Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Neno ‘uchochezi’ linavyotumika kuminya wapinzani
Makala & Uchambuzi

Neno ‘uchochezi’ linavyotumika kuminya wapinzani

Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema (wakwanza) kulia ni Wakili Fatma Karume, Mwanasheria wa kujitegemea
Spread the love

Na Rashid Abdallah

KILA nyakati huwa na mbwembwe zake. Nyakati za sasa katika uwanja wa siasa nazo zinazo. Ni mbwembwe nyingi; vituko vingi; mambo ya kuhuzunisha na mengine kufurahisha.

Neno “uchochezi” kwa siasa za zama hizi limegeuka kituko. Watawala hulitumia ili kunyamazisha yule wanayeamini anaisema kweli, ila haisemi kwa maslahi yao.

Ndo maana kesi za tuhuma za uchochezi hujazana mahakamani. Wanaokumbwa na kesi hizi wengi si haba hata kama uzoefu unaonesha nyingi yake hazisimami mahakamani. Zinatupwa kwa kukosekana ushahidi.

Pamoja na ukweli huo, kama unavoonekana kwa kesi za miaka mingi nyuma baada ya mageuzi mapya ya kidemokrasia – miaka ya 1990 – bado serekali kwa kutumia Jeshi la Polisi haijachoka kuimba kiitikio “uchochezi.”

Ni sehemu ya mkakati wa kisiasa wa chama tawala kudhoofisha upinzani. Watu wasiuamini. Basi wanamageuzi dhaifu watasita kusema. Watahofu kuhoji au kuikosoa serikali kwa makosa yake mbalimbali.

Katika hofu hii, kwa namna hali inavyokwenda, vyombo vya habari vimekutwa. Vyenyewe pamoja na waandishi wake wamo katika mtihani mkubwa. Kila wakati wanahojiwa na Polisi.

Wenye roho nyepesi wameanza kuogopa. Hawataki kuingizwa katika makarandinga na kupelekwa vituoni saa kadhaa ili kuhojiwa.

Uchochezi ni ngao kwa wakati wetu wa sasa kuilinda serekali, hutumika nguvu nyingi kuwashitaki watu lakini mahakama haiwapati na hatia yoyote.

Unaitwa kupitia bomba ufike mwenyewe – ujisalimishe – kujibu tuhuma za kufanya uchochezi. Nia yako? Unaambiwa unataka kuichonganisha serikali ichukiwe na wananchi. Au unataka kuhatarisha usalama wa nchi. Ukikakamaa baada ya mahojiano inaishia. Lakini yaweza kesi kwenda kwa miezi kadhaa unaripoti kituoni.

Mwanasheria Fatma Karume alipata kusema “inaonekana huyu anayetoa amri za watu kukamatwa kwa tuhuma za uchochezi, haelewi hata maana ya huo uchochezi.”

Wakili huyu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na binti wa Rais mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya sita (2000/2010), Amani Abeid Karume, alisema kesi hizi hata ukiuliza nani aliyechochewa, kachochewa kufanya nini na amevunja sheria ipi, wakamataji wanabaki kimya.

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania na miongoni mwa maulamaa wazoefu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, hivi karibuni alipewa siku tatu ajisalimishe Polisi.

Ni baada ya kutoka jijini Nairobi kumjuulia hali Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, anayeendelea kutibiwa nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 mchana kweupe mjini Dodoma.

Sheikh Ponda aliwaalika waandishi wa habari kueleza kile walichoteta na Lissu, pia kama Mtanzania kutoa maoni yake kuhusu kadhia iliyomkuta. Vyombo vya usalama vilijipanga kumzuia kuhutubia waandishi wa habari. Alihutubia na kuwatoroka polisi. Wakashikwa waandishi waliohudhuria.

Askari wanatoka mbio na magwanda yao kumkamata Sheikh Ponda ambaye hata alichokisema hakijatangazwa. Badala yake, wanakamatwa maripota na wapigapicha.

Ndipo yeye akatangazwa kwa bomba kuwa ajisalimishe Polisi, si hivyo atakiona cha mtema kuni.

Ni kanchi fulani ambako “kana mambo ya ajabu ajabu” na vikosi vyake navyo hutumikia amri ambazo nyingi yake hazifikiriki katika nchi ya kidemokrasia.

Profesa Abdallah Safari alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha habari Oktoba 13 iliyopita, kuhusiana na “uchochezi” alisema, “ukweli sio uchochezi, kuikosoa serikali kwa lengo la kuwataka warekebishe vilevile sio uchochezi.”

Kwa asiyeelewa, kuzungumza jambo la ukweli si uchochezi wala kuikosoa serikali ili ijisahihishe kiutendaji, nako hakuwezi kuhesabiwa kuwa ni uchochezi.

Mtu aliyetoka Nairobi kumkagua Lissu na kutaka kuzungumza na umma wa Watanzania kupitia vyombo vya habari kuhusu safari yake hiyo, unamuita mchochezi. Ni kituko kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayolinda haki ya raia kujieleza.

Au mtu anasimama jukwaani kulalamika kadhia ya kukutwa maiti holela ufukwe wa Coco Beach, na kusihi serikali uchunguze kwa kina na kuleta majibu kwa umma, anaambiwa mchochezi. Ni mambo ya vituko na aibu.

Siku zote kesi za aina hii zinashindwa mahakamani. Kwanza kwa kukosekana tafsiri halisi ya uchochezi. Ni maneno gani yanashawishi uchochezi; ni nani anatafsiri uchochezi umefanyika hata mahakama ipelekewe ushahidi na kuridhika mtuhumiwa amevunja sheria. Hapa pangali na utata.

Ndiyo yale maswali ya Fatma Karume kwa mapolisi walioshika watu kwa tuhuma za uchochezi. Nani amechochewa, kufanya nini na kosa liko wapi. Akasema, “hawaelewi nini maana ya uchochezi.”

Lissu anakabiliwa na kesi nyingi za staili hii. Ni maarufu kukosoa ya serikali. Awe ndani au nje ya bunge. Na anaposema hahofu chochote kwa sababu anaelewa kisheria hatendi kosa lolote.

Unaona kuwa nyuma ya pazia hili la uchochezi linalowafunika watu wengi hasa wale wenye uthubutu na ujasiri wa kuhoji yanayoihusu serikali, siasa za majitaka zinazidi kutumika ili utawala kuzuia upinzani.

Hata kule kuikosoa serekali ambako kumefanywa sana na Tundu Lissu ndiko kulikomfanya kutwishwa kesi lukuki za uchochezi, bahati mbaya kwa hao wanaotuhumu ni kuwa hadi Lissu anapigwa risasi hawakumpata na hatia.

Tegemea kuona vioja vingi katika siasa hizi ambazo nimewahi kuzisema bado hazijastaarabika na zina safari ndefu hadi kufikia katika bustani ya waliostaarabika.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu

Spread the loveGEORGE Francis anasikitika; anatembea akiwa na mawazo mengi, hajui la...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita

Spread the loveWAKATI naandaa makala ya safu hii wiki hii, nimejikuta nakumbuka...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hakuna fedha za Rais

Spread the loveKUNA mambo machache mazuri ya kujifunza kutoka kwa Margaret Thatcher,...

Makala & UchambuziMichezo

TFF kuamua hatima ya Amrouche

Spread the loveHATIMA ya Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Adel Amrouche kuendelea...

error: Content is protected !!