Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Polisi wavamia makao makuu Chadema
Habari za Siasa

Polisi wavamia makao makuu Chadema

Spread the love

MAOFISA waandamizi wa jeshi la polisi jijini Dar es Salaam, wamevamia makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jioni hii ya Jumatatu. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Taarifa kutoka mtaa wa Ufipa, Kinondoni, ambako ndiko makao makuu ya Chadema yalipo zinasema, polisi hao waliokuwa na magari matano, walivamia ofisi hizo, majira ya saa moja kamili jioni hii kwa lengo la kufanya upekuzi. 

Hata hivyo, hawakueleza upekuzi huo unalenga kitu gani.

Afisa mmoja anayefanya kazi makao makuu ya Chadema amethibitisha kufika kwa maofisa hao wa polisi na kwamba chama hicho, kiligoma kuwaruhusu kufanya kazi hiyo.

“Ni kweli walikuja hapa ofisini jioni hii kwa lengo la kutaka kufanya upekuzi. Lakini tumewakatalia kwa kuwa hawakuwa wamefuata taratibu,” ameeleza mfanyakazi huyo aliyekuwapo ofisini wakati polisi walipofika eneo hilo.

Anasema, “tumewazuia kwa kuwa hawawa na kibali kinachoruhusu upekuzi. Tumewazuia kwa kuwa hawakueleza kile wanachokitafuta.”

Kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja katika kipindi ambacho kunafanyika juhudi kubwa za kukihusisha chama hicho na mauaji ya Akwina Akwilina.

Akwine, alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kwenye chuo cha usafirishaji cha taifa (NIT), kilichopo Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Alifariki dunia Ijumaa iliyopita, akiwa ndani ya basi aina ya daladala, kufuatia kupigwa risasi ya kichwa. Risasi iliyokatiza maisha ya Akwilina inadaiwa ilifyatuliwa na askari wa jeshi la polisi.

Miongoni mwa wanaohaha kuituhumu Chadema na mauaji hayo, ni kada wa Chama Cha  Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba. Mwigulu, ndiye waziri wa mambo ya ndani ya nchi ambapo jeshi la polisi liko chini yake.

Akiandika kupitia group moja la wasap linaloitwa,“Singida Siasa Forum,” Mwigulu anasema, “kujiuzulu kwa lipi? Hawa watu (Chadema), hata Morogoro walifyatua risasi wakamuua muuza magazeti na kuwahi kusema, polisi wameuwa.”

Amesema, “haya mambo yanahitaji uchunguzi wa kina kabla ya kusema waziri jiuzulu.”

Mwigulu hakutaja ushahidi unaonyesha kuwa Chadema ndio iliyompiga risasi Ali Zona, ambaye alikutwa na mauti akiwa kwenye kibanda chake za kuuzia magazeti mjini Morogoro.

Mwigulu alikuwa akijibu madai ya baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wanaomtaka kuachia ngazi kutokana na “uzembe wa polisi wa kusababisha kifo cha Akwilina.

Aliyeshikilia bango Mwigulu kujiuzulu, ni Abdul Nondo, mwanafunzi wa mwaka wa tatu kwenye chuo kikuu cha Dar es Salaam. Anachukua masomo ya utawala na sayansi ya siasa.

Tangu kutokea kifo cha Akwilina makada wa CCM wamekuwa wakihaha kushawishi umma kuwa mauaji hayo yamesababishwa na Chadema.

Baadhi ya makada hao wamediriki hata kudai kuwa risasi aliyopigwa Akwilina imerushwa na wafuasi wa Chadema. Wafuasi hao walikuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, kudai hati za viapo vya mawaka wao.

Aidha, kupatikana kwa taarifa kuwa polisi wametaka kufanya upekuzi kwenye ofisi za Chadema zimekuja siku moja baada ya upekuzi wa aina hiyo, kufanyika makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), Visiwani.

Taarifa zilizomnukuu mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma ya CUF, Salim Bimani zinasema, upekuzi huo uliofanyika jana Jumapili, haukuelezwa na polisi ulilenga kitu gani.

Badala yake, Bimani anasema, “walikuja hapa ofisini na nyaraka zinazowaruhusu kutaka kufanya upekuzi. Tuliwaruhusu baada ya kuona taratibu za kisheria, zimekamilika. Lakini wamesema, ‘hakuna walichokipata.’”

Taarifa iliyotolewa baadaye na kurugenzi ya itifaki, mawasiliano na mambo ya nje ya Chadema inasema, maofisa hao wa polisi walijitambulisha kuwa wametokea ofisi ya upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

“Walinzi wetu waliwakatalia kwa kuwa hawakufuata utaratibu na wala hawakueleza kuwa wanataka kupekua nini ndani ya ofisi zetu,” ameeleza John Mrema, mkurugenzi wa mawasiliano na mambo ya nje ya Chadema.

Mrema anasema, “kwa nini wamekuja usiku? Kama huu ndio utaratibu mpya wa jeshi la polisi, basi tunatarajia ukaguzi huu ukaanzie CCM, ambako kuna tuhuma kubwa za kuhifadhi watekaji na watesaji.”

Mrema anasema, “tunatoa wito kwa polisi wafuate sheria za nchi katika kutimiza wajibu wao. Ni kwa sababu, ni jambo la hatari kwa wasimamizi wa sheria kuvunja sheria wanazopaswa kuzisimamia.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Wagombea 127 wa udiwani kutoka vyama 18 kuchaguliwa kesho

Spread the loveWagombea udiwani 127 kutoka vyama 18 vya siasa wanatarajiwa kupigiwa...

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

error: Content is protected !!