July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Polisi Z’bar wamwachia Mazrui

Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar

Spread the love

JESHI la Polisi Visiwani Zanzibar leo Jumanne tarehe 17 Novemba 2020, limemwachia kwa dhamana Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Nassor Ahmed Mazrui pamoja na mwanachama wa chama hicho, Ayoub Bakari, waliokuwa wanashikiliwa kwa zaidi ya siku 15. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa na Janeth Rithe, Naibu Katibu Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, muda mfupi baada ya wanasiasa hao kuachiwa.

“Tunapenda kuwajuilisha wanachama na wapenzi wa chama chetu kwamba, naibu katibu mkuu wetu kwa upande wa Zanzibar, Mazrui na mwanachama wetu, Hamad wameachiwa kwa dhamana,” inaeleza taarifa ya Rithe.

Mazrui na Ayoub walikamatwa katika nyakati tofauti wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, yaliyoitishwa na ACT-Wazalendo pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufanyika tarehe 2 Novemba 2020.

Vyama hivyo vinapinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) yaliyokipa ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani, kwa madai mchakato wa uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Kuachiwa kwa Mazrui na mwenzake kumekuja ikiwa imesalia siku moja kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha utetezi wao katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, kwa nini hawakutoa dhamana kwa wanasiasa hao kwa mujibu wa sheria.

Jeshi hilo la Polisi, limetakiwa kuwasilisha utetezi huo kesho Jumatano tarehe 18 Novemba 2020.

Amri hiyo ya mahakama kwa Jeshi la Polisi ilitolewa baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kufungua kesi ya kuitaka Mahakama Kuu ya Zanzibar itoe amri kwa Mazrui na wenzake kufikishwa mahakamani au kuachiwa huru.

error: Content is protected !!