RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wakurugenzi watatu katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Mbeya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania, Gerson Msigwa imesema, uteuzi wa viongozi hao umeanza leo Jumamosi tarehe 4 Julai 2020.
Msigwa amesema, Rais Magufuli amemteua Anastazia Tutuba kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro.
Kabla ya uteuzi huo, Tutuba alikuwa Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Mkoa wa Arusha na anachukua nafasi ya Anna-Claire Shija.
Pili, Rais Magufuli amemteua Saad Mutambule kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Mkoa wa Arusha.
Kabla ya uteuzi huo, Mutambule alikuwa Afisa Mipango wa Jiji la Mbeya mkoani Mbeya na anachukua nafasi ya Alvera Ndabagoye ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Tatu, Rais Magufuli amemteua Elias Amede Ng’wanidako kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mbeya Mkoa wa Mbeya.
Kabla ya uteuzi huo, Ng’wanidako alikuwa Mweka Hazina wa Jiji la Mbeya na anachukua nafasi ya James Kasusura ambaye amestaafu.
“Wateule wote wanatakiwa kuwepo Ikulu, Chamwino Mkoa wa Dodoma tarehe 06 Julai, 2020 saa 4:00 asubuhi,” amesema Msigwa
Leave a comment