MSANII nyota wa filamu nchini Tanzania, Jafari Makatu maarufu kwa jina la Mzee Chumo, amewataka waandaaji wa filamu kuacha kuzima vipaji vichanga vya wasanii kwa kuendekeza ubaguzi. Anaripoti Hamis Mguta…(endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Online nyota huyo anayewika kwenye thamthilia ya Huba amesema kuwa, kitendo hicho kimekuwa kikiua vipaji vya wasanii wachanga kutokana na kutopata nafasi ya kuonesha vipaji vyao.
“Watu wanafanya hivyo lakini sio sahihi kwasababu unawanyima haki wasanii wanaokuja. Hawa wapya wana wana vionjo vya kipekee na wana hamu ya kuonekana na kuweka majina yao kwenye kiwango cha juu, hivyo wanakuja na mtindo mwingine ambao unamfanya mtazamaji apende,” amesema.
Mzee Chumo amesema kuwa, makosa mengi yanatokana na waandishi na waongozaji wa filamu kutokana na watu kuwa waongozaji hata kama wakiwa hawafahamu maana halisi ya uongozaji.
Mwigizaji huyu aliwahi kufanya kazi hizo na marehemu Sharo Milionea, Yusuph Mlela pamoja na Jokate Mwegelo ambaye kwasasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.
“Mtu akicheza filamu tatu tu anakuja na yeye anakuwa muongozaji (Director), lakini hajui majukumu ya muongozaji na wala hajui muongozaji ni mtu wa aina gani,” amesema.
Leave a comment