JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekiri kumshikilia Tito Magoti, Afisa Program wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ( LHRC ),kwa tuhuma za makosa ya jinai. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea)
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 20 Desemba 2019, na SACP Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Kanda hiyo.
Hata hivyo, Mambosasa hakuweka bayana aina ya makosa ya jinai, yanayomkabili Magoti, pamoja na watu wengine watatu, ambao wamekamatwa na polisi, leo majira ya saa tano asubuhi, maeneo ya Mwenge, jijini Dar es Salaam.
Kamanda Mambosasa amesema Magoti na wenzake, wanahojiwa na Jeshi la Polisi, na kwamba uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili ukikamilika, watafikishwa mahakamani.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Magoti, Mkazi wa Ubungo Kibo , pamoja na watu wengine watatu kwa uchunguzi na mahojiano zaidi. Wanaendelea kuhojiwa kwa tuhuma za makosa ya jinai,” ameeleza Kamanda Mambosasa.
https://youtu.be/uM77yTNOPas
Hata hivyo, Kamanda Mambosasa amesema taarifa ya kwamba Magoti ametekwa na watu wasiojulikana si za kweli, kwa kuwa yuko katika mikono salama ya Jeshi la Polisi.
Leave a comment