Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mwaka 2020 Nenda mwana kwenda – 1
Habari za Siasa

Mwaka 2020 Nenda mwana kwenda – 1

Spread the love

MWAKA 2020 uondoke na usirejee tena, kutokana na jinsi ulivyoacha maumivu, malalamiko, uharibifu na kugharimu maisha ya baadhi ya watu. Anaandika Mwandishi Wetu…(endelea).

Ni mwaka ambao tumeshuhudia matukio tuliyokuwa tukiyasikia ama kuyasoma kutoka mataifa mengine.

Ni mwaka ulioonesha thamani ya matokeo ya demokrasia ya kweli na kinyume chake. Ni mwaka uliojaa machungu.

Ni mwaka wa neema kwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuwa mshidi wa urais Visiwani.

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Ni mwaka ambao kulihitajika ujasiri na uzalendo wa kuirejesha Zanzibar, katika amani, umoja na mshikamano, kufuatia kile kinachodaiwa kimetokea kwenye uchaguzi mkuu uliomuingiza Dk. Mwinyi madarakani.

Katika uchaguzi huo, uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba, upinzani ukiongozwa na aliyekuwa mgombea wake, Maalim Seif Sharif Hamad, ulikuwa ukilalamikia kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu, sheria na upendeleo wa vyombo vya dola kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), dhidi ya upinzani.

Ni mwaka ambao, bila busara na hekima za Maalim Seif, pengine leo tungekuwa tunajadi tofauti kuhusu Zanzibar. Lakini busara hizo, ndizo zimesaidia kufanikisha umoja na mshikamano na kuangaza amani ya visiwa hivyo kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKI).

Aidha, mwaka 2020, hautasahauliwa na washikadau na wananchi wengine, kutokana na kubeba matokeo ya uchaguzi yasiyotarajiwa na wengi. Ikumbukwe kuwa uchaguzi mkuu uliyopita, ni kama umerejesha mfumo wa chama kimoja nchini.

Hata sekta ya habari na utangazaji, iliguswa katika mwaka huu. Ni pale Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), liliponja machungu ya Chadema, kwa kuamriwa kuondoka kwenye mkutano wake wa kampeni, uliofanyika katika viwanja vya Zakiem, Mbagala jijini Dar es Salaam.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Viongozi wa Chadema, wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, waliamuru TBC kufunga mitambo yao na kubeba kila walichonacho kuondoka kwenye mkutano huo. Madai ya Mbowe, ni kuwa TBC imekuwa idara ya parapaganda ya chama tawala, badala ya kuwa chombo cha umma.

Mbowe alichukua maamuzi hayo, baada ya kubaini kuwa chombo hicho cha umma, kilikuwa kinahariri, “kwa nia ovu,” baadhi ya taarifa zake ilizokuwa inazirusha kutoka kwenye mkutano wake huo.

Katika tukio hilo, wafanyakazi wa TBC walijikuta kwenye wakati mgumu wa kuondoka katika viwanja hivyo, huku wakizungukwa na maofisa wa polisi kulinda usalama wao.

Pamoja na kufanikiwa kuondoka wakiwa salama, lakini bado hawataisahau siku hiyo, kutokana na kuzongwa na baadhi ya wafuasi wa Chadema na wapinzani wa TBC.

Kutokana na kadhia hiyo, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), lilijaribu kujitutumua kuwaleta pamoja uongozi wa TBC na Chadema, ili kumaliza walichoita, “tofauti zao,” na hatimaye kushikana mikono.

Chadema walitumia mkutano huo, kueleza machungu na mikakati ya kukabili vitisho vya demokrasia baada ya wagombea wake ngazi ya ubunge na udiwani kutemwa.

Mwaka 2020 ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani. Lakini tofauti na miaka ya nyuma ya uchaguzi, mwaka huu, baadhi ya vyama vya siasa, vililazimika kubadili utamaduni wao wa kufungulia kampeni jijini Dar es Salaam.

Kwa mfano, Chama cha ACT-Wazalendo, kilianza safari yake ya uchaguzi mkuu, mkoani Lindi, huku CCM wakianzia mkoani Dodoma.

Hapa ndipo wakazi wa Lindi walipokuwa wakwanza kumuona kijana wao, Bernard Kamilius Membe, akianza safari za kutafuta kuingia Ikulu kutokea nyumbani kwao. Membe ni mzaliwa kutoka katika kijiji cha Rondo-Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi.

Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,

Ni mwaka pia uliokusanya Wagogo na wageni wengine katika jiji la Dodoma, kumshudia mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli, akikaribishwa na watani zake, katika uwanja wa Jamhuri, kumpa baraka za kurejea tena Ikulu.

Kwenye uzinduzi huo, tulipata kujua ‘tabia’ ya wabunge wa upinzani iliyoelezwa na Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri.

Spika Ndugai amedai kuwa kazi ya upinzani ni kususa bungeni’ na kusisitiza kwamba wabunge hao ni mali ya vyama hivyo, badala kuwa mali ya wananchi.

Kile ambacho Spika Ndugai hakueleza, ni kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, hakuna mbunge ambaye hatokani na chama siasa. Kwa maneno mengine, mbunge awe kutoka upinzani au CCM, ni sharti aidhinishwe  na chama cha siasa

Si hivyo tu. Ni mwaka ambao kwa mara ya kwanza, Dk. Bashiru Ali, katibu mkuu wa CCM, aliweza kuhutubia ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mkuu na kushusha lundo la tambo, kwamba chama chake, kimewasha mitambo, huku akivitahadharisha  vyama vya upinzani, kuwa “kutolaumiana.”

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Vyama vya upinzani havikutambua ni mitambo ipi hiyo, badala yake, uchaguzi ulipomalizika, upinzani uliondoka kapa. Kweli, mwaka 2020 ulijaa mafumbo.

Ni mwaka 2020 ulioshuhudia wanasiasa wa upinzani wakishushwa jukwaani na kupewa likizo ya kampeni bila kutarajia.

Kwenye kalenda ya matukio ya uchaguzi mkuu 2020, aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu, anayo rekodi ya kuondolewa kwenye uwanja wa mapambano kwa siku saba baada ya tarehe 2 Oktoba 2020. Alisimisha kampeni na inayoitwa, “Kamati ya Maadili ya Taifa ya Tume ya Uchaguzi.”

Naye Maalim Seif, alionja ngebe ya ZEC kwa kuingizwa jela ya siku tano kwa madai ya kulalamikiwa na chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) na CCM kuhamasisha wananchi kupiga kura ya mapema, tarehe 27 Oktoba badala ya tarehe 28 Oktoba.

Mwaka 2020 haukumuacha salama Saed Kubenea, aliyekuwa mbunge wa Ubungo na mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni, kupitia ACT-Wazalendo. Huyu alikumbana na mikosi miwili.

Kwanza, alikamatwa mkoani Arusha akituhumiwa kuingia nchini bila kupitia idara ha uhamiaji na bila kueleza kiasi cha fedha alichonacho.

Pili, alisimamishwa na Kamati ya Maadili jimbo la Kinondoni, kufanya kampeni kwa muda wa siku saba.

Kweli mwaka 2020 ulileta mambo mapya kwenye masikio yetu, kwamba mazuzu na waliofanya makossa, ni wagombea wa upinzani pekee. Hahahaaaa mwaka 2020 tuache tupumzike.

Hadi kwenye maisha yetu binafsi mwaka 2020 ulituingilia, uliamua kutengenisha maisha tuliyoyazoea kimtandao. Ni mwaka mbao wananchi waliminywa haki yao ya kupashana habari kupitia mitandao ya kijamii.

Ni mwaka huu, ulionyima uhuru na kutoa fursa kwa waminyaji kutekeleza matakwa ya hisia zao bila kujali haki ya msingi iliyopo kwenye Ibara ya 18 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatukuwahi kushuhudiwa dhuluma ya mawasiliano kama tulivyosoma na kusikia nchi jirani ya Burundi wakati wa uchaguzi mkuu wao, lakini katika hili mwaka 2020 umetuacha na kumbukumbu hasi

Tulistaajabu yaliyoendelea Burundi na kusahau ule usemi usemao ‘mwenzio akinyolewa nawe tia maji,’ hakika 2020 imetu fundisha maana halisi ya msemo huo.

Itaendelea…

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!