Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mwambe, Katani wazungumzia maisha ya upinzani
Habari za Siasa

Mwambe, Katani wazungumzia maisha ya upinzani

Spread the love

WAGOMBEA ubunge wawili wa Mkoa wa Mtwara waliotoka vyama vya upinzani na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameeleza machungu waliyokuwa wakikumbana nayo wakati wakitaka kuwatumikia wananchi wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mtwara … (endelea).

Wabunge hao Cecil Mwambe (Ndanda) na Katani Ahmed Katani (Tandahimba) ambao wamehamia CCM kwenye kinyang’anyiro hiki cha ubunge, wamewaonya wakazi wa Masasi wasifanye makosa ya kuchagua wagombea wa upinzani kwani wataendelea kukosa maendeleo.

Wametoa wito huo jana Jumatano tarehe 21 Oktoba 2020 kwenye mkutano wa kuwanadi wagombea ubunge na udiwani wa CCM uliofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba kata ya Mkuti, wilayani Masasi, mkoani Mtwara ambako Mjumbe wa Kamati Kuu CCM, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.

Mwambe anayegombea Ndanda, ambaye alihamia CCM akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alichojiunga nacho mwaka 2015 akitokea CCM, alisema licha ya kuwa alikuwa akitamani wananchi wake wapate huduma muhimu kama maji, afya na barabara, haikuwa rahisi kwake kuchangia bajeti ya maendeleo kwa sababu walikuwa wanakatazwa.

“Mambo yaliyokuwa yanafanyika huku Masasi hata sisi kule Ndanda tulikuwa tunayatamani. Hii ni kwa sababu hakuna cha maana kule kilichoandikwa kwa ajili yenu, na mimi ni shahidi. Katika miaka mitano ya ubunge wangu, sijawahi kuitikia ndio na madhara yake nimeyaona. Ninawaomba sana, msifanye makosa hayo,” alisema.

Naye Katani anayegombea Tandahimba, ambaye alihamia CCM akitokea Chama cha Wananchi (CUF), aliwataka wananchi hao wasifanye makosa kwa sababu kule alikokuwa hawana ilani.

“Kama Katani anayeongea hapa mbele yenu, alikuwa Mwenyekiti wa Vijana Taifa na kaikimbia CUF, wewe ni nani mwananchi wa Masasi hata upinge maendeleo ya nchi hii? Tena niwaambie, kule hakuna ilani. Nawaomba wana Masasi msifanye makosa ya kuchagua wagombea wa upinzani, sisi wenzenu tumeyaona tukiwa Bungeni.”

“Ukienda Bungeni kutaka kusema Masasi tuna shida ya umeme, wakubwa wanasema kapinge bajeti. Tutaupataje umeme? Tumekwenda Bungeni tumepiga plasta, sasa ukitaka kuomba umeme, utaongea vipi na wewe midomo umeifunga plasta,” alihoji Katani

“Wana Masasi msitucheleweshe, hii gari ya Dkt. Magufuli inatelemka kwa kasi kuleta maendeleo huku mikoa ya Kusini. Acheni Geofrey Mwambe awe mbunge wa jimbo la Masasi, alete maendeleo,” alisisitiza.

Mapema, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Masasi, Rashid Chuachua alisema katika wilaya hiyo, ndani ya miaka mitano, waliwezaa kujenga madarasa 108 ya shule za sekondari na mengine 355 ya shule za misngi.

Alisema kiasi cha Sh.3.5 bilioni kilitolewa kwa ajili ya elimumsingi bila malipo huku sekta ya afya ikiboreshwa kwa kujenga kituo cha afya cha Mbonde kwa gharama ya Sh.500 milioni na hospitali ya Mkomaindo ikipatiwa jengo la upasuaji lililogharimu Sh.228 milioni.

“Mradi wa maji unaendelea kujengwa na ukikamilika, hatutakuwa na shida kabisa ya maji hapa Masasi,” alisema na kuwaombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Masasi, Bw. Geofrey Mwambe; na wagombea udiwani 14 wa CCM wa jimbo la Masasi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!