Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Rais Magufuli, ‘toka mafichoni’ ujiandikie historia yako
Makala & UchambuziTangulizi

Rais Magufuli, ‘toka mafichoni’ ujiandikie historia yako

Rais John Magufuli
Spread the love

DK. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano, anakaribia kutimiza miaka mitatu kamili madarakani. Aliapishwa tarehe 5 Novemba 2015. Anaandika Sead Kubenea … (endelea).

Dk. Magufuli, amekuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano. Watangulizi wake wengine kwenye nafasi hiyo, ni Julius Kambarage Nyerere (1961-1985); Ally Hassan Mwinyi (1985-1995); Benjamin Mkapa (1995-2005) na Jakaya Mrisho Kikwete (2005-2015).

Ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake, kuna mengi yamefanyika – mabaya na mazuri.

Miongoni mwa mazuri yanayotajwa, ni pamoja na vita dhidi ya rushwa, ujenzi wa miundombinu, ufufuaji wa shirika la ndege la taifa (ATCL) na kuwaondolea wazazi makali ya mzigo wa ada kwenye sekta ya elimu.

Hata hivyo, katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli, kumefanyika mambo mengi ya hovyo na katili. Mengine hayajawahi kuonekana tangu taifa hili lipate uhuru wake.

Kwa mfano, ndani ya miaka mitatu hii, taifa limezidi kutumbukia kwa kasi katika visa vya visasi, kutekwa na kuteswa; na matukio mengine dhidi ya wananchi na vyombo vya habari.

Ndani ya miaka mitatu, wananchi wameshuhudia, Bunge la Jamhuri – chombo kikuu cha wananchi – kikiendeshwa gizani. Mikutano ya vyama vya siasa ikizuiliwa kwa kisingizio cha “walioko madarakani waachwe watimize majukumu yao.” Orodha ni ndefu.

Lakini jambo moja ni wazi, kwamba Rais Magufuli siyo malaika na siyo mtakatifu. Ni binadamu. Anakosea na aweza kujirekebisha na kwa hakika, anapaswa kufanya hivyo sasa.

Kwamba, miaka miwili iliyosalia ya kuishi kwake Ikulu, badala ya kushughulikia mambo yanayoonekana kutokuwa na tija, kama vile kujibizana na; au “kunyang’anyana” vinasa sauti na wapinzani, rais anapaswa kushughulikia mambo mawili makubwa:

Kwanza, ni kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na hatua ya chama kikuu cha upinzani nchini (Chadema) na washirika wake kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kususia chaguzi ndogo.

Kilio cha upinzani, ni kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), siyo chombo huru. Hili linathibitishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva.

Mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, Jaji Lubuva alikiri kuwa tume yake siyo chombo huru. Akataka katika mchakato wa Katiba Mpya, “kiundwe chombo huru kitakachosimamia uchaguzi.”

Aliongeza, “…ili chombo hicho kipate mwafaka wa kitaifa wa kusimamia mchakato mzima kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chini ya Katiba Mpya, ni sharti mchakato wa uteuzi wa watendaji wake uwe wazi.” Haya yamo katika randama ya Tume ya Jaji Warioba.

Madai ya kuwapo Katiba Mpya na “tume huru ya uchaguzi,” yanatokana na ukweli kuwa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 inayotumika sasa, imesheheni matundu ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, ndani ya mazingira ya vyama vingi.

Aidha, ndani ya vyama vingi, kumewekwa mifumo na vyombo vya kusimamia uchaguzi, kwa mshololo wa “ujima wa chama kimoja.”

Kwamba ili kuwapo kwa uchaguzi huru na haki, vyombo vikuu vya kusimamia “maamuzi ya wananchi wanayoyatoa kupitia sanduku la kura,” sharti viwe huru na vinavyoaminika.

Ni sharti sheria zinazosimamia mifumo ya uchaguzi, iwe na uwezo na mamlaka ya kutoa haki kwa pande zote zinazoshiriki uchaguzi.

Sharti pia mfumo wa kuendesha uchaguzi uwe endelevu na unaobeba uwakilishi wa kutosha wa wadau; wenye kutenda haki na unaojitegemea kimamlaka na kimaamuzi.

Hayo hayapo katika NEC ya sasa ambayo, kwa maoni yangu na kadri ninavyoelewa na kuamini, siyo chombo huru cha kusimamia uchaguzi.

Wadau wengi wa uchaguzi – ukiondoa Chama Cha Mapinduzi, ambacho ndio wanufaikaji wakuu wa mfumo huu – hawakubaliani na muundo wa NEC.

Hawakubaliani na baadhi ya sheria zinazosimamia uchaguzi na hawaamini vyombo vinavyosimamia uchaguzi.

Kilio hiki kimekuwapo tokea mwaka 1991 – takribani miaka 27 iliyopita – wakati Rais Ali Hassan Mwinyi alipounda tume ya kukusanya maoni juu ya mfumo upi unafaa kutumiwa – wa chama kimoja au vyama vingi. Tume iliongozwa na Jaji mkuu, Francis Nyalali.

Pamoja na kutaka kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kuundwa kwa “Tume Huru ya Uchaguzi.” Ilitoa pia mifano ya nchi ambako tume zinazosimamia uchaguzi siyo huru.

Tume ilionya madhara yanayoweza kutokea iwapo taifa halitakuwa na chombo huru cha kusimamia uchaguzi.

Miongoni mwa aliyotaja ni mauaji, machafuko, kudidimia kwa uchumi wa taifa, njaa na maradhi. Hakusikilizwa.

Katika Kifungu cha 591 cha ripoti yake, Jaji Nyalali alisisitiza, “…ni lazima muundo wa tume ya taifa ya uchaguzi ubadilike ili kukidhi haja ya demokrasia ya vyama vingi.”

Nayo Tume iliyoundwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri, Benjamin Mkapa (1999), kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba, ilipigilia msumari mwingine kuhusu muundo wa sasa wa NEC.

Katika ripoti yake, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Robert Kisanga alisema, pamoja na mambo mengine, “…hatua ya wajumbe wa Tume kuteuliwa na rais ambaye ni kiongozi wa chama cha siasa kinachotawala, ama watakuwa na upendeleo kwa chama husika au watakuwa wanalipa fadhila kwa aliyewateuwa.”

Jaji Kisanga anasema, uteuzi wa wajumbe unapofanywa na kiongozi ambaye ni mgombea mtarajiwa kwenye uchaguzi ujao na chama chake kimesimamisha wagombea kwenye nafasi mbalimbali, hakuna shaka kuwa wasimamizi hao watajiegemeza kwenye chama cha aliyewateua.

Haya yameonekana wazi katika chaguzi hizi ndogo. Katika baadhi ya maeneo walioshinda, siyo waliotangazwa. Ndio chanzo cha upinzani kususia chaguzi zinazoendelea. Hatufahamu iwapo watasusia uchaguzi mkuu ujao ama watashiriki.

Pili, Dk. Magufuli anapaswa kutumia miaka miwili hii, kujikita katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa Visiwani Zanzibar.

Mgogoro huu uliotokana na hatua ya Jecha Salim Jecha, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), kumtangaza Dk. Alli Mohammed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, unaweza kumalizika kwa njia ya majadiliano.

Hauwezi kumalizwa kwa njia ya “kumuangamiza,” Maalim Seif Shariff Hamad na chama chake. Huo waweza ukawa mwanzo wa mifarakano, minyukano, uhasama, kutoaminiana na uvunjifu wa sheria.

Hii ni kwa sababu, kufuta uchaguzi, bila kutafuta suluhu ya kilichosababisha hatua hiyo kutendeka, kisha ukaitishwa uchaguzi mwingine katikati ya giza, ni kuficha moto kwenye majani makavu. Yatalipuka.

Wala kufanyika kwa uchaguzi wa marudio kulikohitimishwa na kumtangaza Dk. Shein kuwa mshindi, hakuwezi kuwa mwisho wa migogoro ya kisiasa Visiwani.

Hata hatua ya Chama cha Wananchi (CUF), kususia uchaguzi wa marudio, hakuwezi kuwa suluhu na hivyo kusema, “mambo yameisha.” Yaweza kuwa inajipanga kwa sababu za msingi kwamba sehemu kubwa ya jamii imebaguliwa.

Urais wa Dk. Shein unatokana na kilichoitwa “uchaguzi wa marudio” Visiwani uliofanyika 20 Machi 2016.

Uchaguzi wa marudio Zanzibar ni tunda la Jecha, aliyefuta uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 kwa madai kuwa “kulikuwa na kasoro nyingi.”

Huu ni uchaguzi ambao waangalizi wa ndani na nje walisema “ulikuwa huru na wa haki” na ambamo Maalim Seif, katibu mkuu wa CUF, alidai alikuwa amechaguliwa “kwa kishindo.”

Ripoti za waangalizi zinazoonesha uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, Visiwani ulikuwa huru na haki, ni pamoja na ile iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya (SADC) na Umoja wa Africa (AU).

Lakini uchaguzi wa marudio umefanyika bila kupata majibu mwafaka ya uhalali wa uamuzi wa Jecha kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba.

Hivyo basi, rais anapaswa kueleza wasaidizi wake, kuwa hii siyo mara ya kwanza kuibuka mgogoro wa kisiasa Zanzibar. Waweza kuwa siyo wa mwisho pia. Kuna migogoro mingi imeibuka. Mingine imetatuliwa na mingine imeshindikana.

Mgogoro ambao bado unakumbukwa na wengi, ni ule wa mwaka 2000. Machafuko makubwa ya kisiasa, vurugu na mauaji yalitokea 26 na 27 Januari 2001 huko Unguja na Pemba.

Taarifa huru zinasema, watu zaidi ya 40 walifariki dunia katika machafuko hayo. Wengine mamia waliomba hifadhi ya ukimbizi nchini Kenya. Taifa ambalo lilikuwa kimbilio la wakimbizi, kwa mara ya kwanza, likazalisha wakimbizi wake.

Lakini akiamua anaweza kunyamaza – japokuwa siyo jambo jema – kwa kuwa mgogoro mpya wa Zanzibar, “unamvua nguo” zaidi mtangulizi wake – Rais Kikwete – kuliko unavyomuaibisha yeye.

Hii ni kwa sababu, Kikwete anaijua vema Zanzibar kuliko Magufuli. Aliwahi kufanya kazi Zanzibar. Ameishi Zanzibar na amekuwa ndani ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi – kwa miaka mingi, ukilinganisha na mrithi wake.

Hili amelithibitisha hata katika hotuba yake ya kwanza mbele ya Bunge, tarehe 30 Desemba 2005. Alikiri “Zanzibar kuna mpasuko wa kisiasa.”

Alitamka kwa sauti ya ukakamavu kuwa atafanya kila awezalo kumaliza mpasuko wa Zanzibar. Hakuishia kusema tu. Aliunda kamati ya maridhiano iliyoshirikisha chama chake (CCM) na CUF, ili kutafuta njia ya kumaliza mgogoro.

Vikao kadhaa vilifanyika, tena kwa maelekezo yake kwa lengo la kutafuta suluhu. Mazungumzo yaliyochukua miezi 14 yalimalizika; ikawa sasa kazi ya vikao vya juu vya vyama hivyo kuidhinisha kile kilichokubaliwa.

Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, uliofanyika Butiama mkoani Mara, tarehe 2 na 3 Machi 2008, ulimalizika bila makubaliano. Ni baada ya CCM kuibua hoja mpya ya kutaka kufanyika kura ya maoni.

Alhamisi, 21 Agosti 2008, Kikwete aliliambia Bunge mjini Dodoma, kwamba CCM na CUF, haviaminiani. Alikuwa akielezea mazungumzo kati ya vyama hivyo viwili yenye shabaha ya kuleta mwafaka mpya katika kile alichoita “kumaliza mpasuko Zanzibar.”

Alisema yeye, Rais Kikwete, ni mtu mzima; anajua kuna tatizo; anatafuta njia mwafaka ya kuhakikisha anafika anakokwenda.

“Sijakata tamaa. Najua lipo tatizo kubwa la kutoaminiana. Tutaangalia kama kura ya maoni au makubaliano ya vyama yanatosha,” alisema Kikwete.

Lakini alikuwa ni kada wa CCM na muasisi wa Afro-Shirazi Party (ASP), Hassan Nassor Moyo, aliyemaliza mvutano Visiwani. Aliwakutanisha Maalim Seif na Rais Karume. Serikali mpya ikaundwa. Utulivu ukapatikana.

Lakini ni Kikwete huyohuyo anayetuhumiwa kuchochea mgogoro huu wa sasa; na au kuunyamazia.

Haikutarajiwa mtu ambaye miaka 10 iliyopita, amekiri bungeni kuwa “Zanzibar kuna tatizo na linahitaji ufumbuzi wa haraka kwa manufaa ya nchi na wananchi wake,” ndiye huyohuyo aliyeshindwa kutambua tatizo kwa sababu ya kutaka kulazimisha ushindi kwa chama chake.

Kikwete anafahamu kuwa ni rahisi kwa CUF kushirikiana na CCM kuliko CCM kukubali kushirikiana na CUF. Hivyo ndivyo ilivyotokea pale CUF ilipoonekana kuelekea kushinda uchaguzi.

Hii ni kwa sababu, chama kilichokuwa madarakani kwa nusu karne, hakiko tayari hata kuona chama kingine kikiunda utawala kwa ngazi ya halmashauri, jiji na manipaa ambako kimeshindwa.

Panahitajika ukomavu wa kisiasa. Kwamba mtu yumo katika chama kilichoko madarakani haina maana kwamba ndiye mwenye akili nyingi na hekima.

Wananchi wamechoka chokochoko na malumbano ya mwaka hadi mwaka. Rais anaweza kututoa katika mkwamo huu. Anaweza kujiandikia historia yake. Ni vema akafanya hivyo. Siyo tu kwa Zanzibar, hata kwa Bara.

Katika hili, mwalimu mzuri, ni rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume. Alirithi mgogoro wa Zanzibar, lakini akiwa Ikulu akafanya juhudi za kuutatua. Nchi yake ikatulia. Umoja na mshikamano kwa wananchi ukarejea.

Mwandishi wa makala hii, ni mkurugenzi mtendaji wa gazeti la MwanaHALISI, mwandishi wa habari na mbunge wa Ubungo (Chadema). Anapatikana kwa simu Na. 0782 072292.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!