Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mtifuano utakavyokuwa majimbo nane ya uchaguzi
Habari za Siasa

Mtifuano utakavyokuwa majimbo nane ya uchaguzi

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, kimetangaza orodha ya wagombea ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020, huku mchuano mkali ukitarajia kuonekana kwenye majimbo nane. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea). 

Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya chama hicho, iliyokutana leo Alhamisi tarehe 20 Agosti 2020, chini ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli, imefanya uteuzi wa wagombea 264 wa majimbo na wabunge wa viti maalum.

MwanaHALISI Online linaweza kuripoti kuwa katika orodha iliyopitishwa, mchuano mkali unatarajiwa kuwa katika majimbo ya Tarime Vijijini, mkoani Mara na Kawe, jijini Dar es Salaam.

Katika jimbo la Tarime Vijijini, mchuano utakuwa kati ya Mwita Mwaikabe Waitara, anayegombea nafasi hiyo kupitia CCM na John Heche, anayewania nafasi hiyo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Waitara alikuwa mbunge wa Ukonga kupitia Chadema katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.

Mwaka 2018, Waitara alitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na CCM na kupitishwa tena kugombea nafasi hiyo. Alishinda.

Kwa sasa, jimbo la Tarime Vijijini, linaongozwa na Heche, ambaye tayari amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wawili hao, kila mmoja na kwa nyakati tofauti, wamekuwa wakijinasibu kuibuka mshindi.

Nako katika jimbo la Kawe, mchuano mkali unatarajiwa kati ya Halima James Mdee, anatetea nafasi yake kupitia Chadema na Askofu wa Kanisa la Ufufuo NA Uzima, Josephat Gwajima.

Jijini Mbeya, jimbo hilo litakuwa na hekaheka ya hapa na pale kwa Dk. Tulia Ackson ambaye alikuwa naibu spika katika Bunge lililopita na mbunge anayetetea nafasi yake, Joseph Mbilinyi (Sugu).

Sugu amekuwa akisema, haoni wa kumwondoa kwenye jimbo hilo. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Sugu aliongoza kwa kura kati ya wabunge wote waliotangazwa kushinda uchaguzi huo.

Katika jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro, mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei na mwenyekiti wa taifa wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Mbatia alishinda kwa kupata kura 60,187 dhidi ya Innocent Shirima (CCM), aliyepata kura 16,617, huku mwanasiasa mwingine mkongwe, Augustine Lyatonga Mrema, akiambulia kura 6,416.

Mbatia amepata kuwa mbunge wa Vunjo kati yam waka 1995 hadi 2000 na 20015 hadi 2020. Mwenyewe amewahi kunukuliwa akisema, “Dk. Kimei, ni dhaifu mno.”

Katika jimbo la Arusha Mjini, mchuano mkali zaidi unatarajiwa kuwahusisha aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (CCM) na mbunge anayetetea nafasi yake, Godbless Lema (Chadema).

Tayari Lema amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, huku akisema, “siendi kugombea, nakwenda kushinda.” Kwa mujibu wa Lema, haoni yeyote wa kumng’oa kwenye ubunge wake.

Shughuli nyingine pevu itakuwa jimbo la Tunduma, mkoani Songwe, pale ambapo David Silinde (CCM) ambaye alikuwa kada wa Chadema na mbunge wa jimbo hilo mwaka 2005- 2010, kabla ya kuhamia Momba kisha kuhamia CCM, atakapochuana na Frank Mwakajoka (Chadema).

Mwakajoka amekuwa mrithi wa Silinde katika jimbo hilo mwaka 2015 hadi 2020 na ameapa kutetea nafasi yake kwa “gharama yoyote.”

Mkoani Kilimanjaro, mchuano mwingine mkali utakuwa katika jimbo la Rombo, ambako Joseph Selasini, anatarajiwa kuwa na kibarua kigumu cha kutetea nafasi yake.

Katika uchaguzi huu, Selasini ambaye anatetea nafasi hiyo, kupitia NCCR- Mageuzi, atakumbana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda (CCM).

Jimboni Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), atakuwa na shughuli pevu dhidi ya Jesca Msambatavangu (CCM).

Msambatavangu amewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa. Ameapa kulikomboa jimbo hilo kutoka mikononi mwa upinzani tangu mwaka 2010.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!