Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Assad anaendelea kuwa mwiba kwa serikali
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Assad anaendelea kuwa mwiba kwa serikali

Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad
Spread the love

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amefichua tuhuma nyingine mpya. Safari hii, CAG anaituhumu Serikali kutumia zaidi ya Sh. 2.7 bilioni, bila kufuata taratibu za kifedha. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) zinasema, CAG amegundua matumizi hayo ya mabilioni hayo ya shilingi kufuatia ukaguzi wake uliofanywa kwenye akaunti ya mfuko mkuu wa serikali (HAZINA).

“Ni kweli, CAG amegundua kuwapo kwa matumizi ya mabilioni ya shilingi yaliyotumika bila kufuata taratibu. Si hivyo tu, CAG amegundua kutumika kwa fedha nyingine kadhaa, zikiwamo zilizohamishwa kutoka fungu moja kwenda fungu jingine, kinyume na utaratibu wa Bunge,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

Aidha, ofisi hiyo ya mkaguzi imegundua kuwapo kwa kiasi cha zaidi ya Sh. 7.3 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge kwa matumizi ya idara na taasisi za serikali, kuhamishiwa kwenye maeneo mengine, bila idhini ya Bunge.

Vilevile, taarifa zinasema, CAG bado ameendelea kung’ang’aniza kuwa kiasi cha Sh. 1.5 trilioni, alizozitaja kwenye taarifa yake yam waka uliyopita, hazijaweza kupata majibu yanayoridhisha.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuagiza Prof. Mussa Assad, mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, kufuatia kiongozi huyo kunukuliwa akisema, “Bunge la Tanzania ni dhaifu.”

Katika sakata hilo, Spika Ndugai alifika mbali zaidi, baada ya kuelekeza shughuli zote za Kamati ya PAC na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kusimamishwa.

Bunge la Jamhuri, kupitia kamati zake hizo mbili – PAC na LAAC – ndizo zenye “mamlaka ya Kikatiba” ya kupokea na kuchambua, taarifa ya kila mwaka ya CAG, jambo ambalo lilifanya hatua ya Spika Ndugai ya kusimamia kazi za  kamati hizo, kwenda kinyume na Katiba.

Kanuni za Bunge zinaelekeza kuwa baada ya PAC kupokea taarifa kutoka kwa CAG na kisha kuifanyia uchambuzi, huandaa ripoti inayowasilishwa kwa spika na baadaye bungeni.

Katika mkutano wa Bunge wa bajeti uliyopita, serikali kupitia kwa naibu waziri wa fedha,Dk. Ashatu Kijaji, ilidai kuwa kati ya fedha hizo, Sh. 204 bilioni ziliingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Mlipaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Dk. Kijaji aliliambia Bunge, tarehe 8 Juni 2018, kuwa kati ya Sh. 1.5 trilioni ambazo CAG anasema, matumizi yake hayaonekani, Sh. 204 bilioni, ni makusanyo ya Zanzibar na kwamba zililipwa moja kwa moja huko.

“CAG ameileza kamati ya PAC kuwapo kwa matumizi ya mabilioni ya shilingi uliofanywa na serikali, kinyume na taratibu. Miongoni mwa majibu hayo, ni pamoja na baadhi ya fedha ambazo hazionyeshi matumizi yake na nyingine kuhamishiwa kwenye taasisi nyingine, kinyume na Bunge lilivyoidhinisha,” anaeleza mmoja wa wajumbe wa Kamati ya PAC.

Taarifa nyingine kutoka ndani ya kamati zinasema,  mkaguzi huyo bado anasisitiza kuwa serikali haijaweza “kujisafisha kikamilifu” kwenye baadhi ya maeneo yanayohusu matumizi ya fedha za umma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!