Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mtetezi wa JPM awavuruga Kinana, Makamba
Habari za SiasaTangulizi

Mtetezi wa JPM awavuruga Kinana, Makamba

Spread the love

KIGUGUMIZI cha Serikali ya Awamu ya Tano kumchukulia hatua Cyprian Musiba, anayejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Rais John Magufuli, sasa kinahojiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Abdurahman Kinana, Yusuf Makamba ambao ni makatibu wakuu wastaafu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanahoji udhaifu uliokikumba chama na serikali yake kwa kushindwa kulinda heshma yao na wananchi wengine kutokana na kuchafuliwa pia kudhalilishwa na ‘mtetezi wa Rais Magufuli’.

Makamba aliyehudumu nafasi hiyo kuanzia 2007-2011 na Kinana aliyehudumu kuanzia 2012-2018, tarehe tarehe 14 Julai 2019 walimwandikia barua Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM wakilalamikia kuchafuliwa na Musiba huku serikali na taasisi zake zikikaa kimya.

“Tuliamini kwamba pale anapojitokeza mtu hadharani na kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu na huku mtu huyo akijinasibisha na serikali pamoja na rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM basi hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma,” inaeleza sehemu ya tamko la Mzee Makamba na Kinana.

“Kwa bahati mbaya viongozi wetu hawakuchukua hatua yoyote kuhusu jambo hilo. Na zaidi mtu huyu ameendelea kuwadhalilisha na kuvunjia heshima viongozi wastaafu na wengine katika jamii.”

Mzee Kinana na Makamba wametoa tamko hilo, baada ya Musiba kuwatuhumu kwa zaidi ya mara mbili, kwamba wanahusika na vitendo vya kumkwamisha Rais John Magufuli kutekeleza majukumu yake.

“Kwa sasa Watanzania wote wanajua kuwa haya anayosema mtu huyu kuhusu watu mbalimbali siyo ya kwake, yeye anatumwa kutekeleza maagizo tu na kutumika kama kipaza sauti.Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu, katika mazingira hayo hatuwezi kukaa kimya,” wamesema.

Kufuatia kadhia hiyo, Mzee Makamba na Kinana wamemwandikia barua Mzee Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu la chama hicho, kumlalamikia kitendo cha Musiba kuwachafua viongozi wastaafu.

“Tunasikitika kwamba Musiba licha ya kuwatuhumu na kuwakashifu Watanzania wenzake viongozi na watendaji wa serikali, ameachwa akitamba jambo linaloashiria kwamba anakingiwa kifua , hata anapotumia lugha za vitisho na za kuhatarisha usalama wa raia hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake,” wamesema.

Makatibu hao wastaafu wa CCM wamesema wamechukua hatua hiyo badala ya kwenda mahakamani, ili wazee wa CCM watumie busara zao katika kushughulikia jambo hilo.

“Tunafanya hivyo kwa kuzingatia katiba ya CCM , tumewasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kushughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja mshikamano na utulivu ndani ya chama na nchi,” wamesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!