Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mtego anaoundiwa Maalim Seif Z’bar wavuja
Habari za Siasa

Mtego anaoundiwa Maalim Seif Z’bar wavuja

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), visiwani Zanzibar kinahaha namna ya kumzima Maalim Seif Sharif Hamad, Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Taarifa kutoka kwa mmoja wa maofisa wa CCM visiwani humo imeeleza, chama hicho kinapanga kupeleka hoja ya kubadili vigezo vya kugombea urais visiwani humo, kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Suala la kupeleka pendekezo lipo maana kwa upande wetu hali si hali” amesema ofisa huyo na kuongeza: “njia raisi ya kumdhibiti Maalim ni kumzuia kuingia kwenye uchaguzi.”

Amesema, CCM Zanzibar wanajua nguvu ya Maalim Seif hasa katika kipindi hiki ambacho chama hicho visiwani humo kina msigano wa chini kwa chini kuelekea uchaguzi mkuu.

“Mbinu nyingi zimefanyika kumkatisha tamaa Maalim Seif, lakini zimeshindwa kufanikiwa, hakati tamaa. Sasa hivi anaonekana kutokuwa tayari kukubali iwapo hatoshindwa kihalali, nadhani dhamira ni kwamba asiingie kabisha kwenye uchaguzi ujao,” ameeleza.

Hoja hiyo ilipangwa kupelekwa kwenye Baraza la Wawakilishi visiwani humo lililoanza kuketi leo tarehe 5 Februari 2020.

Omar Said Shaaban, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ya chama hicho, amesema wanafahamu taarifa hizo na kwamba, chama chao kinaendelea kuwa makini na kila taarifa kinayopokea.

Omar ambaye pia ni wakili wa kujitegemea katika Mahakama Kuu Zanzibar, amesema tayari CCM imewabebesha mzigo wajumbe wake wa Baraza la Wawakilishi wa kushawishi mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ya Zanzibar, ili kuzuia kundi kubwa la wananchi haki ya kugombea uongozi.

Huku akionesha karatasi aliyosema ni ajenda za kikao cha Kamati ya Wawakilishi wa CCM katika Baraza la Wawakilishi, Omar amesema kunaandaliwa hoja binafsi ya kuwasilishwa kwa lengo la kutimiza matakwa ya CCM.

Amesema, mwakilishi wa Kwamtipura mjini Zanzibar, Hamza Hassan Juma, ndiye anayetarajiwa kutumika kuwasilisha hoja hiyo ya kutaka mgombea urais, uwakilishi na udiwani sharti awe ametimiza angalau miaka miwili kuwa mwanachama wa chama kile anachotaka kimdhamini.

Sifa za wagombea nafasi hizo kwa mujibu wa sheria hiyo zinaelekezwa kwenye vifungu 43 kwa urais, 44 kwa uwakilishi na kifungu cha 45 kwa udiwani.

“Naomba niwaambie CCM, mpango wanaotaka kuutekeleza utakuwa ni kituko na wanahitaji kuutafakari mara mbili kabla ya kuibua hoja hiyo barazani,” alisema Omar na kuhoji:

“Inakuwaje Mzanzibari mmoja mwenye kutokana na chama kimoja cha siasa, mwenye kugombea eneo moja la siasa awe na uanachama wa miaka mitatu kwenye uchaguzi wa wabunge lakini sifa hiyo asiwe nayo kwenye uwakilishi?”

Amesema, ni vema Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Said Hassan Mzee, ajiepushe na mpango huo kwa sababu “hauna tija yoyote zaidi ya kutaka kukandamiza haki za watu zilizobainishwa kwenye Katiba ya Zanzibar.

“Hebu tujiulize, mabadiliko haya yana tija kiasi gani kwa nchi hii? CCM badala ya kutumia Baraza la Wawakilishi kuisimamia serikali na kubuni mbinu sahihi za kusimamia uchumi ambao kila siku unaporomoka, watu hawana uhakika wa kipato, vijana hawana ajira, wao wanaitumia kudhibiti nguvu ya upinzani,” amesema.

Maalim Seif aliwahi kutoa tuhuma hizo miezi michache iliyopita, miongoni mwa viongozi waliomtuhumu kusema uongo ni Dk. Bashiru Ali, Katibu Mkuu wa CCM.

Chama cha ACT Wazalendo kinajiandaa na Mkutano Mkuu wa kwanza tangu kumpokea mwanasiasa huyo maarufu nchini na kundi kubwa la wafuasi.

Tayari chama hicho kimekamilisha uchaguzi wa viongozi ngazi ya matawi mpaka majimbo. Mwishoni mwa wiki, Maalim Seif alichukua fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho na juzi msaidizi wake mkuu, Babu Juma Duni Haji alifanya hivyo akiwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!