June 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwambe amponza Spika Ndugai, washtakiwa

Spread the love

JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri na Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda aliyejiengua Chadema, wameshtakiwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Wameshtakiwa kwa madai ya kuvunja Katiba ya Jamhuri. Mwingine aliyeunganishwa kwenye mashata hayo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kesi hiyo imefunguliwa na Shirika la Uraia na Msaada wa sheria (CILAO), leo tarehe 20 Mei 2020 kupitia wakili wake John Seko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Odera Odero, Mkurugenzi wa CILAO, wamefungua shauri baada ya kupata maoni ya Watanzania 3000 waliopinga kitendo cha Spika Ndugai kumrejesha bungeni Mwambe.

Mwambe alikuwa mbunge kupitia Chadema ambapo tarehe 15,Februari 2020, alijiuzulu na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, Spika Ndugai alimrejesha bungeni licha ya kujivua uanachama wa Chadema.

Shirika hilo linaiomba mahakama kutoa tafsiri juu ya kitendo cha kumruhusu Mwambe kuhudhuria vikao vya Bunge kama mbunge baada ya kujiuzulu.

Odero ameeleza, kwa mujibu wa Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, inatoa wajibu wa kila raia kuitii Katiba pamoja na Sheria za Jamhuri ya Muungano.

Spika Job Ndugai

“Spika wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ndanda, Cecil Mwambe wanawajibu pia wa kuitii Katiba ikiwemo Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba pamoja na kifungu namba 6C(2) na 6C(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 288 Toleo la Mwaka 2002].”

Amefafanua kuwa Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba na kifungu namba 6C(2) na 6C(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa {Sura ya 288} Toleo la Mwaka 2002], Mbunge atakoma kuwa mbunge endapo atajihuzuru nafasi yake ya ubunge na kuhamia chama kingine kama ambavyo Mwambe alijiuzulu.

Odero amedai, spika alishathibitisha kujiuzulu kwa Mwambe na alitoa maagizo ya kusitishwa mshara wake baada ya tarehe 15 Februari 2020.

Spika Ndugai alitangaza bungeni kuwa, hajaridhwa na barua iliyoandikwa na John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema kumtaarifu ukomo wa ubunge wa Mwambe.

Pia Spika Ndugai alieleza, hajapokea barua ya Mwambe ya kujivua uanachama wa Chadema na kujiuzulu ubunge wake na kwamba, barua ya Mnyika haina maana yoyote.

error: Content is protected !!