Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rekodi  inayowaumiza Chadema
Habari za Siasa

Rekodi  inayowaumiza Chadema

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema Taifa
Spread the love

MWAKA 2020 unaelekea ukingoni, hata hivyo umeacha jambo ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Ndani ya mwaka 2020 dalili za kubomolewa kwa chama hicho zilikuwa wazi. Harakari za kumong’onyoa kuta zake  zilifanywa ndani na nje ya chama hicho.

Kilianza kupoteza tawala zake baada ya walioaminiwa kupewa nafasi na hata kuchaguliwa kuwa madiwani na hatimaye mameya kujiengua. Wengine walitimuliwa kwa za chama tawala hila na wengine walijipeleka kwa maslahi binafsi.

Daviud Mwashilindi aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya kupitia Chadema aliamua kwa utashi wake kujivua madaraka hayo kwa madai ya kuunga juhudi.

Ilikuwa tarehe 24 Februari 2020 siku ambayo Mwashilindi aliongoza madiwani 11 kutelekeza Chadema na kujivua uanachama eti wanaunga juhudi.

Chadema haikua na cha kufanya kwa kada wao waliompika na kumjaza ujasiri lakini hatimaye aka-yuda chama chao.

Isaya Mwita, aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam alipigana vilivyo dhidi ya wabaya wake waliopanga kumng’oa.

Alikwenda Kusini na Kaskazini, Mashariki na Magharibi, lililopangwa na wengi kwa hila likamfika, hatimaye alivuliwa umeya hata na akidi isiyokidhi.

Mwita aliondolewa katika wadhifa huo tarehe 9 Januari 2020, kwa tuhuma za kutoidhinisha matumizi ya Sh. 5.8 Bil. zilizotokana na mauzo ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Kabla ya kuondolewa madarakani, Mwita aliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akiiomba itoe amri ya kusitisha mchakato wa kuvuliwa U-Meya, hadi maombi yake ya msingi yatakaposikilizwa.

Mpambanaji huyu aliwasilisha maombi hayo tarehe 8 Januari 2020, katika mahakama hiyo chini ya hati ya dharula. Akipinga kuvuliwa madaraka bila ya kupewa haki ya kujitetea.

Katika maombi hayo, Mwita alidai kwamba, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda walipanga mkakati wa kumuondoa madarakani kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Mwita aligonga mwamba katika maombi hayo, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali maombi yake.

Mahakama ikieleza, haikuona uthibitisho juu ya uwepo wa mkakati wa mwanasiasa huyo kuondolewa madarakani, wala hasara atakayoipata endapo ataondolewa.

Baada ya maombi hayo kugonga mwamba, Mwita aliiomba mahakama hiyo iifute kesi yake ya msingi kwa kuwa, ilikuwa haina maana tena baada ya kuondolewa madarakani. Mwita na Chadema yake waligonga mwamba, hasadi ikashinda.

Alex Kimbe,  alikuwa Meya wa pili wa Chadema kuondolewa madarakani. Tarehe 28 Machi 2020, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia kikao chake maalumu lilimuondoa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Kimbe aliondolewa madarakani kwa kura za ndio 14 kati ya 26 ya wajumbe waliohudhuria  katika kikao hicho, baada ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa dhidi yake, kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Tarehe 31 Machi mwaka huu, Kimbe aliamua kukabidhi ofisi kwa wenye nguvu.

Wakati anakabidhi ofisi hiyo, Kimbe alisema amechukua hatua hiyo kwa kuwa, angeendelea kubaki asingepata ushirikiano kutoka kwa mkurugenzi huyo, ikiwemo uandaaji wa vikao vya baraza la madiwani.

Boniface Jacob, huyu alivuliwa U-Meya wa Halmshauri ya Manispaa ya Ubungo katika mazingira ya kutatanisha, ambapo mkurugenzi wa manispaa hiyo, Beatrice Dominic aliamuandikia barua Jacob akimtaarifu kupoteza sifa ya kuwa mjumbe wa manispaa hiyo.

Kwa mujibu wa barua ya Dominic ya tarehe 2 Aprili 2020 kwenda kwa Jacob, alieleza sababu za mwanasiasa huyo kupoteza sifa ya kuwa mjumbe na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kuwa ni kufukuzwa uanachama wa Chadema.

Dominic alidai kuwa, alipokea barua kutoka kwa uongozi wa Chadema Kata ya Ubungo  iliyomtaarifu  Jacob kufukuzwa uanachama.

Utata wa Jacob kung’olewa U-Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, uliibuka baada ya uongozi wa juu wa Chadema kukana kumvua uanachama mwanasiasa huyo.

Licha ya uongozi wa juu wa Chadema kukana madai hayo na kukiri kwamba Jacob alikuwa mwanachama wake.

Asheri Mlagwa ambaye jina lake lilitumika katika barua iliyodai Jacob amefukuzwa uanachama, alikana kuandika barua hiyo. Huku akitoa wito kwa watu kupuuza barua hiyo.

Kung’olewa kwa Ma-Meya wa Chadema sambamba na wale waliokihama chama hicho kwenda CCM, kulipelekea chama hicho kupoteza halmashauri za majiji  na manispaa iliyokuwa inaziongoza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!