February 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Safari awasulubu Mdee, Spika Ndugai

Spread the love

PROFESA Abdallah Safari, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema, Halima Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho amapotosha umma huku akishangazwa na mahaba ya ghafla ya Job Ndugai, Spika wa Bunge kwa wapinzani. Anaandika Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, yapo mashaka kati ya uamuzi wa Mdee na wenzake 18 kukiuka katiba ya chama hicho na msimamo unaolazimishwa na Spika Ndugai kuwatambua wanachama waliotimuliwa na chama chao kwamba waendelee kuwa wabunge.

Amesema, msimamo wa Mdee kwamba, mazingira ya uchaguzi mkuu 2020 yaliyosukumu vyama vya upinzani kugomea matokeo ya uchaguzi na kutopeleka wabunge bungeni, yanafanana na yale ya mwaka 2010 na 2015, ni upotoshaji.

Prof. Safari ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chadema kabla ya kustaafu kwake, amesema kiwango cha makosa kwenye uchaguzi wa mwaka huu na msimamo wa chama hakijawahi kutokea huko nyuma.

“Chaguzi zilizopita zina tofauti kubwa na uchaguzi huu, tofauti yake kiwango cha makosa ya uchaguzi ni kikubwa sana, Zitto (Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo) na Lissu (Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema) walitoa ushahidi kwenye press (mkutano na waandishi),” amesema aliyewahi kuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Matatizo Zanzibar yametokea ikiwa ni pamoja na watu kuuawa, nyumba kuvunjwa. Kama tungekuwa na uwezo wa kushitaki kutengua urais kama ilivyo Malawi na Kenya, mwaka huu ingekuwa rahisi sana. Halima na wenzake wasifananishe ushahidi wa mwaka huu na miaka iliyopita.”

Prof. Safari amesema, mwaka huu chama kimefanya uamuzi wa kutopeleka wabunge tofauti na chaguzi zilizopia ambapo hakukuwa na uamuzi huo.

Akizungumzia uamuzi wa Spika Ndugai kuwatambua Mdee na wenzake 18, amesema mwenye mamlaka ya kutafsiri sheria kutokana na sakata la kina Mdee ni mahakama pekee.

“Mwenye mamlaka ya kutafsiri sheria za nchi hii, sio Mwanasheria Mkuu, sio spika, sio DPP wala sio Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Mtu mwenye mamlaka ya kusema sheria hii maana yake ni hii, ni mahakama.”

“Ukishatimuliwa, huwezi kukingiwa kifua na mtu yeyote yule na bahati nzuri, matukio haya yametokea mara nyingi sana. Wakati wa TANU walifukuzwa akina Elia Anangise, wengi tu walitimuliwa, wabunge wa CUF walitimuliwa mara nyingi tu, hao CCM wenyewe hivi karibuni akina Sofia Simba walitimuliwa na walitema ubunge,” amesema.

Profesa Safari amesema, “Itakuwaje ghafla mambo yabadilike, hii ni fedheha. halafu inashangaza, tangu lini Ndugai akawa na urafiki na wabunge wa upinzani? hawa akina Halima Mdee mwenyewe na rafiki yake mkubwa Bulaya waliishafukuzwa na Ndugai bungeni.”

Ameshangazwa na mabadiliko ya ghafla aliyoyaonesha Spika Ndugai kwa Mdee na wenzake 18 waliotimuliwa Chadema kung’ang’ania kuwatimua.

“Leo kwanini (Ngudai) anakuwa na usuluba mkubwa sana wa kuwakingia kifua?  na (Ndugai) anabishana na spika anayeheshimika zaidi kuliko maspika wote wa nchi Pius Msekwa na Msekwa ni mwanasheria, sasa dhana yake ni nini?” amehoji na kuongeza:

“Kuna kitu hawataki kukisema, sasa kuna siku watakisema. Kwanini unang’ang’ania hawa waendelee kuwa wabunge?”

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa Chadema kwa tuhuma za usaliti, kughushi na kujipeleka bungeni kuapishwa tarehe 24 Novemba 2020 na Spika Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, wakijua chama hicho, hakijapendekeza majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Uamuzi wa kamati kuu, ulitolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe tarehe 27 Novemba 2020 akisema, Mdee na wenzake wamekisaliti chama na kama hawaridhiki na uamuzi huo wa kuwafukuza, wanaweza kukata rufaa baraza kuu ndani ya siku 30 au kuomba radhi.

Hata hivyo, Spika Ndugai alisema, yeye ataendelea kuwatambua Mdee na wenzake 18 kama wabunge  hadi pale ‘wao wenyewe kwa mujibu wa katiba wapende kujiuzulu.”

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa ni wale waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko. Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje. Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega.

Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga. Naibu Katibu Mkuu Bawacha, Jesca Kishoa  na Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambat.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mtwara, Tunza Malapo, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao.Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

error: Content is protected !!