January 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ndugai achaguliwa Spika wa Bunge 

Job Ndugai, Spika wa Bunge la 12 la Tanzania

Spread the love

JOB Ndugai, amechaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea)

Uchaguzi wa Spika, umefanyika leo Jumanne tarehe 10 Novemba 2020 bungeni jijini Dodoma katika Kikao cha kwanza, Mkutano wa kwanza wa Bunge la 12.

Mkutano huo wa uchaguzi, umesimamiwa na Mwenyekiti wa muda, William Lukuvi ambaye ni mbunge mteule wa Ismani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema, kura 345 zilipigwa, na Ndugai ameshinda kwa kupata kura 344 huku kura moja ya hapana, hivyo kuibuka kwa ushindi wa asilimia 99.7.

Baada ya kumaliza kutangazwa matokeo hayo, Ndugai aliapishwa na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai.

Kiapo cha Utii;

“Mimi, ………………. naapa kwamba, nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba, nitaihifadhi, nitailinda na kuitetea Katiba ya Tanzania kwa mujibu wa Sheria iliyowekwa. Ewe Mwenyezi Mungu, nisaidie.”

Kiapo cha Spika; 

“Mimi,…………., naapa kwamba, nitaitumikia vyema na kwa moyo thabiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kazi zangu kama Spika wa Bunge, na katika kutimiza wajibu wa cheo hicho nitawatendea haki watu wote kwa mujibu wa Katiba, Kanuni za Bunge na Sheria, Mila na Desturi za Jamhuri ya Muungano na kwa vyovyote vile sitatoa siri za Bunge. Ewe Mwenyezi Mungu, nisaidie.”

Spika Job Ndugai akiapa

Alipomaliza kuapishwa, Mwenyekiti wa kikao hicho cha uchaguzi, William Lukuvu alimweleza Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa, kwenda kuvaa joho la uspika ili kuanza kuendesha shughuli za Bunge ikiwemo kuapisha wabunge.

“Tumempata Spika ambaye amepita kwa rekodi ambayo haijaweza kupatikana. Nawashukuru sana waheshimiwa wabunge kwa kumaliza uchaguzi,” amesema Lukuvi

Mara baada ya Spika Ndugai kuingia, amesema “kazi inaanza. Wimbo wa Taifa” ulioimbwa na kwanza ya Bunge pamoja na wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Ndugai alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo. Katika Bunge la 11 lililomaliza muda wake, Ndugai alikuwa Spika wa Bunge hilo.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI TV na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!