Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Tangulizi NEC yamkabidhi cheti Magufuli, kuapishwa Dodoma
Tangulizi

NEC yamkabidhi cheti Magufuli, kuapishwa Dodoma

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemkabidhi cheti cha ushindi Rais mteule wa Tanzania, John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Pia, mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan naye amekabidhiwa cheti cha ushindi.

Shughuli hiyo imefanyika leo Jumapili tarehe 1 Novemba 2020 ofisi za NEC zilizopo Njedegwa jijini Dodoma.

Viongozi mbalimbali wa kiserikali, dini na kisiasa wamehudhulia hafla hiyo ikiwemo wagombea urais tisa kati ya 15 waliochuana na Dk. Magufuli katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020.

Baadhi ya wagombea hao waliohudhuria ni; Yeremea Maganja (NCCR-Mageuzi), Cecilia Mwanga (Demokrasia Makini), Queen Sendiga (ADC), Muttamwega Mgaya (SAU), John Shibuda (Ade Tadea) na Leopard Mahona (NRA)

Wengine ni; Twalib Kadege (UPDP), Seif Maalim Seif (AAFP), Philip Fumbo (DP) na Khalifan Mazurui wa UMD.

Wagombea ambao hawakuhudhulia hafla hiyo ni; Bernard Membe (ACT-Wazalendo), Hashim Rungwe (Chaumma), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Tundu Lissu wa Chadema.

Dk. Magufuli amekabidhiwa cheti hicho na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage ambaye tarehe 30 Oktoba 2020, alintangaza mshindi wa uchaguzi mkuu.

Dk. Magufuli ambaye ataongoza kwa muhula wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, aliibuka wa kura milioni 12.5 kati ya milioni 15.9.

Akitangaza matokeo tarehe 30 Oktoba 2020, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage alisema waliojiandilisha kupiga kura walikuwa milioni 29.Alisema, waliopiga kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 walikuwa milioni 15.9.

 

Jaji Kaijage alisema, kura halali zilikuwa milioni 14.8.

Tundu Lissu wa Chadema alipata kura milioni 1.9.

Dk. Magufuli anatarajia kuapishwa Alhamisi tarehe 5 Novemba 2020 katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma kunalizia ungwe yake ya miaka kumi kwa mujibu wa Katiba.

 

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kuapishwa Dodoma kwani mara zote watangulizi wake, waliapishwa Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) jijini Dar es Salaam.

Pia, Dk. Magufuli katika awamu yake ya kwanza, aliapishwa Uwanja wa Uhuru tarehe 5 Novemba 2015 akipokea kijiti kutoka kwa Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete.

Taarifa ya NEC

Kabla ya kukabidhi cheti hicho, akitoa taarifa ya uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera amesema, uchaguzi huo ulihusisha majimbo 264, kati ya hayo 214 Tanzania Bara na 50 Zanzibar.

Dk. Mahera amesema, kulikuwa na Kata 3956 “kata nne hawakufanya uchaguzi, kata tatu wagombea walifariki na kata moja haikufanya kutokana na changamoto siku ya uchaguzi.”

Amesema, kila chama kilichopata angalau asilimia tano ya kura halali za wabunge kitakuwa na fursa ya kupata wabunge wa viti maalum.

Semistocles Kaijage, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC)

Dk. Mahera amesema, mwaka huu kumekuwa na ongezeko la wagombea urais 17 waliojitokeza kuwania urais na 15 waliteuliwa kuwania urais wakiwemo wagombea wawili wanawake.

“Tume imefanikiwa kutangaza matokeo ya urais ndani ya saa 48 kutokana na mtandao uliojengwa na Watanzania,” amesema Dk. Mahera

Katika uchaguzi mkuu uliomwingiza magufuli madarakani mwaka 2015, Dk. Magufuli alipata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46 huku mshindani wake, Edward Lowassa wa Chadema alipata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97

…tupo tayari kushirikiana.

Akizungumza kwa niaba ya wagombea wenzake wa urais, Queen Sendiga wa ADV amempongeza Rais mteule wa Tanzania, John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi.

“Uchaguzi umemalizika, hata wanaotumia nguvu na ngumi kupigana, refa akipiga filimbi ya mchezo kumalizika, mshindi anakuwa amepatikana. Uchaguzi umemalizika, turudi kuijenge nchi yetu.”

“Sisi tupo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwako Rais mteule. Lakini, tumeona Watanzania wanataka maisha bora na maendeleo. Tuitunze amani yetu ili kupata maendeleo tunayoipata,” amesema Queen

Ametumia fursa hiyo, kufikisha ombi la vyama visivyokuwa na wabunge bungeni kupata ruzuku japo kidogo ili kuwawezesha kufanya shughuli za kisiasa.

Qeen Cuthbert Sendiga- aliyekuwa mgombea urais 2020 kupitia ADC

Naye Leopord Mahona wa NRA amewashukuru Watanzania wote “kwa kunifanya kuwa historia kwanza. Nawashukuru kwa kura zao kwangu.”

Mahona amesema, “nampongeza sana Mzee wangu Dk. John Pombe Magufuli kwa ushindi mkubwa alioupata. Mimi nikiwa mgombea mdogo kuliko wote, niko tayari kufanya kazi na yeye.”

Uchaguzi umefanyika kwa haki

Mwakilishi wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais mstaafu wa Burundi, Sylvester Ntibantunganya ameanza kwa kumpongeza Dk. Magufuli kwa ushindi alioupata.

Amesema, wamepitia maeneo mbalimbali nchini kuangalia kuhusu uchaguzi huo na kuona uchaguzi umefanyika kwa amani, umoja na “tutumie nafasi hii kuwapongeza watu wote na vyama vya siasa, vilivyoshiriki uchaguzi huu kwa kutunza amani.”

Rais mstaafu wa Burundi, Sylvester Ntibantunganya

“Bila amani, pasipo usalama na pasipo uchaguzi huru na haki hakuna matokeo. Kwa tuliyoyaona, tunaweza kusema uchaguzi ulikuwa umepangwa kuendeshwa vizuri sana na tunawapongeza kwa kuwa na uchaguzi mzuri sana,” amesema Rais huyo mstaafu Ntibantunganya

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!