July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Muswada unaoweka kinga viongozi wakuu kushtakiwa watua bungeni

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof. Adelardus Kilangi

Spread the love

MUSWADA  wa wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2020 umewasilishwa bungeni ukipendekeza kufanyika marekebisho ya sheria 13 ikiwemo inayoweka masharti ya viongozi wakuu kushtakiwa mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Muswada huo umewasilishwa bungeni jijini Dodoma leo Jumatano tarehe 10 Juni 2020 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG), Profesa Adelardus Kilangi.

Amesema, katika Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, Sura ya 3, Muswada unalenga kufanya marekebisho katika Kifungu cha 4 ili kuweka masharti yatakayotaka mtu yoyote anayekusudia kufungua shauri lolote la kikatiba chini ya Ibara za 12-29 zinazohusu haki za msingi kuidhihirishia mahakama ni kwa kiasi gani mlalamikaji ameathiriwa na ukiukwaji wa haki anayolalamikia.

“Lengo la marekebisho hayo ni kuhakikisha utekelezaji wa masharti ya Ibara hizo unazingatia matakwa ya Ibara ya 30(3).”

“Aidha, marekebisho katika kifungu hiki yanapendekeza mashauri yote ya madai dhidi ya viongozi wakuu wa nchi yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema Profesa Kilangi

Amesema, “Lengo la marekebisho haya ni kukidhi maudhui ya dhana ya kinga ya mashtaka dhidi ya viongozi hao.”

Baadhi ya viongozi hao wanaolengwa na marekebisho hayo ni; Rais, Jaji Mkuu, Spika wa Bunge, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

 

Muswada huo umewasilishwa huku wadau mbalimbali wa utetezi wa masuala ya haki za binadamu wakiupinga kwamba unalenga kuzuia ufunguaji wa malalamiko mahakamani dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu pindi utakapokuwa ukifanyika.

Maoni ya Kamati

Akiwasilisha maoni ya kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa amesema, walipokea maoni mbalimbali kutoka kwa Umoja wa AZAKI (CSOs) 220 kupitia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC);  Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na TWAWEZA iliyowasilisha Maoni ya Wadau 210.

Amesema, Kamati ilipitia na kufanya uchambuzi wa Sehemu Kumi na Nne (14) za Musawada zenye jumla ya Ibara Hamsini na Moja (51) pamoja na vifungu vyote vya Sheria vinavyopendekezwa kurekebishwa.

Rais John Magufuli akiteta jambo na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma

Mchengerwa amesema, kutokana na uchambuzi wa Muswada uliofanywa na Kamati, kwa kupitia Ibara zote zinazopendekeza marekebisho katika Sheria Mama husika, kamati inapenda kutoa maoni kuwa, kwa ujumla maudhui ya Muswada huu yana tija kwa Taifa na endapo mapendekezo ya marekebisho yatapitishwa na kuwa sheria yatasaidia kuondoa mapungufu yaliyopo katika sheria hizo ili ziweze kuendana na hali halisi ya wakati huu.

“Hivyo, kamati imeridhia marekebisho yanayopendekezwa kwa kila Sheria inayorekebishwa katika Muswada huu, na inaipongeza Serikali kwa kubainisha upungufu katika sheria husika na kuandaa mapendekezo ya kuboresha yaliyowasilishwa katika muswada huu, na ambayo yameridhiwa na Kamati, pamoja na maoni ya kamati kwa baadhi ya vifungu vya sheria husika vyenye kuhitaji maboresho,” amesema.

Amesema, Ibara ya 7(b) inayopendekeza Marekebisho katika Kifungu cha 4 cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, Sura ya 3, “Uchambuzi wa kamati ulibaini, Ibara ya 7(b) ya Muswada inaweka masharti kwa maombi yanayowasilishwa mahakamani kulalamikia ukiukwaji wa Katiba katika Ibara ya 12 hadi 29 kuambatishwa na hati ya kiapo inayofafanua kwa kina athari ambazo mwasilisha maombi amezipata yeye binafsi.”

Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria

“Kamati iliitaka Serikali itoe ufafanuzi kuhusu mantiki ya matumizi ya maneno “has affected such person personally” sambamba na Mantiki ya Masharti ya Ibara ya 26(2) na 30 (3) za Katiba,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema, “Lengo la kamati ilikuwa ni kujiridhisha uzingatiaji wa masharti ya Ibara ya 26(2) na 30 (3) za Katiba zinazo toa haki na wajibu kwa mtu yeyote kuchukua hatua iwapo anaona Katiba inavunjwa.”

Mchengerwa amesema, uchambuzi wa kamati ulibaini, Ibara ya 26(2) ya Katiba inatoa masharti ya jumla kuhusu haki za binadamu na ulinzi wake.

Amesema, Ibara ya 30(3) ndiyo inatoa masharti mahsusi (enabling provisions) ya kuwezesha kutungwa kwa Sheria ambayo inaruhusu mtu ambaye anadai haki yake kuvunjwa kuweza kupata nafuu Mahakamani.

“Lengo la masharti ya kifungu kipya cha (2) ni kufafanua kwa uwazi maudhui yaliyokusudiwa katika kifungu cha 4 kilichopo sasa pamoja na Ibara ya 30(3) ya Katiba ambavyo kwa pamoja masharti ya kifungu na Ibara hiyo yalikusudia kutoa haki ya kuhoji ukiukwaji wa masharti ya Ibara hizo kwa mtu aliyeathiriwa na kuvunjwa kwa haki husika.”

“Kwahiyo, Kamati ilijiridhisha, maneno “has affected such person personally” ni ya msingi kuwepo katika kifungu kinachopendekezwa. kwa mantiki hiyo, Kamati inakubaliana na mapendekezo ya Serikali kama yalivyo kwenye Ibara ya 7(b) ya Muswada,” amesema.

Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania

Akiendelea kusoma muswada huo, Profesa Kilangi amesema, katika Sheria ya Masuala ya Rais, Sura ya 9, Muswada unalenga kufanya marekebisho katika Kifungu cha 6 ili mashauri dhidi ya Rais kwa mambo anayodaiwa kuyatenda yeye binafsi kama raia yaliyoruhusiwa kufunguliwa dhidi yake kwa mujibu wa Ibara ya 46(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yafunguliwe baada ya kutoka madarakani.

“Kifungu cha 7 kinapendekezwa kurekebishwa ili mashauri yoyote dhidi 
 ya Rais yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Lengo la marekebisho haya ni kuwa na maudhui ya dhana ya kinga dhidi ya Rais ambayo ni kulinda hadhi ya Rais na nafasi yake,” amesema Profesa Kilangi

Profesa Kilangi amesema, katika Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi, Sura ya 223, Muswada unakusudia kufanya marekebisho kwa kuongeza kifungu kipya cha 20A ili kuweka katazo kwa wamiliki halali wa silaha na risasi kuhamisha silaha hizo kwa watu wasioruhusiwa kumiliki silaha hizo.

“Lengo la marekebisho hayo ni kuhakikisha kuwa kwa wakati wote silaha na risasi zinakuwa chini ya mmiliki halali,” amesema

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!