Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais wa China alivyompigia simu Magufuli
Habari za Siasa

Rais wa China alivyompigia simu Magufuli

Rais John Magufuli
Spread the love

RAIS wa China, Xi Jinping amempigia simu Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli na kuzungumza masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania hususani katika masuala ya uchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa iliyotolewana Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema, Rais Jinping amempigia simu Rais Magufuli jana Jumanne tarehe 15 Desemba 2020.

Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa muda wa saa 1, Rais Xi Jinping amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.

Ameeleza, kuchaguliwa kwake kumetokana na kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ambapo uchumi umeimarika zaidi na kwamba anaiona Tanzania kuwa nchi itakayoongoza kwa ukuaji wa uchumi Barani Afrika.

Rais Jinping amempongeza Rais Magufuli kwa namna Tanzania ilivyokabiliana na ugonjwa wa corona (Covid-19) na ameeleza jinsi China inavyoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.

Amempongeza Rais Magufuli kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway) na ujenzi wa bwawa la kuzalisha megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji (Bwawa la Mwl. Nyerere) na ameeleza kuwa China itaangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amemshukuru Rais Jinping kwa kumpigia simu, kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha pili na kumpongeza kwa hatua za kimaendeleo zinazopigwa na Tanzania hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Rais Magufuli amemhakikishia Rais Jinping kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na China uliodumu kwa takribani miaka 55 baada ya kuasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong na kwamba Tanzania itaendelea kuiunga mkono China katika masuala mbalimbali ya kimataifa.

Rais Magufuli amesema, Tanzania inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, utalii, ujenzi na biashara kwa manufaa pande zote mbili.

Aidha, Rais Magufuli ameiomba China kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji wa miradi mikubwa kwa kutoa mikopo nafuu na ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni wa kuzalisha megawati 358 za umeme katika mto Ruhudji, Megawati 222 za umeme katika mto Rumakali na ujenzi wa barabara Visiwani Zanzibar.

Halikadhalika, Rais Magufuli ameiomba China kufungua zaidi masoko ya bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania hususani mazao mbalimbali ya kilimo.

Rais Jinping ameahidi kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli ikiwemo ujenzi wa miradi ya kuzalisha umeme ya Ruhudji na Rumakali, ujenzi wa reli, Bwawa la Nyerere na ununuzi wa mazao ya Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!