Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Z’bar itafakari kauli ya Polepole
Makala & Uchambuzi

Z’bar itafakari kauli ya Polepole

Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM
Spread the love

TANGU Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole afanye ziara ya kikazi Zanzibar mwaka jana, akili za wanachama na hasa wale wenye ushawishi katika kufikiwa maamuzi ndani ya chama hicho, hazijatulia sawasawa. Anaandika Jabir Idrisa, Zanzibar…(endelea).

Akitambua fika kilichokuwa kikiendelea fikirani mwa wanachama kuhusu ni nani atakayemrithi Dk. Ali Mohamed Shein utakapowadia uchaguzi mkuu, Polepole “alidondosha” kauli nzito, labda kwa kuamini inaweza kuwa muongozo kwao.

Akiwa juu ya jukwaa la mkutano wa hadhara, Polepole, aliyekuwa mpya machoni mwa wengi katika chama, kwanza alianza kwa kuwananga wale aliosema wanajipanga kuwania nafasi hiyo; wanakosea kwani wanakiuka utaratibu.

Akasema kwa wale wanaodhani nafasi hiyo hupewa mtu yeyote tu muradi anatoka ndani ya chama, wasahau. Ndipo akakunjua makucha, akatunisha misuli ya shingo na kunyooshea mkono wasikilizaji wake.

Kauli nzito: Mnajihangaisha bure kutengeneza kambi eti mnataka kuteuliwa kugombea urais 2020. Hakuna anayemfahamu mrithi wa Dk. Shein na wala msidhani atapatikana kwa utaratibu mliouzoea. Mimi niwaambie msijisumbue! Chama kitamtoa “mtu wake” Dodoma; mtaletewa mumpigie kura huyo.

Ni kauli nzito kwelikweli. Na imechukuliwa hivyohivyo tangu hapo. Lakini kauli ya Polepole imesababisha mjadala mkali na mpana ndani ya chama, achilia mbali nje yake ambako ni kawaida pia jambo hilo kuchochea mjadala.

(Urais si kazi ya mchezo ndo maana humchangamsha kifikra kila aliye mfuatiliaji siasa nchini. Na hali huzidi nyumbani Zanzibar ambako siasa ni chakula cha moyo kwa watu wake kila siku iendayo kwa jaala).

Sasa hili ndilo swali muhimu katika siasa za CCM kwa Zanzibar tangu pale: Ni mwanachama gani atapewa tunu hii ya kugombea kiti cha urais wa Zanzibar itakapoamuliwa kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar ufanyike.

Hivyo, makada wanajadiliana jambo hili usiku na mchana; wawapo maofisini katika chama na hata walioko serikalini na kwengineko. Wanajadiliana kwenye viwanja vya michezo na marikiti na wanajadiliana kwenye mikusanyiko ya shughuli za kijamii kama vile harusi na misiba. Ni mjadala mtindo mmoja.

Yumkini wakati Polepole anaamua kutoa kauli yake, maneno na minong’ono iliyokuwa ikisikika kusemwa viwanjani mwa duru za siasa miongoni mwa wakubwa, ndio ukweli wa mambo. Kwamba walishakuwepo viongozi wawili- watatu wamejipeleka juu kiushawishi kama kwamba watakuwa orodhani muda utakapowadia.

Basi walio wakitajwa mbele kabisa mwa orodha ya kuhangaikia kumrithi Dk. Shein, ni Balozi Seif Ali Iddi, makamu wa pili wa rais, na Dk. Khalid Salim Ali, waziri wa fedha na mipango wakati ule. Taarifa za ndani ya mamlaka zinadai kuwa hao hasa ndio waliolengwa haraka katika kauli ya Polepole, mtendaji wa CCM aliye karibu zaidi kikazi na Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

Viongozi hao wawili hawakuwa peke yao waliokuwa wakitajwa kwa kujenga matamanio ya kuidaka nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini. Wapo wengine wachache. Lakini, wao ndio waliokuwa wakitajwa hata kuunda kambi pinzani kiasi cha kusemekana kuchukiza uongozi wa juu chini ya Rais Magufuli.

Wakati fulani, kulingana na vyanzo vya taarifa kutoka mamlaka ya juu ya CCM, kulienea fununu kuwa Balozi Seif na Dk. Khalid waliwahi “kukaripiwa” na kiongozi mkubwa kuwa waache kujishughulisha na harakati hizo badala yake wamsaidie kazi Dk. Shein ya kuongoza Zanzibar.

Ni kama vile kuambiwa kuwa hawana sababu ya kuhangaikia suala hilo kwa sasa kwa kuwa muda wake ukifika, kutakuwa na wasaa wa kutosha wa kushiriki utaratibu utakaowekwa kwa kila anayetamani kuingia kuwania.

Baadaye, kukatokea matukio au hali mbili kuhusu suala hilo: Kwanza ilitokea Balozi Seif kutangaza hadharani kuwa hatogombea nafasi yoyote – atajiuzulu siasa – baada ya kumaliza awamu ya uongozi uliopo.

Maana yake hatogombea kiti cha uwakilishi jimbo la Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako kuingia kwake kulizusha tafrani kubwa na wanasiasa wengine mkoani; na hiyo ikawa na maana kuwa amesita kuendelea na shauku ya kusaka urais.

Hali ya pili ni pale Dk. Shein alipomtema Dk. Khalid katika wadhifa adimu wa hazina – Wizara ya Fedha na Mipango. Dk. Khalid aliondolewa mapema Machi mwaka huu na akateuliwa Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, mwanasiasa wa enzi.

Wapo wanaodhani kuondolewa kwa Dk. Khalid kulichagizwa na harakati zake hizo za kujipanga kwa kuwania urais. Jitihada za kumpata ili atoe kauli kuhusu hilo, hazikufanikiwa.

Walio karibu naye wanadai, daktari huyu wa mipango ya uchumi hajapunguza kasi hasa kwa kuwa angali tegemeo la kimustakbali la watu wa Donge, linalojulikana kuwa ngome imara ya CCM katika mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kama alivyo Balozi Seif, Dk. Khalid naye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa kuchaguliwa kutokea jimbo la Donge, akishika ngome hiyo iliyokuwa ikilindwa na Ali Ameir Mohamed na Ali Juma Shamhuna, wanasiasa wakongwe waliotajika kwa siasa za kijabari za kudhibiti mambo, baada ya kufifia kizazi cha wana Afro-Shirazi Party (ASP) kama kina Hamid Ameir waliofanikisha mapinduzi ya Januari 1964.

Wakati Ali Ameir, aliyefikia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar mbali na kuwa waziri katika serikali zote mbili, anaendelea kuchechemea kiafya baada ya kuumwa kiharusi hapo nyuma, Shamhuna aliaga dunia Mei mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu akiwa nyumbani kwake.

Balozi Seif na Dk. Khalid walisemekana kutopikika chungu kimoja baada ya Dk. Khalid kuwa na msimamo imara wa kusimamia matumizi ya fedha za serikali.

Wao walipigwa ‘gavana’ wakati yakiwepo majina kadhaa ya wanasiasa wanaotamani kuteuliwa wakiwemo wale wanaoonekana kumvutia Mwenyekiti Rais Magufuli.

Hawa ni pamoja na Profesa Makame Mbarawa, mbunge wa kuteuliwa anayeendelea kutumikia uwaziri baada ya kuteuliwa awali na Dk. Jakaya Kikwete kama waziri wa sayansi na teknolojia.

Profesa Mbarawa ni Mtanzania mwenye asili ya Wilaya ya Mkoani katika kijiji cha Mkanyageni kisiwani Pemba, karibu na nyumbani kwao Dk. Shein. Kwa sasa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, akiwa amebadilishwa kutoka Wizara ya Ujenzi alikoteuliwa katika serikali ya kwanza ya Rais Magufuli Disemba 2015.

Yupo pia Pereira Ame Silima, mtendaji katika Sekretariati ya CCM makao makuu. Huyu ni Mzanzibari kutokea kijiji cha Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye baada ya kutumikia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi wadhifa wa ukatibu mkuu, aligombea ubunge na akapata kuteuliwa miongoni mwa manaibu waziri wakati wa Dk. Kikwete.

Makada wengine wanaotajwa ni Dk. Hussein Mwinyi, mbunge wa Kwahani mjini Zanzibar na ambaye ni Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiendelea kubaki kwenye Baraza la Mawaziri kwa miaka tangu awamu ya Rais Jakaya Kikwete.

Daktari huyu wa binadamu ni mtoto wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, anatajwa kama mwanasiasa asiye na makeke (mtulivu) na ambaye anafanya vizuri jimboni. Wanaomjua vizuri baba yake, maarufu kama Mzee Mwinyi, wanasema huwa akitaja kuwa atajisikia vizuri akishuhudia mwanawe anabahatika.

Wengine ni Balozi Ali Abeid Karume, Waziri wa Vijana na Sanaa wa Zanzibar, mwenye uzoefu wa uongozi akiwa ametumikia ubalozi nchi za nje kwa miaka 22 mfululizo.

Anasemekana kutamani “mno” urais wa Zanzibar na mara kadhaa hujitokeza kama mtetezi wa sera ya Mapinduzi Daima inayopendwa na wanasiasa wahafidhina.

Wakati fulani baada ya kuzuka mgogoro wa kisiasa Zanzibar kulikotokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, Balozi Karume alisikika kwenye mahojiano na chombo cha habari nchini, akisema “CCM ndiyo chama pekee chenye haki ya kugombea urais Zanzibar; vyama vingine vishike tu viti vya uwakilishi.”

Vyanzo vya ndani ya chama chake vimepata kusema Balozi Karume ambaye ni mchumi, amewahi kukwaruzana na uongozi wa juu serikalini kwa msimamo wake wa kuipenda Zanzibar lakini akitamani kuongoza kwa misimamo mikali, mfano wa alivyokuwa Mzee Abeid Amani Karume, baba yake mzazi pamoja na Rais Mstaafu Amani Abeid Karume.

Katika orodha ya wanasiasa wanaotajwa kutamani urais Zanzibar, wamo pia wanawake wakiongozwa na Samia Suluhu Hassan, mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa umakamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akiwa ameshinda ubunge jimbo la nyumbani kwao Makunduchi, Samia aliteuliwa waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais.

Wanawake wengine ni Balozi Amina Salum Ali, mtaalamu wa masuala ya fedha na waziri mzoefu katika serikali Zanzibar ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita aliingia katika mbio za kusaka uteuzi ili agombee urais wa Tanzania.

Wakati wa mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma, alifikia nafasi ya wagombea watatu wa mwisho akiwa na January Makamba na aliyekuja kuchaguliwa Dk. Magufuli.

Balozi Amina alikuwa ametoka kutumikia taifa kwenye Umoja wa Mataifa, Marekani. Aliteuliwa baada ya kukosa urais wa Zanzibar mwaka 2010. Aliteuliwa Dk. Shein ambaye alikuja kutangazwa mshindi ndani ya kiwingu cha shutuma za uvurugaji matokeo.

Hata hivyo, ushindi wake uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ulisimama baada ya Maalim Seif Shariff Hamad kuridhia kupoteza kwa lengo la kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Saada Mkuya ni mwanamke mwingine katika orodha. Waziri wa zamani wa Fedha wa Tanzania, huyu anaendelea kuwa mbunge ambaye ametokea kuwa mtetezi mkubwa wa maslahi ya Zanzibar ndani ya mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Wakati hao ni wanasiasa wakongwe, wapo wachache katika wachanga wanatajwa kujijenga kwa kujaribu bahati. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni Yussuf ni mmoja wao.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!