TAASISI ya Kinamama na Kinababa kwa Mageuzi ya Jamii (MPFCR), imewataka vijana kuacha matumizi ya mihadarati kutokana na madhara yake. Anaripoti Kamote Martin … (endelea).
Pia imewataka vijana hao kuacha kulalamika kukosa ajira na badala yake watumie fursa zinazowazunguka ili wajipatie kipato.
Emmy Jahai, Mkurugenzi Mtendaji wa MPFCR ametoa kauli hiyo leo tarehe 4 Oktoba 2019, wakati wa zoezi la usafi na kupanda miti katika Kituo cha Polisi cha Kigamboni.
Amesema, vijana wengi hawajishughulishi na kazi za kuwaingizia kipato na kwamba, wanakaa vijiweni huku wakilalamika kukosa ajira.
Amesema, taasisi yake imekua ikifanya jitihada ya kuwasaidia vijana wenye uraibu wa madawa ya kulevya, ambapo baadhi yao wameacha.
“Zoezi tunalofanya leo ni kufanya usafi, kupanda miti pamoja na kutoa cheti cha heshima kwa mkuu wa kituo hiki cha polisi (ASP Said Msisiri), ikiwa ni kutambua mchango wake wa kuthamini na kujali jamii katika kupambana na vitendo vya uhalifu hapa Kigamboni,” amesema Jahai.
Awali, akisoma risala baada ya zoezi hilo, Dorah Mushi ambaye ni mratibu wa zoezi hilo amesema, awali kulikua na maeneo mengi hatari kwa watu kutekwa mchana, lakini kwa sasa ulinzi na usalama umeimarishwa.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni Midizini, Tungi, Minazi Mikinda, Vijibweni, Feri Bandari, Geza Ulole, Maeneo ya Beach.
ASP Msisiri amesema, Jeshi la Polisi litaendelea kupambana na baadhi ya mawakala wa madawa za kulevya.
Amesema, MPFCR inapaswa kuigwa kwa mchango wake wa kuanzisha kituo cha kuwahudumia watu wenye uraibu wa madawa ya kulevya (Sobber’s House).
Amina Mbonde, mmoja wa waathirika wa madawa ya kulevya ameshauri vijana kuacha matumizi ya dawa hizo kwa kuwa yana madhara mengi ikiwa ni pamoja na matatizo ya akili n ahata kifo.
Leave a comment