWA KUWA, Wateule hao wa Rais ndio wenye jukumu kisheria la kumtangaza mshindi wa uchaguzi, iwe amepata kura kidogo au nyingi,

NA KWA KUWA, Utaratibu huu unaotolewa na Katiba yetu pamoja na sheria ni kinyume cha Tamko la Dunia kuhusu Haki za Binadamu la mwaka 1948,

HIVYO BASI, kutokana na madhaifu hayo, ninaomba Bunge lako tukufu lijadili na kutoa maazimio;

NA HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba;

  1. Serikali ilete Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ili:-
  2. Kuruhusu kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoitwa, “Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
  3. Kuanzisha Mfuko wa Fedha wa Tume Huru ya Uchaguzi (Tanzania Independent Electoral Commission Fund).
  4. Serikali ilete Bungeni Muswada wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi itakayoweka Muundo, Utaratibu wa Upatikanaji wa Wajumbe; Mamlaka ya Tume, Mipaka ya kazi na utaratibu mzima wa kuendesha chaguzi. 

Mheshimiwa Spika,

Baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.

Saed Ahmed Kubenea

MBUNGE WA UBUNGO

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu

Spread the loveGEORGE Francis anasikitika; anatembea akiwa na mawazo mengi, hajui la...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita

Spread the loveWAKATI naandaa makala ya safu hii wiki hii, nimejikuta nakumbuka...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hakuna fedha za Rais

Spread the loveKUNA mambo machache mazuri ya kujifunza kutoka kwa Margaret Thatcher,...

error: Content is protected !!