Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ndesamburo mwingine aondoka Moshi
Habari za SiasaTangulizi

Ndesamburo mwingine aondoka Moshi

Mwili wa Marehemu Hawa Mushi, diwani wa Chadema katika kata ya Mawenzi ukipelekwa makaburini tayari kwa mazishi yake
Spread the love

HAWA Mushi, diwani wa Chadema katika kata ya Mawenzi, katika halmashauri ya Manispaa ya Moshi, hatimaye amezikwa mchana huu, nyumbani kwake Mawenzi. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Moshi … (endelea).

Hawa alifariki dunia juzi Alhamisi, katika hospitali ya Rufaa inayomilikiwa na Kanisa la Kilutheli Tanzania (KCMC), mkoani Kilimanjaro. Alikuwa anasumbuliwa na vidonda vya tumbo na uvimbe kwenye kizazi.

Mazishi ya mwanasiasa huyo mashuhuri jijini Moshi, yalihudhuriwa na mamia ya waombelezaji wakiongozwa na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wengine waliohudhuria msiba huo, ni meya wa manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, madiwani wa manispaa ya Moshi na mbunge wa Moshi Mjini, Jaffary Michael.

Wengine, ni Joseph Selasini, mbunge wa Rombo na kaimu mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro; mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na mbunge wa Viti Maalum mkoani Dar es Salaam, Suzana Lyimo.

Wengine waliokuwapo, ni Lucy Owenya na Grace Kiwelu, ambao ni wabunge wa Viti Maalum mkoani Kilimanjaro.

Kifo cha Hawa kimekuja mwaka mmoja tangu chama hicho kimpoteze mmoja wa waasisi wake na nguzo yake kuu mkoani humo, Philemon Ndesamburo.

Ndesamburo alikuwa mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo kati ya mwaka 2000 hadi 2015, alipoamua mwenyewe kustaafu.

Alifariki dunia ghafla, tarehe 31 Mei mwaka jana mara alipofikishwa kwenye hospitali ya KCMC kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mbali ya kuwa mbunge na mwasisi wa Chadema, Ndesamburo alikuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Kilimanjaro na mmoja wa wafadhili wakuu wa Chadema.

MwanaHALISI Online, limezunguma na baadhi ya waombolezaji na kusema, Hawa alikuwa nguzo muhimu ya Chadema katika manispaa ya Moshi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

“Katika kipindi cha uhai wake, diwani Hawa alikuwa mstari wa mbele kupigania maendeleo ya wananchi wa kata yake na Manispaa ya Moshi kwa ujumla,” anaeleza Janeth Mbambo, mkazi wa Mawenzi.

Anasema, “Mama huyu alikuwa mstari wa mbele katika kupingania manispaa ya Moshi kuwa jiji. Hakuwa mbaguzi. Alishirikiana na kila mmoja katika kuhakikisha Moshi inapata maendeleo.

“Hapa petu alihamasiha uanzishwaji wa ulinzi wa Sungusungu kwa lengo la kupambana na uhalifu. Alianzisha na kusimamia operesheni ya kuondoa changudoa. Ni bahati mbaya sana kwamba amefariki dunia kabla ya kumaliza kazi ambayo alikuwa anaisimamia.”

Naye mbunge wa Moshi Mjini, Jafar Michael, akimzungumzia marehemu anasema, “tumempoteza mpiganaji kwa kweli ndani ya Chadema. Tumempoteza mwanamke shupavu na jasiri. Tumempoteza mpambanaji mahiri na thabiti.”

Anasema, “…mheshimiwa Hawa Mushi, alikuwa akitetea maamuzi ya chama na baraza bila woga. Hakika, tumempoteza kiongozi. Tumepoteza mmoja wa nguzo yetu.”

Akiongea huku chozi likimtililika, Jafar anasema, “ni kweli kuwa kifo kimeumbwa na hivyo hatupaswi kulalamika. Lakini kifo cha Hawa kimeacha pengo kubwa kwa chama chetu na manispaa yetu.”

Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema, amemueleza marehemu Hawa kuwa alikuwa “jembe lisilohitaji mpini kulifanyia kazi.”

Alisema, “tumeondokewa. Hawa alikuwa jembe na alifanya kazi zake bila kusimamiwa. Kwa kweli alikuwa kiongozi wa kuigwa.”

Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa mjini Moshi wanasema, ukiacha tofauti ya uwezo wa kiuchumi na umashuhuri, diwani huyo anaweza kuwa mtu wa pili kufananishwa na marehemu Ndesamburo kwa kuwa karibu na wananchi.

Mwingine ambaye anatajwa kuwa karibu na wananchi ni mbunge wa jimbo hilo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!