June 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NEC yazungumzia kura feki zilizokamatwa 

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), imesema haijapokea taarifa rasmi ya kukamatwa kwa masanduku ya kura yenye kura za kughushi ‘feki’. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage amesema hyo leo Jumatano jioni tarehe 28 Oktoba 2020 wakati anazungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Jaji Kaijage amesema, NEC haijathibitisha taarifa hizo na kwamba wananchi wazipuuze.

“Kuna taarifa ya kuwepo masanduku ya kura feki katika Jimbo la Buhigwe, Kawe na Pangani, taarifa hizo hazijathibitishwa na hazijawasilishwa rasmi kwa tume.”

“NEC inataka wananchi wapuuze taarifa hizo kwa kuwa hazijathibitishwa. Tume inaendelea kufuatilia zoezi hilo nchi nzima,” amesema Jaji Kaijage.

Mapema leo asubuhi, Mgombea Ubunge wa Kawe kupitia Chadema, Halima Mdee alidai uwepo wa kura feki katika moja ya kituo jimboni humo, hali iliyoibua mvutano na kusababisha kukamatwa na polisi kwa mahojiano kisha kuachiwa.

Halima Mdee, Mgombea ubunge Kawe kwa tiketi ya Chadema akikwaruzana na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo

Katika mitandao mbalimbali ya kijamii, kuna video inasambaa ikionyesha baadhi ya wananchi wa Kawe wakichoma moto karatasi za kura zilizokuwa zimepigwa ambazo walidai wamezikamata kwa mmoja wa wananchi.

Huko Kigoma Mjini, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Zitto Kabwe amesema, wamekamata karasi za kura zikiwa zimepigwa.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Zitto ameandika “Tumekamata kura ambazo zimeshapigwa katika Jimbo langu la Uchaguzi. Tutazuia kila mbinu yao chafu. Kila mbinu yao chafu.”

“Hii ni sehemu ya karatasi za kura ambazo tumezikamata katika Kata ya Kasingirima Jimbo la Kigoma Mjini zikiwa zimeshapigwa. Walikuwa wanajaribu kuziingiza kwenye vituo. Katika Kata hii tumekamata Begi zima limejaa Kura,” ameandika Zitto na kuambatanisha picha za karatasi za kura.

Wengine waliolalamikia kura feki ni wagombea ubunge wa Kinondoni, Saed Kubenea wa ACT-Wazalendo na Mustafa Muro wa NCCR-Mageuzi waliodai kwamba kuna kura zimeingizwa kinyemela vituoni.

error: Content is protected !!